Rais, tumesoma na kutafakari hotuba yako, wasiwasi wetu uko kwa watendaji wako
MHESHIMIWA Rais tumesoma na kutafakari hotuba yako uliyoitoa kwenye mkutano mkuu wa BAKWATA Dodoma hivi karibuni.
Ni jambo la kutia moyo kwamba katika kipindi cha nusu mwaka umehiari kuzungumzia masuala yanayowahusu Waislamu nchini, mara mbili. Mara ya kwanza ilikuwa katika Baraza la Eid, Dar es Salaam. Tunashukuru kwa hilo.
Bahati mbaya Mhe. Rais moyo huo wa kusimama na kuwataja Waislamu kwa njia ya kheri hatujazoea kuuona kwa viongozi wengi wa juu katika serikali yako ikiwa ni pamoja na wale walio karibu nawe.
Tunasema ni bahati mbaya kwa sababu miongoni mwa maneno mazuri uliyoyazungumza, zipo ahadi za kuwatekelezea Waislamu yale mambo yatakayowaondolea kero ya kudhulumiwa haki zao nchini kama binadamu na kama wananchi.
Maana mambo hayaendi kwa kutamkwa tu. Sharti yatekelezwe kwa vitendo. Na hao walio chini yako ndiyo watendaji na watekelezaji wenyewe.
Lakini kama nao walio chini yako watakuwa ni wenye kutoa kauli zisizo fanana na zako, na yale unayo yaahidi ikawa si yenye kutekelezwa, kwa vyovyote vile wananchi Waislamu wataondokewa na tamaa ya kutegemea waliyoahidiwa na Rais wao.
Mhe. Rais, tukipima msisitizo wako wa ahadi za kuwatendea haki Waislamu sawa na wananchi wengine kama ilivyoainishwa ndani ya Katiba ya nchi na jinsi Waislamu wanavyoendelea kupuuzwa na kudhulumiwa ni dhahiri kwamba upo uwezekano wa kuwepo watu katika serikali yako wanaodhani kuwa mambo mengi yaliyomo katika katiba hayawahusu Waislamu kama wananchi.
Hali hiyo haifai kuachiwa. Tungependa kushauri kwamba kwa hapo tulipofika ni vyema Mheshimiwa ikawepo dhamira na jitihada ya kuwabana watendaji wako kuhusu utekelezaji wa yale uliyokwisha ahidi.
Waislamu hawafurahi kuona kila kukicha uteuzi wa nafasi za uongozi una kwenda kwa Wakristo kwa zaidi ya asilimia 80 au 100 hata baada ya kuahidi kufanya uteuzi kwa uwiano kama ulivyoagiza kuhusu Bodi za Parole.
Waislamu hawapendi kuona wanaendelea kunyanyaswa, kupigwa na kuwa mahabusu kwa sababu tu ya kudai kufanya maandamano ya amani kutoa hisia zao dhidi ya Wabunge walioruhusiwa kutoa hisia zao za chuki dhidi ya imani ya Waislamu kuhusu swala ya Ijumaa na vazi la Hijabu.
Mhe. Rais, kama kuna jambo ambalo Waislamu wanashindwa kuwaelewa watendaji wako, ni hili la kuvamia Msikiti na kuwakamata waumini waliomo ndani katika kipindi ambacho bado Waislamu wanadai hatua zilichukuliwe dhidi ya wale walioamrisha na kuvamia Msikiti wa Mwembechai mwaka 1998. Kisha kuwakamata waumini waliokuwemo ndani ya Msikiti huo. Wakawapiga, wakawaweka mahabusu na kuwatesa, wagonjwa wakanyimwa haki yao ya kupata matibabu. Baadhi yao wakafia mahabusu. Wengine wakatoka taabani na kufariki.
Baya zaidi hata wale waliotoa amri na kuwauwa Waislamu kwa kuwapiga risasi bado hawajachukuliwa hatua.
Si hivyo tu, watendaji wako pia hawaoni vibaya kuwazushia Waislamu mambo mazito na kutisha mpaka kwenye Bunge. Kwa mfano, katika mauaji ya Mwembechai yaliyofanywa na polisi, ulitolewa uzushi usio kuwa na mashiko na kwa sababu hiyo ukawa ukipewa sura mpya kila kukicha, ili mradi suala lile la polisi wa serikali yako kuwauwa Waislamu kama wanyama wa porini, lipate kufifia. Uzushi ule mara ulirukia balozi za nchi za nje ambazo hadi leo hazijatajwa. Mara uelekee kwenye vyama vya vya upinzani, mara wasingizie "wakorofi wachache", mara matajiri wa ndani na kadhalika. Hali hiyo kwa kweli si dalili njema ya kuwepo kwa utawala wa haki, wa sheria na unaoendesha mambo yake kwa uwazi kama ambavyo wengi tungependa kuamini kuwa ndiyo matarajio ya msimamo wako.
Inasikitisha zaidi kuona kuwa hata pale uzushi huu ulipofikishwa Bungeni baadhi ya viongozi wengi wanaounga mkono utawala wako walishangilia kwa vifijo na nderemo zilizounga mkono kauli za "kuendelea kupambana na Waislamu".
Katika Bunge hilo, yupo kiongozi wa serikali aliyesimama na kudai kuwa mtoto Chuki Athumani aliyepigwa risasi na polisi na kumsababishia ulemavu wa kupooza mwili maishani, alipigwa risasi hizo kwa sababu alikuwa kabeba "makaratasi ya uchochezi". Lakini kiongozi huyo hadi leo bado hajawajibu swali lao Waislamu wanaotaka kujua makaratasi hayo ni yepi na yako wapi! Wala hajaweza kujibu swali linalotaka kujua je, polisi wale walimpiga risasi mtoto Chuki ndipo wakagundua kuwa alikuwa na makaratasi, au walimuona na makaratasi ndipo wakaamua kumpiga?
Kimya chao maana yake majibu ya maswali hayo hawana. Lakini hatudhani kuwa kimya chao kitawafanya Waislamu waache kuhoji maswali mengine zaidi yanayoambatana na hayo. Wala hakitowafanya Waislamu waache kuiona, kuilaani na kukumbuka dhulma waliyofanyiwa katika kadhia ya mauaji ya Mwembechai. Ndiyo maana Mhe. Rais, Waislamu bado wanaendelea kukusihi uunde tume iliyo huru na itakayoridhiwa na pande zote ili ukweli kuhusu wahusika wa mauaji ya Mwembechai wapate kujulikana na kuchukuliwa hatua zinazostahili kisheria.
Mhe. Rais, lipo jambo jingine lisilopendeza kwa vile limejaa chuki na harufu mbaya ya udini dhidi ya Waislamu. Hili lina hatari sana kwa kuwa baadhi ya watendaji wako wa chama na serikali wanadhani wanaweza kuwatendea hivyo Waislamu na mambo yakaendelea kuwa mazuri tu upande wao daima milele.
Katika tukio la kukamatwa waumini katika Msikiti wa Manyema. Waumini wamekuwa wakipigwa kiasi cha kutisha, wakisindikizwa kwa marungu hadi wanaingia ndani ya gari na kule wanapokewa na marungu ya askari walio ndani ya gari. Je, tafsiri ya marungu haya kwa mtu ambaye tangu hapo hana kosa, lakini pia hajakataa kukamatwa, ni nini! Kama si chuki za kidini za watendaji wa serikali yako ni nini!
Hivi karibuni yupo mmoja wao aliyetamka kuwa Waislamu walikuwa wakihongwa kanzu na kofia au "vibandiko" ndani ya Misikiti ili wapate kuwapigia kura wale waliowahonga.
Mhe. Rais, wewe ni msomi na ni mwanasiasa wa muda mrefu. Unajua historia ya nchi hii hususan jinsi Waislamu walivyosimama kidete kuung'oa utawala wa Mjerumani na Mwingereza. Na unafahamu kuwa wakoloni waliweka wananchi katika hali ya umaskini mkubwa. Kama Waislamu ni wenye kuhongwa katika nyanja za siasa, hebu wenzetu hawa na wajiulize, ni chama gani leo chenye uwezo wa kutoa hongo kuliko uwezo waliokuwa nao watawala wa kikoloni? Na kama Waislamu ni wenye kuhongwa wakoloni hao wangeliondolewa na nani? Hebu na wasome vitabu vya Mohamed Saidi (Abdulwahid Sykes 1998) na Susan Greier (Tanu Women 1997) waone kama wapo watu wa dini nyingine waliowazidi Waislamu katika ushujaa wa kuikomboa nchi hii. Hakika watu wa aina hii (katika chama na serikali) hawakusaidii kitu Mhe. Rais. Ni watu wepesi wa kuleta fitna na vurugu nchini hususan pale watakapogundua kuwa propaganda zao za vitisho na kejeli kwa Waislamu haziwapi tija ya KURA wala KULA.
Eneo jingine Mhe. Rais ambalo linaweza kuchafua ridhaa njema ya Waislamu ni hili la baadhi ya watendaji wako kudhani kuwa watu wote nchini wanastahili haki isipokuwa Waislamu tu.
Kwa mfano ipo haki ya kibinadamu na kikatiba ambapo mtu ana haki ya kujumuika na wenzake kuanzisha chama au jumuiya aitakayo. Wananchi wengi wana ruhusa hiyo, isipokuwa Waislamu tu! Kwanini?
Mfano ni BAKWATA na Waislamu. BAKWATA iliasisiwa kwa shinikizo la serikali mwaka 1968 baada ya kuivunja jumuiya ya East African Muslim Welfare Society iliyoundwa na Waislamu wenyewe kwa ridhaa yao. Jumuiya hiyo ilikuwa na mali, majumba, shule na Misikiti. Vyote vikaporwa na kukabidhiwa BAKWATA. Waislamu walizipinga hatua hizo na ndiyo maana hadi leo BAKWATA haina ridhaa ya Waislamu ila wachache tu wanaolindwa na katiba ya kidikteta iliyompa mamlaka makubwa Mufti wao. Lakini pamoja na uchache wao, BAKWATA hao hao bado hawaelewani. Wengi wao wapo mahakamani wakidaiwa mambo mbalimbali.
Waislamu wengi nchini wameamua kujiendeshea mambo yao kupitia jumuiya zao mbalimbali hawana haja na BAKWATA na BAKWATA wenyewe wanajua! Kwa ushahidi mzuri, BAKWATA inashindwa hata kupata pesa kwa Waislamu za kuitisha mkutano wao mkuu kiasi cha kuchangiwa na Makanisa kama ilivyokuwa mwaka 1994.
Lakini baya zaidi, watendaji wako wanadhani wanayo haki ya kuwalazimisha Waislamu kuwa chini ya BAKWATA.
Mwaka juzi yalitokea mambo ya kusikitisha sana. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni aliwahi kutoa amri zilizovuruga ibada katika Msikiti (Masjid Nuur) wa Sinza.
Mhe. Rais, ni vipi serikali yako ina uwezo kujijengea sifa ya kuongozwa chini ya misingi ya kidemokrasia ikiwa vitendo kama hivyo vinaachwa viendelee dhidi ya Waislamu? Hali hiyo Mhe. Rais inatudhulumu Waislamu. Inatugombanisha na kutugawa kati ya wale wanao "kubalika na serikali" na wale "wasiokubalika".
Hali hiyo imepelekea kuwepo kwa mtindo wa baadhi ya viongozi wa Msikiti ambao huchaguliwa na waumini, wanapokataliwa na waliowachagua hukimbilia kutangaza kuwa hawatakiwi kwa sababu eti wanaungwa mkono na serikali au chama. Na mara nyingi madai hayo huwa ni uzushi mtupu. Lakini hata hivyo hebu tujiulize Chama au serikali kinakusudia kupata faida gani kinapokuwa upande mmoja tena upande ambao haupendwi na wengi? Ni vipi serikali inadhani inapendeza kujiingiza mahali ambapo panahusu masuala ya kidini.
Mhe. Rais, inawezekana watendaji wako wakatetea vitendo vyao vya kuingilia masuala ya uongozi wa Misikiti na jumuiya za Waislamu kwa kisingizio cha kulinda amani. Lakini mbona hawaonekani kufanya hivyo kwa Wakristo waliowahi kugombana hadi kuuana huko Arumeru? Je, serikali bado ipo ikisimamia Makanisa ya viongozi walio upande wake, huko Arumeru? Ni Makanisa gani hayo. Je serikali ipo upande gani na upi katika mgogoro uliozuka kuhusu uongozi wa Kanisa la Anglikana Iringa? Serikali ipo upande gani na upi kwenye mgogoro wa uongozi wa Kanisa huko Mwanga? Mbona serikali hadi leo haijapeleka Makamu wa Rais au DC kuingilia mgogoro wa waumini na viongozi wa Kanisa Katoliki unaomgusa Padri Nkwera?
Mheshimiwa, neno "udini" na chuki za kidini haliwezi kuwa na maana halisi nchini petu kuliko hali hii ya watendaji wako kuwa na mtazamo tofauti.
Hali hiyo haifai kuachiwa. Endepo itaachiwa kuna hatari ya wananchi kujiuliza maswali yafuatayo; ni chombo kipi kinachoongoza serikali yetu; CCM au Kanisa? Ni nani watendaji wa serikali na taasisi zake, ni wananchi (Watanzania) au Wakristo?
Ni matumaini yetu kuwa
hatutafika huko.
--
|
|