Barua
 
 

Huku ndiko kushughulikia matatizo ya Waislamu?

Ndugu Mhariri

KATIKA kile kinachoonekana kama kupotea hisia za Waislamu ya unyimwaji haki za kimsingi ndani ya nchi yao unaofanywa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuna gazeti moja linalotolewa kila siku lilizipa uzito wa juu habari zinazoelezea kuwa serikali imeanza kuyashughulikia matatizo ya Waislamu likimnukuu Mhe. Rais Mkapa alipokuwa akiwahutubia Watanzania kupitia Mkutano Mkuu wa Bakwata uliofanyika Dodoma hivi karibuni ambapo yeye alikuwa mgeni rasmi katika Jitimai hiyo ya Kiislamu.

Liliandika kwamba Rais Mkapa amesema kuwa serikali yake imeshaanza kuyashughulikia matatizo ya Waislamu. Hakukuhitajika PhD wala cheti cha shule ya msingi kugundua kuwa habari ya gazeti hilo ilikuwa ni kuwakejeli Waislamu.

Sio lengo la barua hii kujaribu kuzungumzia au kushangazwa na propaganda za baadhi ya magazeti yetu ya hapa nchini yanaporipoti habari zinazohusu Waislamu. Lakini wasiwasi wangu mdogo kama sio mkubwa upo katika namna ya hicho kinachoitwa ushughulikiwaji wa matatizo ya Waislamu jinsi unavyoendeshwa.

Kwa mfano, serikali kuendelea kumsaka Katibu wa Kutetea Haki za Waislamu kwa kule kuitaka serikali iunde tume huru kuchunguza mauaji ya Mwembechai na kumwacha Paroko Lwambano na wale wote walioamrisha kuua, ndiko kushughulikia matatizo ya Waislamu?

Jumamosi na Jumapili ni siku za mapumziko zilizolengwa kuwapa nafasi zaidi Wakristo kufanya ibada zao bila matatizo lakini Ijumaa muda wa masaa mawili tu Waislamu kwenda Msikitini tunaambiwa na Baraza Kuu la Kutunga Sheria nchini (Bunge) kuwa kuomba wasaa kama huo siku ya kazi ni kuleta udini, je, hivi huku ndiko kushughulikia matatizo ya Waislamu?

Waislamu waliandaa maandamano ya amani kupinga kauli za Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya Waislamu, kabla ya hata hayo maandamano yenyewe polisi wa serikali wakawa wanapita mitaani na Misikitini kuwapa mkong'oto raia yeyote aliyeonekana anglau ana alama ya Uislamu. Je, askari kuingia Msikitini na mabuti kisha kuwakamata Waislamu na kuwasulubu kama vile tupo Bosnia ndiko huku kushughulikia matatizo ya Waislamu?

Pamoja na ukweli kwamba Nabii Issa bin Mariam (Yesu) si Mungu wala si Mwana wa Mungu lakini wenzetu Wakristo wamekuwa mara nyingi wakiandamana bila ya bughudha na huku wakijigamba kuwa Yesu ni Mungu Yesu ni Mwana wa Mungu, kwa Waisalmu hali haiko hivyo. Mtu mmoja tu wala hakuandamana na wala hakuandika katika gari, kaandika kwenye baiskeli yake kuwa Yesu si Mungu, kakamatwa na amevunguliwa ksei eti anajeruhi imani za wengine! Je, nako huku ndiko kushughulikia matatizo ya Waislamu?

Kwa kumalizia ni kwamba ninavyofahamu mimi hakuna Mbunge yeyote aliyekwenda bungeni kwa tiketi ya dhehebu fulani la dini, bali Wabunge wote wanayawakilisha majimbo yao ya uchaguzi ambayo bila ya shaka yana mchanganyiko wa wapiga kura.

Sasa ikiwa Wabunge wametoa kauli inayowakataza Waislamu wasifany ibada ya swala wala kuvaa mavazi ya stara wakati Waislamu hao ni sehemu ya wapiga kura, unafikiri wachukue hatua gani ili kuonyesha serikali yao kuwa haitendi haki zaidi ya kufanya maandamano ya amani? Na ni ushahdi gani wa kutosha kupita ule wa Waislamu kupigwa na kujeruhiwa ndani ya Misikiti yao kila wanapojaribu kudai haki zao anaotaka apelekewe Mheshimiwa Rais Mkapa?

Mtagaluka Rashid,
Dar es Salaam.


Betty Mkwasa, majambia uliyaona peke yako?

Ndugu Mhariri

AKIWASILISHA ripoti yake juu ya suala la "mapambano ya polisi na Waislamu walioandamana" katika redio ya Sauti ya Amerika (VOA) siku ya Jumamosi Julai 31, mwaka huu saa 1:30 usiku, Betty Mkwasa mwandishi wa habari na mtangazaji wa vyombo vya habari vya IPP, alisema kUwa Waislamu waliokuwa wanaandamana walikuwa wakipunga majambia hewani.

Ni vigumu kujuwa habari hii aliipata wapi. Hayo majambia aliyaona peke yake? Je, aliona chumvi inayoongezwa na vyombo vya vingine vya habari ilikuwa haijatosha au ndio katika ule muendelezo wa kudai "Waislamu waingiza makontena ya silaha?

Jambo moja la kutia changamoto juu ya habari hiyo ni kuwa Betty ameyasema hayo siku moja tu baada ya bosi wake Bw. Reginald Mengi kuwaambia waandishi wa habari kuwa wafanyakazi katika vyombo vyake vya habari wako huru na wanafanya kazi yao kwa kufuata "ethics of truth" (maadili ya kusema ukweli). Je, Bw. Mengi anataka tuamini kuwa ethics of truth aliyoizungumzia kuwa nayo wafanyakazi wake ndIyo kama hii ya Betty Mkwasa?

H. Mrisho,
P.O. Box 129,
Kigoma.



Waandishi wa habari kuweni waadilifu

Ndugu Mhariri

BINAFSI niliyapitia magazeti huru yatolewayo kila siku kwa lugha ya Kiswahili matoleo ya Jumamosi na Jumapili Julai 31, mwaka huu na Agosti 1, mwaka huu. Habari zilizopewa uzito wa juu zilihusu maandamano ya Waislamu.

Jambo la kushangaza ni kuwa licha ya waandaaji wa maandamano kutoa taarifa rasmi ya nini lilikuwa lengo la maandamano, bado vyombo hivi viliripoti fotauti. Pia ni vigumu kuelewa kwanini gazeti moja linaripoti tukio moja katika kauli mbili tofauti.

Mfano, gazeti la Majira la Jumamosi linasema kuwa lengo la maandamano lilikuwa "kupinga amri ya serikali ya kuzuia wanafunzi kuvaa hijab mashuleni na kuhudhuria sala siku ya Ijumaa". Majira Jumapili linasema lengo lilikuwa "kudai Profesa angeshikilia msimamo wake wa awali wa wanafunzi Waislamu kuvaa hijab na kusali Ijumaa, pia kumuunga mkono Mbunge wa Kigamboni Kitwana Kondo aliyoyasema Bungeni kuwa wahubiri wanaosema Yesu sio Mungu wako sahihi".

Mtanzania Jumamosi linasema lengo lilikuwa "kupinga hatua ya baadhi ya Wabunge kumshinikiza Waziri Kapuya kuondoa kipengele cha udini kilichojitokeza katika hotuba ya Wizara yake". Lile la Jumapili linasema maandamano yalisababishwa na "vazi la hijab na kusali siku ya Ijumaa".

Gazeti la Nipashe Jumamosi liliandika lengo lilikuwa "kupinga kuzuiwa wanafunzi wa Kiislamu kuvaa hijab (wanawake) na kushiriki katika ibada". La Jumapili linasema lengo lilikuwa "Waislamu kudai kukerwa na hatua ya Waziri Kapuya kurekebisha maeneo yaliyogusa Uislamu katika hotuba yake bungeni".

Kwa mifano hiyo michache ni wazi kuwa yeyote aliyetegemea vyombo vya habari kujua nini hasa lilikuwa lengo la maandamano basi hakulijua.

Hivyo waandishi ni vema wakafanyakazi kwa kufuata maadili ya kazi yao badala ya kutanguliza chuki zao jambo ambalo linawashushia hadhi kitaaluma.

Said Bachinoni,
Box 35152,
Dar es Salaam.



Mwenziwe Makamba anasubiriwa

Ndugu Mhariri

MHESHIMIWA Yusuf Rajab Makamba amejiwekea rekodi ya pekee nchini hapa. Ambapo itamfanya asisahaulike katika historia ya Uislamu nchini. Yeye alikuwa kiongozi wa kwanza wa serikali ya CCM kuingia Msikiti wa Mwembechai baada ya Waislamu kuuliwa na kusema aliyoyassema bila ya kujali hisia za Waislamu bali akiwajali wazee wachache waliokusanywa kukabidhiwa Msikitini.

Wiki iliyopita wanawake Waislamu wakiwa ndani ya nyumba tukufu ya amani ya Mwenyezi Mungu, waliswagwa nje wakakabiliane na virungu, mbwa, risasi na mabuti ya polisi.

Bila kujali hawa ni Waislamu, ni wake za watu, ni dada za watu, ni watoto wa watu na ni binadamu. Waliowaswaga ni watu katika watu wa Msikiti. Pengine wakilenga kuwafurahisha polisi na waliowatuma polisi.

Wanachosubiri Waislamu ni kuona nani watapupia kuingia kwenye historia ya nchi kupitia tukio hili.

Mustafa Osman,
Kibaha,
Pwani.


Heri muaji na mchuna ngozi za watu
 

Ndugu Mhariri

KUPITIA TV niliona wale watu walioua na kumchuna ngozi mtoto wa shule kule Mbozi Mbeya.

Watu wale wamepandishwa kwenye gari la polisi kwa heshima bila ya kupigwa teke wala kirungu.

Juzi hapa watu walipokamatwa Msikitini na polisi ni kipigo kisicho kifani kikiwasindikiza mpaka mtu anaingia ndani ya gari. Hali inatufanya wengi tujiulize ni kigezo gani kinachotumika kuchagua polisi wa kwenda kwenye operesheni inayowahusu Waislamu?

Mbona wanaonyesha kuwa na chuki isiyo kawaida dhidi ya watuhumiwa?

Hatibu Senzia,
Same.


Mbukuzi Amir wa Waislamu sio wa Bakwata au Manyema

Ndugu Mhariri

HAKUNA mtu aliyewahi kusema kuwa Sheikh Juma Mbukuzi ni Amir wa Waislamu wa Manyema wala wa Bakwata. Yeye ni Amir wa Waislamu na hajawapora haki yao wale wa Bakwata na Manyema kuwa kuwa Amir wao.

Ruqaya Mussa,
Tandika,
Dar es Salaam.



Msiba; tena mkubwa sana
 

Ndugu Mhariri

Wakati mauaji ya halaiki yanafanyika kule Burundi, maelfu ya watu walikimbilia makanisani kupata hifadhi. Baadhi ya Maaskofu walishiriki kuwaua watu hawa kwa kuwaswaga mikononi mwa Interrahamwe. Mpaka leo Maaskofu hao wanasakwa washitakiwe.

Ama waliokimbilia Misikini Misikitini walisalimika, hakuna Sheikh leo anayetuhumiwa Burundi kwa kuwatoa watu waliokimbilia hifadhi Misikitini.

Leo Tanzania wanawake Waislamu wanaotafuta hifadhi Misikitini wanaswagwa nje na 'Masheikh' (Manyema) wakatwangwe virungu vya F.F.U na kung'atwa na mbwa wa polisi. Ama katika Misiba, huu ni msiba wa pekee.

Mama Sofia,
Ilala,
Dar es Salaam. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook