Acheni kuichokoza serikali
Na Mwinjilisti Kamara Kusupa
NIMESHINDWA kujizuia kusema kutokana na tahariri yenu kama ilivyochapishwa kwenye gazeti la ANNUUR Na. 213 ya Ijumaa Agosti 6-12, 1999 kwasababu tahariri ndiyo msimamo wa gazeti, si vyema kuinyamazia. Kwanza nasita kuwaita nyinyi "Waislamu" kwa sababu vitendo vyenu ni tofauti kabisa na Waislamu niliozoea kuwaona na kuwasikia hapa nchini kwetu katika kukua kwangu, pia ninyi ni tofauti kabisa na Waislamu niliowaona kutoka nchi za Kiislamu kama Uturuki na Misri. Kwa ajili hiyo kwa kuwa si jukumu langu kuwatafutia jina, wala sipendi katika makala hii kuwaita jina lolote litakaloashiria tusi, kejeli au dharau, basi nitawaiteni "watu wa njia yenu" au "watu wa jinsi yenu" maana ninyi wenyewe ni mashahidi juu ya nafsi yenu ni kwa jinsi gani mlivyojitofautisha na Waislamu wengine wa dunia hii.
KWANZA kabisa mna ubaguzi wa ajabu kiasi kwamba tayari kuna Waislamu wenzenu ambao ninyi mmewafuta kwenye orodha ya Waislamu na pia kuwaondolea kabisa Uislamu wao kwa sababu mnazozijua ninyi wenyewe. Sijui haki ya kuwahukumu wengine ninyi mmeipata wapi maana kwa kadri nijuavyo katika mambo ya kiroho mwene haki ya kuhukumu ni Mungu peke yake, na wala si binadamu awaye yote mwenye mwili, nyama na damu, hata kama mtu huyo angekuwa mtakatifu na mwenye haki kuliko watu wote.
Pia mmeweka mbele uwongo hata pasipo hofu ya kwamba Mwenyezi Mungu anauchukia uwongo. Neno la kukumbuka ni kwamba uwongo, mtu anaweza akausema, huku akijua kwamba anasema uwongo, ama anaweza akasema huku akiwa hajui kwamba anasema uwongo. Hata hivyo kutokujua kwake hakutafanya uwongo wake ugeuke kuwa ukweli. Pia mtu anaweza akautumia uwongo, nao huu uwongo wa kutamani nao ni sawa tu na uwongo wa kusema ama uwongo wa kushuhudia. Na mwisho mtu, anaweza kuufanya uwongo. Mfano hai wa mtu kufanya uwongo, ni maandamano mliyoyatetea sana kwenye tahariri yenu. Mimi siungi mkono hatua ya serikali kuyahujumu maandamano yale kwa sababu kuandamana kama kulivyo hakuna madhara yoyote wala hakumuumizi mtu yeyote, na pia kutoa ujumbe kwa wahusika wa kile anachotaka kifanyike.
Hivyo moja kwa moja naungana na wapenda haki wengine kuilaumu serikali kwa kutumia nguvu mahala ambapo ilitakiwa kutumia hekima kidogo tu na sayansi ndogo ili kudhibiti mambo yaende kiutu na yawe na mwisho mwema. Siafikiani hata na kitendo cha kuwafikisha watu mahakamani kwani hakuna kosa lolote la jinai walilofanya. Endapo kuna sheria yoyote itakayotumika katika kuwahukumu washitakiwa, basi sheria hiyo ni "Immoral and illegal".
Hata hivyo nasema pasipo woga wala kujipendekeza kwenu kwamba mumeweka mbele uwongo na baya zaidi uwongo huo mnaurembea kwa kuupa jina zuri la kupigania haki za Waislamu. Haki za Waislamu ni kweli zipo, hakuna awezaye kukanusha kwa maana Waislamu wa nchi hii kama walivyo wananchi wengine wanazo haki zao za kikatiba, haki za kisiasa, kijamii na haki za kiuchumi.
Haki ni lazima ipiganiwe, hapo hakuna ubishi, kwani siku zote haki haiombwi bali inadaiwa ama kupigania. Ukikuta binadamu yeyote amegeuka kuwa omba omba wa haki zake, basi huyo ana kasoro katika utu wake. Lakini ninyi watu wa njia yenu hampiganii haki, badala yake mnachokipigania ni "uwongo mtupu". Yawezekana wengine hawajui kwamba ni uwongo, na pia yawezekana kati yenu wengine wanajua fika kwamba hilo wafanyalo ni uwongo lakini ili kutimiza ajenda yao ya siri wameamua kuushangilia kwa bidii zao zote. Hapa nitaonyesha uwongo ulio kwenye tahariri yenu na pia kudonoa kidogo tu uwongo ulio kwenye hoja ya Mheshimiwa Kitwana Seleman Kongo (Mbunge wa Jimbo la Kigamboni) ambaye kwa namna moja au nyingine mmeamua kumuenzi na kumvika ushujaa ambao hana wala haustahili.
Katika tahariri yenu mmerudia mara nyingi sana maneno haya "Wabunge Wakristo". Katika uhalisi wa mambo hakuna Wabunge Wakristo, kwa sababu kwanza hawakuchaguliwa wala hawakupigiwa kura na Wakristo bali wamepigiwa kuwa na Watanzania katika ujumla wao. Pili, hawakupigiwa kura kama Wakristo kwa maana ya kwamba hakuna mgombea ambaye alichaguliwa kwa sababu tu ya dini yake wala sidhani kwamba dini ya mtu ilihusishwa na sifa ya kumfanya mtu kuchaguliwa kuwa Mbunge.
Hata hivyo Mheshimiwa Kitwana Kondo, sidhani kwamba wapiga kura wa Kigamboni walimchagua kwa sababu tu ya Uislamu wake bali naamini waliona ana kitu zaidi ya dini yake ndipo wakaamua awe mwakilishi wao. Mwisho ni kwamba hakuna Mbunge anayewakilisha waumini au wafuasi wa dini yake hivyo basi hakuna Wabunge wanaowakilisha Wakristo kiasi cha kustahili kuitwa jina hilo la Wabunge Wakristo.
Sasa "uwongo" wenu unaanzia hapo. Mnapoamua kuwachora watu na kuweka "lebo" ya dini zao kwenye vipaji vya nyuso zao na kisha kuwajingea hoja kwamba wanaupinga Uislamu ili kuamsha hisia za watu wengine kwamba din ya Allah iko mashakani katika nchi hii, basi hapo ni kupanda mbegu ya fitina na kuanza uwongo. Nauita uwongo wenu kwa sababu najua Uislamu wenyewe kama ulivyo hauna uwongo. Nauita uwongo wenu kwa sababu vipimo na vigezo mnavyotumia hata kufikia hatua hiyo ya kuwaita wengine "Wabunge Wakristo" ni dhaifu sana. Kigezo chenu kikubwa ni majina tu wala si zaidi ya hapo. Ninyi mkisikia mtu anaitwa Julius, John, Daniel au Stephan basi moja kwa moja mnaweka Lebo ya Ukristo. Je, ni nani aliyewaambia haya ni majina ya Kikristo? Kulingana na ufahamu wangu haya ni majina ya Kizungu, sasa "Uzungu" na "Ukristo" ni vitu viwili tofauti kama vile ilivyo tofauti kati "Uislamu" na "Uarabu".
Na sasa tuje kwenye hoja mlizozijenga ndani ya tahariri yenu, mnasema eti Wabunge Wakristo walionyesha chuki zao dhidi ya Waislamu ndani ya Bunge. Mna uthibitisho gani kwamba wao ni Wabunge Wakristo na siyo Wabunge Wapagani? Mnasema kina Sheikh Juma Mbukuzi wasingekuwa ndani kama si wale Wabunge Wakristo kumshambulia Mbunge mwenzao Muislamu na Waziri kwa kuleta hoja ya serikali inayolinda haki na uhuru wa dini kwa wanafunzi.
Huu ni uwongo mweupe. Kwa sababu kuzomeana na kushambuliana Bungeni ni kitu cha kawaida sana kwa Mabunge ya hapa duniani hata huko Zanzibar ambako kuna Bunge la Waislamu watupu. Mbunge kumzomea Mbunge mwenzake ni tabia za binafsi haziwakilishi waumini wa dini fulani. Wakristo hawakuwatuma Wabunge wakawawakilshe huko Bungeni wala hawakuwatuma wamzomee Waziri. Sasa ninyi watu wa njia ile mnapokusudia kuandamana hadi kwa Mkuu wa Mkoa na siyo kwenda hadi bungeni kwa wahusika wenyewe mlidhamiria nini hasa? Mlitaka serikali ifanye nini? Mlitaka Yusuf Makamba afanyeje ndipo ninyi muweze kufurahi?
Kitu kingine kinachothibitisha uwongo ni waandamanaji wenyewe si wahusika halisi wa vazi la Hijab. Imekuwaje mabinti wa Kiislamu (wanafunzi ambao ndio wahusika wakuu) wasiandamane wala kushirikishwa katika kudai haki yao badala yake watu wale wale wenye kumsomea itikafu Yusufu Makamba ili adhuruke ndiyo ati waandamane kwa niaba ya wengine. Tangu lini mtu akamuandamia mwingine!!
Nasema wazi ingawa kuandamana ni haki ya msingi katika utawala wa demokrasia, kuandamana kwenu ilikuwa ni kufanya uwongo kwa sababu nia na madhumuni ya maandamano haikuwa kutafuta haki bali kuichokoza serikali ili kuona itafanya nini. Sasa kwa bahati mbaya hila yenu ikakutana na tatizo hili la serikali kuenenda katika ujinga wa Kikomunisti, mwishowe ikanaswa kwenye mtego wa lawama. Nauita ujinga wa kikomunisti kwa sababu ni wakomunisti peke yao ndio ambao walikuwa na utamaduni wa kupambana na wananchi wao kwa gharama zozote zile. Wakati mwingine wakomunisti walifikia hatua ya kuwaona raia wema ambao wanaipina serikali au wenye mawazo tofauti na mawazo ya wao walioko madarakani kama adui anayestahili kuteketezwa.
Kwa bahati mbaya serikali ya Tanzania haijaachana na mila zake potofu na utamaduni wa kikomunisti. Inastaajabisha kuona serikali imekuza na kuwasomesha na kuwahubiria wanawake waachane na mila potofu za tohara, wakati yenyewe inaendelea na mila yake potofu ya kupambana na wanachi na kupigana na watu wanaotaka kueleza hisia zao kupitia maandamano ya amani. Ingawa serikali inaendeshwa katika misingi ya haki, basi busara ilikuwa ni polisi wa FFU kuwazingira wanaandamanaji ili kwanza kuhakikisha watu wasiohusika na maandamano hawaingilii msafara wala kujiunga na waanandamanaji kufanya chochote nje ya lengo la maandamano na pia polisi au FFU kuwapa waandamanaji "route" au njia ya kupita ili kufika huko ambako maandamano yamekusudiwa kufika ama kufikisha ujumbe. Na pia kwa busara hiyo serikali ingetoa mwakilishi wake kama ni Mkuu wa Mkoa, Mbunge au Spika au yeyote yule kwa niaba ya serikali angekwenda kuonana nao uso kwa uso na waandamanaji na kuwajibika kuwajibu madai yao. Madai ya wanaandamaji yangeweza kujibika kwamba siyo jukumu la serikali kustawisha utamaduni wa Kiislamu bali ni jukumu la Waislamu wenyewe kuhakikisha utamaduni wao unaoshamiri na kudumishwa.
Si jukumu la serikali kuwaadabisha Wabunge kwa sababu haikuwachagua. Serikali haiwezi kuwachagulia Wabunge neno jema la kusema ili kuwafurahisha watu wala kuwachagulia la kuacha kusema ili kutoawaudhi watu. Mwenye jukumu la kumshikisha adabu Mbunge ni mpiga kura wa jimbo husika. Maadam hakuna mwanafunzi aliyeadhibiwa kutokana na kuvaa hija, wala hakuna aliyefukuzwa shule kwa kosa la kuvaa hijab ama kuswali siku ya Ijumaa, basi serikali haina cha kufanya na dai hili.
Inavyoelekea mabinti wa Kiislamu wa kizazi hiki hawaitaki hijab, ingekuwa wanaitaka mara baada ya kuvua sare zao za shule tungewaona wakizivaa hijab hizo katika maeneo mengine ya maisha. Lakini kinyume chake hatuwaoni na hijab masokoni wala sehemu zingine wanazokwenda kujifurahisha kama watu huru. Kumbukeni wengi wetu tunaishi na familia za Kiislamu lakini hatuoni mkiwashinikiza mabinti zenu majumbani, mitaani, michezoni, ngomani na kwenye sherehe za harusi kuvaa hijab ila cha ajabu mnataka serikali ndiyo ifanye hayo shule za msingi na sekondari. Kulikoni? Kwani ni jukumu la nani kustawisha utamaduni wa Kiislamu, serikali au Waislamu wenyewe? Ni kwanini hamuwashinikizi Wabunge wanawake wa Kiislamu kuvaa hijab Bungeni? Huu ni uthibitisho kwamba Hijab ya wanafunzi inatumiwa kama kisingizio tu, lakini nia halisi ni kuichokoza serikali.
Inaendelea toleo lijalo
|
|