Ijumaa iliyopita, Waislamu walipata kipigo kingine kutoka kwa polisi wa serikali ya CCM. Kama ilivyokuwa Mwembechai, kipigo hiki nacho kilianza na kuvamiwa Msikiti ambamo Waislamu walikaa kutafakari mwenendo wa nchi baada ya kuzuiliwa kuonesha hasira zao hadharani kwa kufanya maandamano ya amani kupinga kuzuiliwa wanafunzi Waislamu kuvaa mavazi ya stara na kuhudhuria swala ya Ijumaa. Makala haya yanajaribu kuoanisha vitendo vya dhulma vilivyofanyika wakati wa utawala wa makaburu Afrika ya kusini na mwenendo wa jeshi la polisi la nchi iliyohuru na iliyokuwa mstari wa mbele kupinga dhulma ya watu weupe kusini mwa Afrika. Na Mohamed Hussein.
AMANDLA!! Malimule!! Malimule!! De Afrika!! Ni mbiu ya mwamko uliochochea hamasa kwa waafrika kuanza kuuelekea ukombozi.
"Wanakuogopeni kwa sababu ninyi ni vijana, wanakugopeni kwa sababu ninyi ni kizazi cha baadaye ambacho kitachokuwa huru. Nami natamani ningekuwa hai kuiona siku hiyo mpya", anasema mchungaji mmoja mbele ya majeneza yaliyobeba maiti za wanafunzi waliouawa na utawala dhalimu wa makaburu wakati ule nchini Afrika kusini.
Juni 13, 1976 wanafunzi wa shule za sekondari Jimbo la Soweto walikutana katika kitongoji cha Naledi ambapo waliazimia kufanya maandamano juni 16, mwaka huo huo kupinga utawala wa kidhalimu wa makaburu na zaidi azimio lake la kukifanya kiafrikana(lugha ya weupe wachache) kuwa lugha rasmi ya masomo nchini humo. Kweli, saa mbili asubuhi ya juni 16 wanafunzi walianza kukusanyika katika shule ya sekondari ya Orlando west, kuanza maandamano ya amani kuelekea uwanja wa mpira miguu. Ilipofika saa tatu na nusu wanafunzi waliokisiwa kufikia 15,000 walikuwa mitaani wakiwa wamebeba mabango yaliyokuwa na maandishi "Down with Afrikaans", Afrikaans-Language of Opressors!" na Revoke Afrikaans" .
Kinyume na matazamio yao kwamba maandamano yale yangekuwa ya amani, vijana hawa walikabiliwa na nguvu kubwa ya kijeshi iliyodhamiria kujeruhi, kukamata na kuua ili kuzima kile walichokiita "vurugu". Mabomu ya machozi yalipigwa, virungu vilitembezwa na risasi zilifyatuliwa kuwalenga mashujaa wale. Ili kujitetea vijana nao walianza kurusha mawe, kuchoma magari ya serikali na kuanza kuwasaka vibaraka miongoni mwao, wale "malipyoto wa watu weupe", wale "wanaowauza ndugu zao", "wale waasi waliokuwa miongoni mwao", wale waliokula na kunywa kutokana na damu zao", wale waliosababisha watu wazima wa Soweto kuwa wafungwa magerezani, wale walisababisha vijana kuikimbia nchi na wale walioufanya mji wa Soweto kubaki katika hali ya ukiwa ambapo ni akina mama na watoto tu waloonekana.
Katika tukio hilo la kuhuzunisha mamia ya wanafunzi waliuawa, wengine kujeruhiwa na zaidi ya wanafunzi 8,000 kurundikwa magerezani wakipata mateso makali.
"Sikusikia polisi ikitoa ilani kutawanya waaandamanaji kabla ya kuanza kupiga mabomu ya machozi kuukabili umati mkubwa wa wanafunzi uliokuwa ukiimba", aliripoti mwandishi wa gazeti moja nchini Afrika Kusini ambaye alikuwepo kwenye eneo la tukio akijaribu kuonesha unyama wa makaburu katika tukio hilo.
"Shahidi wa kwanza katika mauaji yale alikuwa kijana Hector Peterson aliyekuwa na umri wa miaka 13.
Walioshuhudia tukio la kuuawa kijana huyu walieleza kwamba walimuana polisi mmoja akifyatua bunduki kumpiga kijana huyu ambaye alianguka na kufa pale pale.
Kama kawaida ya madhalimu, Waziri wa sheria wa wakati ule Kaburu Kruger alisimama bungeni kutetea hatua ya kinyama ya polisi, waziri huyo alisema " Police "fired in-self defence" because "their lives were in danger" yaani Polisi walirusha risasi kujitetea kwa sababu maisha yao yalikuwa hatarini").
Maneno haya alimkasirisha kila mpenda haki duniani, wale waliokuwa na mioyo jasiri walianza kuyatoa muhanga maisha yao kuondoa ubaguzi, kupigania utu, heshima, haki na usawa kwa watu wote.
"Mtatuua, lakini hamuwezi kutusimamisha, tunakuja. Mtatuua, lakini tutaishi tena (kizazi kijacho kitakuwa huru). Tunakuja, noeni mikuki yenu. Vita iko milangoni mwenu, tunakuja".
Hizo ni baadhi ya nyimbo zenye hisia na hamasa ya kutaka kujikomboa. Ni matamshi yaliyokuwa yakitolewa na wenyeji wa Afrika Kusini zama za ukandamizaji wa makaburu.
Vijana walioamshwa na mauaji yale walitamani zaidi kufa kuliko kuishi chini ya utawala dhalimu wa makaburu.
"I want to die like him than to live like you", kijana (msichana) mdogo wa shule alimkabili mama yake kumueleza maneno hayo huku akisifu ushujaa wa baba yake aliyekufa katika harakati akiwa katika kambi iliyowaandaa wapiganaji wa Soweto nchini Msumbiji.
Mama aliyekuwa mtumishi katika makazi ya weupe alitafsiri maneno hayo kuwa sawa na ndoto ya mchana ambayo humpotezea muda mhusika. Alijibu kwa woga kuwa kuanzisha mapambano na watawala wakati huna silaha mkononi ni kujiangamiza.
Ni dhahiri ujumbe wa msichana kwa mama uliashiria kutokuwa tayari kuishi chini ya manyanyaso, kukandamizwa na kudhalilishwa huku ukifanywa mbumbumbu anaetakiwa kufunga mdomo wakati wenye fursa zao wakiendelea kuhodhi rasilimali na sekta muhimu na kuponda maisha.
Kama asemavyo msichana Leleti katika igizo la "Sarafina" kuwa umma unaposimama kuuelekea ukombozi hakuna bunduki wala bomu litakalouzuia. Kufa katika harakati hizi ndiyo ustawi wa dhamiri, azma na mwako wa ukombozi unaotokana na chuki dhidi ya udhalimu.
Moja ya tuzo kuu kwa mwanaharakati wa kweli ni ushujaa usiosahaulika kwa vizazi vinavyofuata. Hatasahaulika katika mabuku ya historia miaka kadhaa baadaye. Kufa ni lazima hakuna njia ya kukwepa kifo lakini ni kifo gani kingekuwa bora kwako?
"Wengi wangependa kuambiwa "He dies because of struggles (amekufa katika harakati za ukombozi)"
Kiini cha hali ya pilika pilika iliyokuwepo Afirika ya Kusini ni maisha ya dhiki, manyanyaso, kejeli na ukandamizaji wa utawala wa makaburu. Jimbo la Soweto lilitafsiri maisha ya mwenyeji wa Afrika Kusini yalikuwaje. Bidhaa muhimu kama chumvi, sukari na kadhalika zilikuwa tabu kuzipata mkazi wa Soweto ambaye asubuhi alitakiwa kuwahi kibaruwani ambako baada ya mtulinga wa mchana kutwa aliambulia ujira mdogo kabla hajapanda gari moshi jioni kurudi Soweto. Nyumba nyingi hazikuwa na kifungua kinywa asubuhi. Familia nyingi zilirundikana ndani ya vijibanda vilivyokuwa na nafasi finyu kama mifugo. Watoto kwa wakubwa walipangana kama wafungwa kuweza kujipatia japo lepe la usingizi usiku.
Mfumo wa elimu uliwekwa katika namna ambayo "msomi" mweusi angekuwa kibaraka wa watawala. Hivyo Elimu haikuweza kuwa chachu ya ukombozi wa wananchi wale kama anavyoeleza mwanafunzi mmoja wa kambi ya Mazimbu wakati ule kuwa "elimu ya utawala wa makaburu inatumika kuwagawa wananchi kimatabaka, msomi mweusi haoni sababu ya kukaa pamoja na ndugu zake kujadili yanayowasibu, lakini msomi huyo huyo hakuwa na thamani yoyote mbele ya mtu mweupe hata kwa kiwango gani cha elimu alichonacho".
Makundi ya wanafunzi na vijana yaliijadili kwa mapana hali hiyo ya udhalili na kukandamizwa. Wako waliopendekeza "wajielimishe (wasome) kwanza kabla ya kuanza mapambano. Wapo walioona ni kupoteza muda kufanya hivyo, kwa maana ni bahati nasibu kuweza kusalimika na vishawishi vya ajira, mshahara mzuri na makazi mazuri, kwa hiyo ingechukuwa karne nyingi kuweza kuwapata "masumbuka" wengi katika chujio lile la kitabaka (elimu).
"Fungua macho yako (amka), elimu hii inawatoa mitaani ndugu zetu", anasema kijana mmoja mkereketwa wa harakati.
Utawala wa makaburu ulikuwa wa vitisho na kamata kamata iliyosababisha magereza kujaa mahubusu na wanaume wengi kuzikimbia familia zao. "The old men are prisoners. The young men have fled, only women and babies in Soweto", wanaimba vijana wadogo wa Soweto, In umlazi na in kwa mashu wakiwa na maana "watu wazima wanaume wamekuwa wafungwa magerezani, vijana wamekimbia familia zao, wengine wamehama nchi. waliobakia Soweto ni wanawake na watoto.
Watu, majumba na mikusanyiko ilizingirwa na polisi wa makaburu, wananchi wakapigwa, kujeruhiwa na kuuawa. Mitaa ilivamiwa na makachero weusi kwa weupe waliodhamiria kunyamazisha harakati zozote dhidi ya serikali.
Wananchi walizolewa na kupakiwa kama mifugo katika makarandinga. Watu wengi walikata tamaa waliona kwamba isingewezekana utawala kusalimu amri kwa wanyonge wasio na silaha. Ilikuwa kama ni kujiua kujaribu kupambana na ukuta mnene usioweza kupenywa kwa vyovyote.
" Watu wamepigwa bumbuwazi, ganzi la kukandamizwa limewakolea vilivyo, ni wale wenye kusema "tutafanyeje, wenzetu wana silaha sisi wanyonge," anasema kijana mmoja kwa hasira.
Katika hali hiyo hapakuwa na budi umma kutoa kilio chake, Taifa la weusi lilipaswa kulia kwa kuwa lilipotezewa watu muhimu na nguvu kazi kubwa.
Lakini ilisikitisha kwamba baadhi ya weusi walionufaika na mfumo huo kutokana na utumishi serikalini nao walikuwa na mchango mkubwa katika kupiga vita ndugu zao.
Hawa walitumika ipasavyo kuwafitini wenzao kwa watawala.
Wanafiki hawa waliuwauza ndugu zao kwa thamani ndogo. Walikula kutokana na damu za ndugu zao.
Watu waliteswa na kuuawa kwa sababu yao. Nchi ilikufa kwa sababu yao. Ni "traitors among us" nyimbo ziliwakabili walafi hawa zikimaanisha waasi waliokuwa wakitumiwa na madhalimu kuwadhulumu ndugu zao.
"You who talk with white men" (Nyinyi malipyoto wa watu weupe).
"You who sell your own people" (Nyinyi mnaowauza ndugu zenu).
"Our land is dying" (Nchi inakufa).
"Our people are dying" (Watu wanakufa).
"Trators among us" (Ni waasi mlio miongoni mwetu).
"Feed on our blood" (Mnakula na kunywa kutokana na damu).
"The nation is crying" (Umma unalia).
"The old men are prisoners" (Watu wazima wamekuwa wafungwa magerezani)
"The young men have fled" (Vijana wamekimbia majumba na nchi).
"Only women and babies in Soweto" (Ni wanawake na watoto tu waliobaki Soweto).
|
|