Mahojiano kati ya Prof. Lipumba na Sauti ya Amerika (VOA)


MAJUMA mawili yaliyopita Profesa Ibrahim Lipumba mtaalam wa masuala ya uchumi duniani na mshauri wa chama cha Wananchi (CUF) alikwenda kikazi nchini Marekani ambako pamoja na shughuli alizoendea alipata fursa ya kuongea na Umoja wa Mataifa, Mashirika ya Fedha Duniani (IMF na World Bank), Watanzania waishio Marekani na mwisho Voice of America (VOA) ilifanya mahojiano naye. Gazeti hili limefanikiwa kupata mkanda ulionasa mahojiano hivyo kwa kwa faida ya wasomaji wetu tumeamua kuyachapisha kama ifuatavyo:

VOA: TUANZE na muafaka. Profesa Lipumba bila shaka Watanzania na hasa wanachama cha CUF walijiona wameondokewa na mzigo mkubwa kufuatia muafaka kati ya CUF na CCM baada ya mgogoro uliochukua muda mrefu sana. Kwa upande wake CUF ina majuto yoyote na imejifunza nini baada ya mgogoro ule?

Prof. Lipumba: Chama chetu cha CUF kimejifunza mengi kutokana na mgogoro ule uliotokana na uchaguzi wa mwaka 1995. Kwanza tumejifunza kwamba demokrasia ni kitu ambacho kitachukua muda kukijenga katika nchi yetu. Pili, tumejifunza kwamba jambo muhimu kuwa na uvumilivu. Tatu, wanachama wetu wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba pamoja na mgogoro wa kisiasa na pamoja na dhulma iliyotokea katika uchaguzi wa mwaka 1995, tumeweza kuimarisha amani katika visiwa vya Unguja na Pemba, tumeweza kuimarisha mshikamano na umoja wa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla pamoja na kwamba tunaamini kwamba katika uchaguzi wa mwaka 1995 chama chetu kilishinda uchaguzi wa Zanzibar.

VOA: Mwakani kunafanyika uchaguzi mkuu mpya Tanzania, nini hasa itakuwa ujumbe wa CUF katika kampeni, inataka kuipeleka wapi Tanzania?

Prof. Lipumba: Ujumbe wa CUF katika kampeni unatokana na sera zetu za haki sawa kwa wananchi wote. Chama cha CUF kinaamini kwamba Tanzania na Watanzania kwa ujumla tunahitaji kuwa na haki sawa. Kuna haki za kidemokrasia za kuchagua viongozi tunaowataka, kuchagua Rais tunayemtaka, kuchaguliwa kuwa kiongozi, mwananchi kuchaguliwa kuwa Rais. Tunaamini katika haki za kiraia kwamba mtu asitiwe jela bila ya kufuata sheria na kuwa na utawala wa kisheria kwa nchi yetu. Tunaamini katika haki za kiuchumi Watanzania wapate nafasi zilizo sawa katika kuweza kujiendeleza kiuchumi kwa uwezo wao wote. Na tunaamini katika haki za kijamii na hasa haki za kupata elimu na haki za kupata huduma za afya kwa Watanzania wote.

VOA: Tangu vyama vya upinzani viruhusiwe nchini Tanzania kumekuwa na madai miongoni mwa wananchi kuwa viongozi wa vyama vya upinzani hawaelekei kuwa na sera kamili, hamzungumzi kwa kina kuhusu masuala yanayohusu jamii, mnaonekana mahodari tu mnapolaumu Chama tawala na kwamba shauku yenu iko hasa katika kuingia Ikulu. Unasemaje kuhusu madai haya?

Prof. Lipumba: Madai hayo zaidi yametolewa na chama tawala na kwa kweli chama tawala ndicho hasa hakina sera, dira yake ya kuchaguai bado inazungumzia kwamba tutaendelea kujenga ujamaa na kujitegemea. Sisi Chama chetu cha CUF kina sera zilizo wazi, misingi ya sera zetu ni haki sawa kwa Watanzania wote. Katika upande wa uchumi, chama cha CUF kinahitaji kujenga uchumi wa soko wenye manufaa kwa wananchi wote. Katika upande wa huduma za jamii chama cha CUF kinaamini kabisa kwamba elimu ndiyo ufunguo wa maisha. Na wananchi waweze kupata elimu iliyo bora na waweze kupata huduma za jamii na hasa huduma za afya. Katika upande wa haki za kiraia, tunaamini kwamba lazima tujenge utawala unaokuwa na sheria, mahakama ziwe huru na zifanye kazi zake kwa haki. Polisi iwe ni polisi ya kitaalam sio polisi ya jazba, polisi isiwe kada wa chama chochote tawala au chama chochote cha siasa.

VOA: Ni kitu gani ambacho CUF kinaona ni muhimu sana kulingana na mtazamo wake, ambacho kama ingekuwa madarakani sasa hivi ingefanya juhudi za haraka haraka kukishughulikia?

Prof. Lipumba: Shughuli ambazo tutazipa kipaumbele kama tukiwa madarakani hivi sasa ni kuongeza ajira kwa Watanzania, kuboresha kilimo cha wakulima wadogo wadogo ambao kilimo chao wanategemea kilimo cha mashamba ambayo ni madogo madogo, tutaongeza huduma za sekta ya afya na sekta ya elimu.

Kwa sababu bila kuwa na elimu na bila kuwa na afya bora, hamuwezi mkakuza uchumi wa nchi. Na hauwezi ukafaidi matunda ya demokrasia. Kwa hiyo masuala ya elimu na masuala ya afya yatapewa kipaumbele. Tutatokana kabisa na bajeti ya hivi sasa, bajeti inayoitwa 'Cash Badget' ambayo serikali inatumia fedha inazokusanya kutokana na kodi kila mwezi, matokeo yake kipaumbele kinapewa kwa matumizi ambayo yanaidhinishwa matumizi ya Waziri, Manaibu Waziri na Makatibu Wakuu. Matumizi ya kujenga rasilimali ya Taifa yamekuwa yakididimia. Katika Bajeti ya miaka mitatu iliyopita, serikali ilipanga fedha kidogo sana kutumia kukuza rasilimali ya Taifa, kukuza vitega uchumi na hata hizo fedha zilizopangwa na serikali zilizotumika ni kiasi cha 50% yaani nusu ya fedha zilizopangwa na serikali kwa sababu wanafuata hii Bajeti iliyopangwa hivi sasa. Sisi tutaondokana kabisa na utaratibu wa bajeti wa hivi sasa.

VOA: Siku hizi Tanzania kumezuka huu mtindo wa sera za wazawa na watu wanapozungumzia sera za wazawa ni wazi wanazungumzia tofauti za rangi baina ya Watanzania wa rangi nyeusi na Watanzania wasio na rangi nyeusi, ingawa wote ni Watanzania tangu mababu na mabibi zao. Humo humo ndani mnatokota masuala ya kidini, kunatokota masuala ya kikabila. Msimamo wa CUF uko wapi katika suala hili?

Prof. Lipumba: Katika suala la uzawa msimamo wa CUF uko wazi kabisa. Sisi tunaamini haki sawa kwa Watanzania wote. Watanzania wote bila kujali kabila, dini au rangi wawe na haki katika nchi yao. Tukianza kujigawa kwamba kuna Watanzania wazawa na Watanzania wasio wazawa, kesho na keshokutwa tutaanza kujigawa kwa Watanzania Wachagga na Watanzania wasio Wachagga, kuna Watanzania Wanyamwezi na kuna Watanzania wasio Wanyamwezi. Matokeo ni kwamba tutakuwa tunaligawa taifa. Lakini la msingi ni kwamba wananchi wote wawe na haki sawa, waweze kujiendeleza kiuchumi. Matokeo ya sera za CCM yamewanyima Watanzania wengi na hasa Watanzania wazawa, hawa Watanzania wa asili ya Tanzania , nafasi ya kuweza kujiendeleza kiuchumi. Azimio la Arusha na utekelezaji wa Azimio la Arusha hata mtu alipokuwa na shamba dogo tu alionekana bepari. Aliyekuwa anafuga kuku, kuna mzee wangu aliyekuwa Waziri, marehemu Mzee Maswanya alikuwa Mbunge Tabora alikuwa na kuku Ukonga akaonekana Bepari kwa kuwa alikuwa na shamba la kuku. Kwa hiyo tuliwanyima umma wa Watanzania nafasi ya kuweza kujiendeleza kiuchumi. Na sera ambazo zinachukuliwa na CCM hivi sasa kwa kweli hazitoi nafasi kwa Watanzania wa kawaida kujiendeleza kiuchumi. Kwa mfano katika sera za vitega uchumi, vitega uchumi vinavyopewa nafuu ya kodi, vinavyofutiwa kodi, vitega uchumi visivyopungua dola za Kimarekani laki tano (500,000) ambazo kwa fedha za Tanzania hivi sasa ni kama milioni 400, shilingi milioni 400, sasa Mtanzania wa kawaida anaweza kuwa na vitega uchumi vya shilingi milioni , shilingi 50,000. Lakini sera za sasa hazitoi upendeleo wowote kwa vitega uchumi vidogo vidogo. Kwa hiyo sisi tutatoka katika hii sera ya sasa na kupendelea vitega uchumi vikubwa na kuweka sera ambayo inampa nafuu mtu wa kawaida kuweka vitega uchumi, vinampa nafuu ya kodi mtu wa kawaida anapoweka vitega uchumi.

VOA: Wewe mwenyewe Profesa Lipumba unapozungumzia wazawa, unamhesabu Peter Maganga na Mohamed Mrisho ambaye ni Mdigo au unamuhesabu pia Abdulrahaman Bafadhil ambaye ana asili ya Kiarabu lakini amezaliwa Tanzania na mababu zake wamezaliwa Tanzania. Je unamhesabu pia Alnuru Mehta ambaye amezaliwa Tanzania na babu yake amezaliwa Tanzania.

Prof. Lipumba: Mimi nawahesabu wote hao ni Watanzania, katika Watanzania ambao walikuwa watetezi wa mbele sana wa haki za kila mwananchi. Kuna Mwalimu mmoja Profesa Issa Shivji, ukimuona Issa Shivji utamuona kama ni Mhindi, lakini, katika Watanzania ambao wamekuwa mstari wa mbele kutetea haki za wafanyakazi, haki za Watanzania wa kawaida. Yeye amekuwa ni mtu wa mbele kabisa. Kwa hiyo mimi nikimuona Mhindi siwezi nikasema huyo sio mzawa halali. Watanzania ni Watanzania halali na kabisa ikiwa tutajigawa kwamba kuna Watanzania wengine Waarabu, Watanzania wengine Wahindi, basi lazima tutaendelea kusema kuna Watanzania wengine Wabondei, kuna Watanzania wengine Wanyamwezi, kuna Watanzania wengine Waha na kwa hiyo haki hizo itakuwa pia tunazigawa, Waha ama Wanyamwezi wawe na haki zaidi, kuzidi Wabondei au Warufiji au Wandengereko. Kwa sisi tunaamini kabisa kwamba tukianza kujigawa kwa rangi, kwa Uhindi, Uarabu au Uafrika tutaendelea kujigawa kwa dini, na tutaendelea kujigawa kwa makabila. Wananchi wote wa Tanzania almuradi ni Watanzana wana haki sawa.

VOA: Inajulikana chama cha CUF kina nguvu zaidi Zanzibar kuliko bara na mara nyingi mmetokea kutetea maslahi ya Zanzibar kuliko Tanzania nzima. Kwa mfano hivi sasa katika Bunge CUF inadai kwamba Zanzibar ipatiwe kiti huru cha uwakilishi katika jumuiya ya Afrika Mashariki. Madai kama hayo yanapotokea yanaiweka CUF ya bara katika nafasi gani?

Prof. Lipumba: Kwa kweli chama cha CUF ni chama cha siasa cha Tanzania. Ni kweli viti vyetu vya Bunge na viti vyetu vya Baraza la Wawakilishi vimepatikana Zanzibar, lakini si kweli kwamba CUF ni chama cha Zanzibar. CUF ni chama ambacho kimeanzishwa na vyama viwili, kimoja kilikuwa cha Zanzibar KAMAHURU na Chama cha Wananchi kilikuwa chama cha Tanzania Bara. Kwa bahati mbaya palitokea mfarakano kati ya James Mapalala aliyekuwa Mwenyekiti wetu wa Kwanza na chama cha CUF. Mtafaruku huo ulipunguza nguvu ya chama chetu bara. Lakini hivi sasa chama chetu kimekuwa na nguvu sana bara. Mathalan katika uchaguzi ambao tumeufanya hivi karibuni pamoja na kuibiwa kura chama cha CUF kimekuwa chama cha pili kufuatia Chama Cha CCM. CCM wametuzidi kura 1300 kwa jimbo la Temeke na kura 2000 katika jimbo la Ubungo. Lakini mimi naamini kabisa katika majimbo yote mawili chama chetu kilishinda.

VOA: Mgombea Urais katika uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa nani, wewe au Maalim Seif?

Prof. Lipumba: Maamuzi ya nani atakuwa mgombea wa Urais yatachukuliwa na chama chetu wakati utakapofika. Tuna utaratibu mtu anapotaka kuwa mgombea wa kiti basi lazima apate kuungwa mkono kwanza katika tawi lake la chama na watu wanaweza kujitokeza wengi. Naweza kuwa mimi na anaweza kuwa mtu mwingine yeyote akawa mgombea Urais. Jambo hilo inabidi liamuliwe na chama chetu wakati utakapofika.

VOA: Asante sana Profesa Ibrahim Lipumba.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook