Ni siku ya Ijumaa tarehe 30/7/99 baada ya sala Waisilamu walijikuta wanapigwa kwa marungu, kutupwa kwenye karandanga, na kulundikwa rumande mfano wa ng'ombe.
Miaka ya nyuma kulikuwa na Chama kinachoitwa TSPCA - Tanzania Society for Protection of Animals - yaani Chama cha kutetea ukatili wanaofanyiwa wanyama. Lengo lake ni kuondoa maonevu na ukatili wanaofanyiwa wanyama kwa kupigwa na kudhalilishwa na binaadamu. Kupitia Chama hiki ukitambulika umefanya ukatili kwa wanyama unaweza hata kushitakiwa. Naamini chombo hichi kiko mpaka leo.
Inasikitisha leo hii kusikia, na kuona kwamba Waislamu wanapigwa marungu na kulundikwa ukiachilia mbali ile ya kuuliwa katika msikiti wa Mwembechai na bado hawatakiwi kuwa na chombo cha kuwalalamikia "UDHALIMU, UKATILI NA UNYAMA WA AINA GANI HUU".
Waisilamu hawa wanatendewa hivi sio kwa jambo jingine lolote ila tu kwa sababu wanasema
(1) Wao ni Waisilamu,
(2) Wanataka wao na watoto wao iwe majumbani makazini, vyuoni au mashuleni waweze kwenda misikitini siku ya Ijumaa.
(3) Waweze kuvaa mavazi sambamba na maamrisho ya dini yao.
(4) Waweze kuishi na kuondoa kero zinazozunguka maeneo yao ya kuabudu mfano pasiwe na pombe mabucha ya nguruwe n.k. katika maeneo yanayozunguka ibada zao.
(5) Na mengineyo mengi sana.
Waisilamu hawa wametoa tamko kwenye vyombo vya habari na vyombo vya Serekali kwamba wataandamana zaidi ya wiki mbili kabla ya maandamano,
Kama ingekuwa Serekali yenye uadilifu hata kama ingekuwa ya kikafiri na viongozi wenye busara kitu ambacho kingeweza kufanyika ni angalau kuwahakikishia kwamba watashughulikiwa kero zao kama ni za msingi na vikao vya viongozi wao vikae na kutafakari na kupata ufumbuzi wa jambo hilo. Badala yake ni Slogans kama "Nchi hii ni ya amani" Slogans kama na mshikamano" n.k.
Hali kama hii inapoendelea Waislamu wanachoshwa na wanafikia mahala wanahisi sasa litakavyokuwa na liwe.
Inapofikia hali kama hii hata wale walio madarakani wanahisi moto wa viti vyao na utamu wa vyakula vyao vinapungua.
Inapofikia hali hii watu wanajiuliza kama kweli misaada ya hali na mali tulizotumia kuwaunga mkono ndugu zetu wa Afrika ya kusini na nchi zingine kama kweli sasa hivi zinaleta maana katika nchi yetu ya Tanzania.
Watu wanajiuliza kama kweli, viongozi wetu wanaweza wakasuluhisha vizuri migogoro ya nchi ya Zaire, Rwanda, Burundi n.k..
Inapofikia hali kama hii watu wanajiuliza je kweli vita kati ya Tanzania na Uganda wakati wa kumng'oa Iddi Amin kama ilikuwa ni haki au kulikuwa na Agenda ya siri.
Tunafahamu kwamba Waisilamu wa nchi hii idadi yao ni zaidi ya asilimia Hamsini (50%). Ni watu ambao katika jamii yoyote, atawale Mkiristo au Muislamu, sio watu wa kuwapuuza au kuwanyanyasa. Mtu anayefanya hivyo hana akili na hastahili kuongoza. Wasabato ni asilimia ndogo sana ya jamii ya Wakiristo nchini.Wao pamoja na watoto wao wamekuwa wakisali siku ya Jumamosi na kufanya siku hiyo kuwa ya mapumziko kwao hata kabla ya kuidhinishwa. Walifanya hivyo makazini, mashuleni n.k. Naamini mchango wao huu uliulazimisha Serekali kufanya Jumamosi kuwa siku nzima ya kupumzika. Ijapokuwa naamini vile vile kuwa kulikuwa na sababu zingine.
Ni imani yetu kuwa Waisilamu wanapoonyesha hisia zao ama kwa maneno au matendo ndio msingi wa amani. Wanahitaji kushughulikiwa. Kinyume na hapo itafikiwa mahali watakuwa wamechoka. Hali hii ikifikiwa hata kama viongozi watajaa majukwani na kuhubiri "Nchi hii ya amani" haitasaidia kitu tena.
Ewe Mwenyezi Mungu ijaalie nchi hii kuwa ni ya amani ya kweli kwa misingi ya haki na uadilifu wa vitendo bila ubaguzi au unyanyasaji wa dini.
Mwisho kwa wote wanaoitakia
heri nchi wanaona ni vizuri Serikali na vyombo vyake vikae na Waisilamu.
Wajue kero zao zote na kuwe na muafaka wa jinsi ya kuvitatua. Kinyume chake
Sererikali itaonekana imefilisika kimawazo iwapo watakuwa hawayashughulikii
matatizo haya na kusubiri wafanyiwe fujo, halafu wawafunge. Hii sio busara.
Ukiangalia utaona hawa walio magerezani ndio wenye busara kuliko sisi tulio
nje ya magereza. Sasa ikifikia hali hii, nchi hii itakuwa kweli ni Tanzania?
Serekali iwaachie Waislamu na ishughulikie matatizo yao.
--
|
|