KUTOKA MAGAZETI YA ZAMANI
 
Wanachuoni siasa yenu inanuka Ukoloni - Dr. Kleruu
 
Ngurumo, Jumatano Septemba 19, 1962
 

MAANDAMANO yaliyofanywa hivi majuzi na wanafunzi arubaini wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupinga maendeleo ya siasa ya nchi ya Ghana yamepunguza sana sifa ya Tanganyika katika hadhara ya nchi za Afrika. TANU chama cha Wananchi hakiwezi kuunga mkono kitendo hicho cha maandamano kilichofanywa na wanafunzi hao.

TANU imeshangazwa sana kwa vile hawa wanafunzi hawakushauriana kwanza na serikali na TANU kabla ya kujirasharasha na siasa ya Jamhuri ya nchi ya Kiafrika iliyo rafiki yetu. Iwapo wanafunzi hao wangetafuta mawaidha ya serikali na TANU, wangeonyeshwa mwangaza na faida yeyote. Pamoja na hayo, hawa wanachuoni wanaokataa kutwa "watoto" wamekwisha kujionea wenyewe kuwa mbio za farasi huishia ukingoni. Haya ni maneno yaliyotolewa na Dr. Kleruu, Naibu wa Katibu Mwenezi, TANU.

Anaendelea "Chama cha Wananchi TANU, kimesikitika sana kwa vile "mabwana wakubwa" hao waliofanya maandamano walikataa kumpokea mjumbe wa Wizara ya Elimu aliyepelekwa kuwahutubia ukweli wa siasa ya Jamhuri ya Ghana maana ilitambulikana wazi wazi kuwa wanachuoni hao hawajaelewa undani wa maendeleo ya siasa nchini Ghana ingawa wao wanamaliza saa 24 kila siku kumeza herufu za vitabu. Vingi si hoja, maana kule kumeza maherufi mavolum makubwa kuliku sanduku hakuna faida iwapo wanafunzi hawaelewi kiini cha hadithi na kutumia utaalamu huo madhubuti kwa kusaidia wananchi na taifa.

Hawazijui

Nazidi kusisitiza kuwa hatua ya kudharau Wizara ya Elimu inasikitisha sana TANU na wananchi kwa jumla. Je hii ndiyo kusema kuwa wanafunzi wakishaingia katika chuo Kikuu (University) wanakuwa na pawa au uwezo mkuu kupita serikakli na Wizara yake ya Elimu? Wakati umewadia kwa kila wanachuoni kukumbuka kwamba Chuo Kikuu kinaendeshwa kwa gharama ya serikali kwa kufuata yale madhumuni ya kuondoa ujinga nchini. Hivyo yawapasa wanachuoni wetu wajishughulishe na mambo ya kujenga nchi zaidi kuliko randa randa za kubomoa au rasharasha za kuingilia siasa za nchi ngeni wasizoweza kutambua kichwa au mkia.

Watose serikali

Yatubidi kukumbuka kwamba tangu nchi ya Ghana ilipopata uhuru mambo yae, wakoloni wamejaribu kila njia ili kutosa serikali ya Osagyefo Dakta Nkrumah maana serikali yake ilijibidisha sana kutetea nchi za Afrika zipate uhuru wao. Awali kabisa Dk. Nkrumah alitamka kwamba uhuru hautakamilika mpaka nchi zote za Afrika zimekuwa huru. Hivyo basi mkoloni ni wa zamani (traditional colonists) na mkoloni siri (neo-colonialists) wameiteua serikali ya Dr. Nkrumah kuwa adui yao namba wani.

Makoloni hawa wamewahonga baadhi fulani ya Waghana ili wawatimizie mahitaji yao ya kutosa serikali ya Taifa ya Ghana. Chama cha Wanaghana kinachoitwa Convention Peoples Party (CPP) na serikali ya Rais Nkrumah wamejitahidi iwezekanavyo kujilinda na hatari hizi ziletwazo na hao maadui wa serikali ya Ghana. Na wajibu wa kila serikali kujilinda ili iweze kuwatimizia raia zake haki zao za maendeleo. Kwa hiyo ukitupilia mabli propaganda ya wakoloni na wafuasi wake utaona kuwa Dakta Nkrumah anastahili pongezi kubwa kwa kazi yake mahususi ya kutunza amani na usalama nchini na kudumisha uhuru wa jamhuri ya Ghana kwa kupambana na yale makoloni yanayojaribu kuirudisha Ghana katika hali kikoloni.

Wafanye nini

Hebu basi wanachuoni wetu mlimwandama Dakta Nkrumah tuambieni kama ninyi baada ya kumeza herufi kadhaa katika volumu zenu chache za sheria mnaonelea kuwa ni heri Ghana ibaki huru au irudi tena mikononi mwa wakoloni? Hakika maandamano yenu yaonyesha wazi wazi kuwa mnapendelea Ghana iwe koloni tena. Kinyume kabisa cha hiyo siasa yenu inayonuka ukoloni, TANU pamoja na serikali ya Ghana iwe huru milele.

Mwisho kabisa naomba kuwaonya wanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, juu ya kitendo kingine walichofanya hivi majuzi. Siku chache zilizopita wanachuoni hawa walipata bahati kubwa ya kuhutubiwa na Mwananchi mashuhuri. Baada ya hotuba hii iliyokuwa ya kupendekeza mno kiongozi wa hawa "mabwana wakubwa", badala ya kumshukuru huyo mtu mashuhuri alimsikitikia na kumwambia atakuta dikteta.

Hakika hii ni dharau kubwa sana, na hivyo nawashauri hawa wanafunzi walikiri kosa lao na kumwomba radhi mwananchi huyo mashuhuri bila ya kukawia. Pia kumbukeni kuwa heshima ni msingi mkubwa wa heshima na elimu za aina zote.


Aliyekuwa akimghasi kisura kwa simu kanaswa

Ripota wetu, Dar es Salaam, Jumatano.

MBELE ya Hakimu E. Onweni Abdul Mohammed Satchu alikiri kuwa yaye ndiye alikuwa akimpigia simu Bi. D. Bunji Patel na kumwongelesha maneno ya ukorofi.

Ilielezwa kortini kuwa kijana huyo Satchu alikuwa kila siku akipiga simu kwa kisura Bi. Patel na kumwomba wapange siku waende pafaapo wakafanye mapenzi.

Bi. Patel habari hiyo ilimuudhi na akamweleza baba yake kuwa kuna kijana mkorofi kila siku anapiga simu na kuongea mambo yasiyomfaa. Mzee kusikia hayo alipeleka taarifa polisi na huko sehemu ishughulikayo na upelelezi ikapashwa habari.

Kisura aliambiwa kuwa akipata simu tena toka kwa Satchu asiikate haraka bali ampe vipande na maneno matamu ili waongee kwa muda mrefu.

Wakuu wa Posta walielezwa habari hii nao wakishirikiana na polisi walimkamata huyu kijana siku ya tarehe 10.10.63, maana kama saa sita na dakika ishirini na saba Satchu alipiga simu kwa Bi. Patel.

Watu wa posta kuangalia waliona kuwa huyo aliyepiga simu alikuwa katika kituo cha kupigia simu kwa watu wote wenye namba 20502 kilichoko Splended Hotel katika mtaa wa Independence na bila kuchelewa gari yenye redio ya polisi ikamfuata, ndani yake akiwamo Bwana Singth ambaye ni ofisa wa polisi.

Baada ya dakika moja kijana alikutwa bado anaongea na kisura kigujerati. Bwana Singth aliingia na kumnyanganya kipembe cha simu na kusikiliza na alisikia sauti ya Bi. Patel akiita Chandarakunt jina la bandia la Satchu alilokuwa akijiita kwa yule kisura.

Satchu alisombwa mpaka kituo cha polisi na huko mambo yakawa makubwa yakafika mpaka kufikishwa kortini. Jumamosi itajulikana Satchu atafanywa nini.



Mkaburu amshambuli Mkaburu

Ripota wetu, Nairobi, Alhamisi.

Mwafrika, Ijumaa, Aprili 10,1964

SIKU itakuja ambayo Mwafrika atapata kura na kuitawala Afrika Kusini.

Hayo yamesemwa na bwana Nico Pereira wa Afrika Kusini ambaye zamani alikuwa mfanya kazi wa idara ya kutawaka Waafrika.

Akihutubia mkutano wa Nairobi Club mjini Nairobi, Bwana Pereira alisema kwamba uhuru wa Afrika Kusini hautakuja kwa migomo au kumsusia Mkaburu tu, lakini vuta vya nguvu ni lazima vitafuata.

'Utawala wa Kikaburu nu lazima tutafute njia ya kuuondoa'.Alidokeza kwamba ni lazima Mwafrika apewe haki ya kuamua ni aina gani ya maisha anayotaka kukaa.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook