Inatoka toleo lilopita
Hapa hapahitaji kusherehesha sana, mimea iliyotajwa katika aya hii ni tofauti, mingine inafyonza sukari, mingine wanga, mingine mafuta n.k. kutoka kwenye udongo, kwa ajili ya binadamu, mwenye mwili wa udongo.
Katika aya nyingine, Allah anazidi kutupasha jinsi alivyomuumba mtu, kwa kusema:
(Allah, mwingi wa Rehema) Amemuumba
mtu kwa udongo wa ufinyanzi kama vyombo vya udongo" (Qur-an 55:14)
Picha tunayoipata hapa ni kwamba mtu aliumbwa kwa kufinyangwa kama sanamu (fakh-khaari). Sanamu hii ilikuwa haijatimia mpaka pale Allah (sw) alipoipa uhai, kama tunavyoona tena katika Qur-an:
Na (zingatia) Mola wako alipowaambia Malaika: "Hakima Mimi nitamuumba mtu kwa udongo mkavu, wenye kutokana na matope meusi yaliyovunda. Basi nitakapomkamilisha na kumpulizia roho yangu, basi mumuangukie kwa kumtii". (Qur-an 15:28 - 29).
Hapa ndio tunapata habari kwamba baada ya Allah (sw) kumuumba mtu kwa udongo kama sanamu, akampulizia roho, akampa uhai, na ndipo mtu akawa mtu kama tunavyomfahamu, anaona, anasikia, anasema, n.k.
Hivyo hapa ndipo tunapata jibu muafaka
la asili ya binadamu, kwamba ana asili mbili:
1. asili ya UDONGO.
2. asili ya ROHO
Tumeongelea uhakika wa mtu kuumbwa kwa udongo, kwa kutumia vigezo. Ama uhakika wa roho ni mgumu kuuelezea, kwani hata watu walipokuwa wakimuuliza Mtume Muhammad (saw), Allah (sw) akamwambia jinsi ya kuwajibu, kwamba:
13
"Na wanakuuliza kuhusu roho, sema (uwaambie) hiyo roho inatokana na amri ya Mola wangu". Na hamkupewa katika elimu yake (hiyo roho) ila kidogo tu" (Qur-an 17:85).
Mtu anaweza, kwa mfano, kuona kifaranga cha kuku, kinatembea. Mara anakiona kimetumbukia kwenye beseni la maji, kinahangaika akaamua kwenda kukiokoa, lakini anapokitoa kimeshaathirika, kinakufa. Ndipo mtu mwenye akili anapojiuliza, kuna tofauti gani kati ya kifaranga kile kilichopita kikiwa hai, na hiki ambacho hakina uhai? Kumbe basi kuna kitu kinaitwa uhai ndani ya kiumbe, kitu hiki kinaweza kiwepo au kisiwepo. Mara ya kwanza uhai ulikuwepo ndani ya kifaranga, na sasa haupo. Je uhai ule umeenda wapi? Hapo ndipo penye kitendawili. Hata sayansi imegonga mwamba. Allah (sw) ndiye mjuzi wa habari hii.
Hata hivyo, kuna maelezo ya muhimu kuhusu hii roho. Tunafahamu kuwa ile roho ndiyo ilimpa mtu uhai. Lakini tunafahamu pia kwamba si binadamu peke yake ndiye mwenye uhai. Kuna viumbe vingine ambavyo vinaitwa viumbe hai. Je vinatofautiana vipi na mtu. Hapa pia pana maelezo mazuri ya kumfanya mtu ajitambue.
Kuna aina kuu tatu za uhai. Wataalamu wa kiingereza wanapenda kutumia neno soul.
1. Vegetative soul (Uzima wa uoto); Uzima huu ni wa kuota, na una nguvu za aina tatu; kuzaliana, kukua na kuhitaji chakula.
2. Sensitive soul (uzima wa hisia): Huu ni uzima ambao unahusiana na milango ya fahamu. Viumbe wenye uzima huu wana uwezo wa kuona, kusikia, kuonja, kuhisi kwa kuguswa, na vile vile vina uwezo wa kusogea kutoka mahala pamoja hadi pengine (bila ya kutiwa ufunguo).
3. Diannoetical soul (uzima wa kiutambuzi): Huu ni uzima ambao unahusiana na utambuzi wa hali ya juu wa mambo. Viumbe wenye uzima huu huwa na uwezo wa hali ya juu wa kufahamu mambo, na kuyawekea kumbukumbu, na kutafuta ufumbuzi. Vile vile ni viumbe wanaofundishika, na hawaishi kwa kutegemea hisia za maumbile tu.
Kwa mgawanyo huu, ndipo tunaweza kuwapata viumbe tofauti, na tukaipata nafasi ya binadamu.
Kwanza kabisa kuna mimea, ambayo yenyewe imejaaliwa uzima ule wa kwanza tu (uzima wa uoto) na ina uwezo wa kukua, kuzaliana na kuhitaji chakula tu.
Pili kuna wanyama na wadudu. Hawa wana uzima wa aina mbili. Kwanza ni ule uliomo kwenye mimea, yaani wao pia huzaliana, hukua na huhitaji chakula, lakini pia wana ule mwingine unaohusisha milango ya fahamu (uzima wa hisia) na huweza kusogea kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Mwisho yupo binadamu. yeye
ana uzima wa aina zote. Wa kwenye mimea, na wa kwenye wanyama, ila pia
ana ule wa ziada wa tatu, unaomfanya kuwa tofauti na mimea na wanyama,
hasa kimajukumu, uzima wa utambuzi. Ni kwa nini Muumba kampendelea? Ipo
sababu, tutaiona katika kijitabu cha pili, Inshaallah.
--
|
|