Ijue sheria
 
Wajibu wa mahakama -2
 
Na Dkt. Abdallah J. Saffari

UWEZO huo mkubwa wa wazee wa baraza umepata kujadiliwa kuona iwapo unastahili kuwa hivyo au la. Lakini hadi sasa uwezo wao huo haujapunguzwa wala kubadilishwa kwa jinsi yoyote ile (K.h.j)..

Mahakama ya Mwanzo yana mamlaka ya kusikiliza mashauri yote ya jinai yanayotokea katika wilaya ya mahakama hayo na wala sio nje ya wilaya hiyo yake (9F. 3(1), Sheria ya Mahakama ya Mahakimu, i.h.j.).

Mahakama ya Mwanzo yana uwezo wa kusikiliza karibuni mashauri yote ya jinai isipokuwa yale makubwa sana mathalan mauaji, uhaini, kuzinga na maharimu na kadhalika.

Juu ay mahakama ya Mwanzo yako Mahakama ya Wilaya. Mahakama ya Wilaya yako katika daraja moja na Mahakama ya Hakimu Mkazi. Uwezo wao katika mashauri ya jinai unalingana isipokuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi yana uwezo mkubwa zaidi wa kusikiliza mashauri fulani ya madai kama vile chini ya Sheria ya Kodi za Majumba.

Mahakama ya Wilaya, mbali na Mahakama ya Hakimu Mkazi, yana mamlaka ya kusikiliza mashauri yote ya jinai katika wilaya yake. Kwa upande mwingine Mahakama ya Hakimu Mkazi, kwa kawaida, yana mamlaka ya kusikiliza mashauri yote katika mkoa wake (10F.5 (1), Sheria ya Mahakama ya Mahakimu, i.h.j). Kutokana na hali hiyo mara nyingi mahakama hayo hufahamika kama Mahakama ya Mkoa. Lakini sio lazima kila Mahakama ya Hakimu Mkazi yawe katika mkoa. Jaji Mkuu anao uwezo wa kuyaweka mahakama hayo mahali popote pale (K.h.j). Mathalan wilaya ya Same na Korogwe zina Mahaama ya Hakimu Mkazi.

Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi yana uwezo wa kusikiliza karibu makosa yote ya jinai isipokuwa yale makubwa sana kama vile mauaji, uhaini, ujasusi na kadhalika. Kuhusiana na makosa hayo makubwa yana uwezo wa kuendesha uchunguzi wa awali tu na kupeleka kumbumbuku za uchunguzi huo Mahakama Kuu kusikilizwa rasmi.

Kikao cha mahakama haya kinakuwa kamili wakati Hakimu mmoja anasikiliza shauri linalohusika (hata kosa liwe la uzito kiasi gani) muradi liko ndani ya uwezo wake kisheria. Hata hivyo, iwapo instahili Jaji Mkuu anaweza kuamuru idadi kubwa zaidi ya Hakimu mmoja wasikilize shauri linalohusika (12F. 6(4), Sheria ya Mahakama ya Mahakimu, i.h.j).

Vikao vya aina hiyo ni maarufu kama "Mahakama Maalum". Kwa kawaida idadi yao huwa watatu. Inasadikiwa hii ni kuepukana na mgawanyiko sawa wa mahakimu hao katika uamuzi wao. Hukumu au uamuzi wa mahakama katika kikao hicho huwa niule wa walio wengi.

Sababu za kuwa na "Mahakama Maalum" haziko wazi. Ni Jaji Mkuu tu mwenye uwezo wa kuamua kuwepo kwa vikao vya namna hiyo; hivyo yeye ndiye anayeweza kuelewa sababu za kufanya shauri fulani lisikilizwe na mahakama hayo.

Kuwa na majaji zaidi ya wawili kusikiliza shauri moja sio jambo geni katika mahakama kuu lakin sio la kawaida katika mahakama ya wilaya. Wakati wa kusikiliza mashauri ya katiba Mahakama Kuu hufanya hivyo katika kikao cha majaji watatu. Inawezekana kukubalka kabisa kuwa uwezo wa akili za wengi, kwa kawaida, ni mkubwa na sahihi zaidi. Pamoja na kweli hiyo vikao vya "Mahakama Maalum" vimesababisha ucheleweshaji wa mashauri kwa vile sio rahisi kuwapata mahakamu wote kwa wakati mmoja kusikiliza shauri linalohusika. Isitoshe wana mashauri mengi ya kusikiliza mbali na shughuli za kiutawala.

Wazee wa baraza sio sehemu muhimu katika mahakama ya wilaya wakati wa kusikiliza mashauri ya jinai.

Mamlaka mengine makubwa ya mahakama ya wilaya in kusikiliza rufani na kufanya mashahihisho ya mashauri kutoka mahakama ya mwanzo (F. 22, Sheria ya Mahakma ya Mahakimu, i.h.j). Kwa amri ya Jaji Mkuu, Hakimu Mkazi anaweza akapewa uwezo wa kusikliza mashauri ambayo kwa kawaida husikilizwa na Mahakama Kuu. Uamuzi wake katika mashauri hayo unachukuliwa kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu.

Ngazi ya tatu ni Mahakama Kuu, ambayo huitwa kwa jina kamili Mahakama Kuu ya Tanzania (14Ibara 108, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977). Mahakama haya husikiliza mashauri mintaarafu ya makosa ya aina yoyote ile nchni Tanzania na uweza kutoa adhabu ya juu kbisa iliyowekwa na sheria kwenye kosa lolote ambalo mshitakiwa ametiwa hatiani (F. 166, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, Na. 1. 1985).

Ingawa maahakama hayo yana uwezo wa kusikiliza mashauri ya jinai kwa mara ya kwanza, kwa kawaida hayafanyi hivyo isipokuwa kwa makosa makubwa kama vile mauaji, uhaini, ujasudi na kadhalika, makosa ambayo mahakama ya wilaya hayana mamlaka ya kuyasikiliza. Kwa mara ya kwanza Mahakama Mkuu ya Tanzania, Tanga yalisikiliza shauri la wizi wa fedha za kigeni katika shauri la R.v. Joseph Samwel na Wenzake (Shauri Maalum la Jinai Na. 7, 1980, Mahakama Kuu ya Tanzania, Tanga (Hajachapishwa).

Hivyo basi kazi kubwa ya Mahakama Kuu ni kusikiliza rufani kutka Mahakama ya Wilaya pamoja na kufanya masahihisho ya uamuzi wa mahakama hayo ya chini (F. 359 na 373, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).

Kwa kawaida Jaji mmoja hufanya kikao kamili cha Mahakama Kuu wakati wa kusikiliza mashauri ya jinai, ila huwa watatu wakati wa kusikiliza masuala ya Katiba.

Mahakama ya Rufani ya Tanzania ndiyo ya juu kupita yote (Ibara ya 116, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, i.h.j). Kazi yake ni kusikiliza rufani tu kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania (F.3, Sheria ya Mahakama ya Rufani, Na. 15., 1979). Majaji watatu hufanya kikao kamili cha mahakama hayo, isipokuwa wakati wa kusikiliza rufani kutoka uamuzi wa majaji watatu ambapo hukaa watano (K. 25, Kanuni za Mahakama ya Rufani, 1979).
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook