CHAKULA NA LISHE
 
Na Mujahid Mwinyimvua
 

KATIKA makala ya chakula na lishe iliyopita tulizungumzia umuhimu wa kutafuna chakula. Tuliona kwamba, mtu lazima ale pole pole na chakula kitafunwe kwa muda wa kutosha. Kinyume na hivyo chakula hicho hakitaweza kutoa virutubisho vya kutosha mwilini. Na badala yake, sehemu kubwa ya chakula alichokula mtu kitatoka nje ya mwili kama kinyesi.

Vile vile tulisema kuwa mwili wa binadamu una viungo maalum kwa ajili ya usagaji wa vyakula tunavyokula kila kukicha. Na jambo hili kamwe haliwezi kuwa ni zao la bahatinasibu (chance creation) kama wanavyodai akina Marx. Ila huu ni mpango kabambe wa Mhandisi wa wahandisi (Master of Engineers).

Wiki hii, tunaunganisha wazo kuu la somo lililopita kwa kutazama hatari ya kicheko au kusema kwa sauti kubwa wakati wa mlo.

Kitendo cha kucheka au kusema kwa sauti kubwa wakati wa kula kimekemewa na dini. Hata hivyo, mafundisho hayo ya dini yanaonekana kama kichekesho na ni upuuzi mtupu!

Watu hawaishii hapo, bali wanatupasha kwamba Mungu 'amekufa' hasa kule Ulaya na Marekani! Wakithibitisha hoja yao hiyo, wanatoa takwimu (ambazo ni sahihi) kama ile inayosema kuwa: idadi ya wanaokwenda kanisani katika nchi za Ulaya inapungua kadiri maendeleo ya sayansi yanavyozidi kwenda mbele.

Mpaka sasa kwa mfano, wanaokwenda kanisani nchini Uingereza ni asilimia moja tu yaani 99% ya Wakristo wa Uingerza hawaendi Kanisani. Si hivyo tu bali pia, mmomonyoko wa maadili unakwenda kwa kasi kubwa. Makanisa kdhaa yameruhusu pombe, na pia yanahisa katika kampuni kubwa zinazotengeneza pombe hasa Uingereza!

Wanaume kubadilisha jinsia zao na kuwa za kike "rukhsa", 'ndoa' za jinsia moja (wanaume na wanaume na wanawake kwa wanawake) ni mambo ya kawaida. Kwa kifupi 'uchafu' uko mwingi na wa kila aina. Na sisi watu wa Afrika kigezo chetu ni Ulaya na Marekani.

Kadhia yote hiyo ni 'matunda' ya viongozi wa dini kuipotosha dini sahihi na hatimaye kushirikiana na viongozi wa serikali (wa zama hizo) na kuwanyonya wananchi. Jambo ambalo liliwafanya akina Karl Marx kuibuka na itikadi ya kutenganisha dini na siasa (secularism) ambayo nayo imeleta msiba zaidi kwa wanadamu.

Maelezo ya hapo juu yanalenga kuwazindua wananchi ili wasidharau mafundisho ya dini iliyosahihi. Mengi ya mafundisho hayo yanamaelezo ya kisayansi kama hili la makala ya wiki hii.

Kutafuna na kumeza chakula ni vitendo vinavyoshirikiana vizuri. Baada ya chakula kutafunwa kinatelemka kwenda tumboni na kwa kupitia kooni. Pale kooni kuna njia mbili. Moja ni ile ya chakula kwenda tumboni na ya pili ni ile ya kwenda kwenye mapafu.

Wakati chakula kinapita kwenda tumboni, ile njia ya kupeleka hewa kwenye mapafu hufungwa ili chakula kisiingie kwenye njia hiyo. Kama mtu anakula chakula na huku anacheka (kwa nguvu) au anasema kwa sauti kubwa, utaratibu wa hapo juu huharibika, Ndiyo kusema, ule mlango wa kupeleka hewa unaweza kufunguka na chakula kupenya.

Kama jambo hilo litatokea, mtu huyo atakohoa sana mpaka kile chakula kitoke. Kama chakula hakitatoka maana yake ni kuwa, hewa inaweza kukosa kupita. Na kama mtu hapati hewa kwa muda fulani (siyo mrefu) anaweza kufa.

Kama janga hilo likitokea kwa uzembe au bahati mbaya, mtu aliyeathirika apelekwe hospitali haraka inavyowezekana.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook