KESI ya tuhuma ya
kukashifu dini ya Kikristo inayowakabili wahubiri wanane wa dini ya Kiislamu
imeendelea kusikilizwa katika mahakama ya Hakimu wa wilaya ya Sengerema.
Kesi hiyo namba 83/99imekuwa ikisikilizwa mbele ya Hakimu Raphael .
Watuhumiwa katika kesi hiyo ni wahubiri wa kikundi cha Al Mallid ambao wanakabiliwa na shitaka la kuhubiri Yesu si Mungu, sio mwana wa Mungu, hakufa msalabani na wala hakufufuka.
Kwa kuhubiri hivyo Hakimu Raphael aliwaambia washitakiwa hao kuwa waliudhi na kuumiza imani za Wakristo.
Awali kesi hiyo ya aina yake ilisikilizwa kwa siku mbili mfululizo kati ya Julai 6 na 7 bila ya kujali mapumziko ya sikukuu ya sabasaba.
Mashahidi wawili walitoa ushahidi wao katika tarehe hizo kabla ya Hakimu kuiomba mahakama kuendelea kusikiliza kesi hiyo hata katika siku ya sikukuu kutokana na umuhimu wake kwa jamii.
Baada ya mashahidi hao ambao ni Paroko wa Sengerema na Mzee Elikana ambaye ni Kamanda wa Sungusungu wa kitongoji cha Katunguru kutoa, ushahidi wao kesi hiyo iliahirishwa hadi Julai 13 mwaka huu ambapo mashahidi wengine wa upande wa mashitaka walitoa ushahidi wao.
Katika mashahidi hao alikuwemo Kamanda wa polisi wa Wilaya ya Sengerema hata hivyo Kamanda huyo hakuweza kufika mahakamani hapo badala yake alikwenda koplo William wa kituo cha polisi mjini Sengerema.
Katika maelezo yake Koplo William alidai kuwa ushahidi aliokwenda kuutoa ni kutambua vielelezo vilivyokutwa katika nyumba waliyokuwa wakilala watuhumiwa kuanzia Mei 5 hadi Mei 10 mwaka huu walipopewa amri ya kusitisha mahubiri yao na kutakiwa kuripoti kwa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema.
Koplo William alidai kuwa yeye alifuatana na Kamanda wa polisi wa Wilaya akiwa dereva toka mjini Sengerema hadi kitongoji cha Katunguru huku wakiandamana na Sheikh Jaha Ali ambaye alikuwa mwenyeji wa wahadhiri hao.
William alidai kuwa yeye na kamanda huyo hawakuingia chumba walichofikia washitakiwa kuchukua vielelezo walivyovihitaji bali Sheikh huyo aliwapa kwa hiari yake.
Vielelezo hivyo ni pamoja na kanda 26 na spika kubwa mbili ambazo ni mali ya wahadhiri hao.
Alipoulizwa na washitakiwa kueleza ni utaratibu gani walioufuata kuwaweka rumande na kwenda na Sheikh Jaha kuchukua vielelezo vilivyotakiwa, shahidi huyo alijibu sheria iliwaruhusu kufanya hivyo.
Shahidi wa pili upande wa mashitaka alikuwa Sheikh Jaha ambaye alipinga kuwa yeye ndiye aliyewapa polisi vifaa vya wahubiri hao.
Alisema kuwa waliingia wote chumbani na polisi hao ndio waliofanya upekuzi na kukuta kanda 26 na spika kubwa mbili ndani ya chumba walichofikia washitakiwa.
Aidha, Sheikh Jaha alidai kuwa hakufuatana na polisi hao wakati wa kurudi mjini Sengerema.
Sheikh huyo aliiambia mahakama kuwa baada ya polisi kuzisikiliza kanda hizo ilidai kuwa hazikuwa na la maana.
Alipoulizwa na Hakimu kuwa yeye akiwa kiongozi wa Waislamu aliwahi kupata kuwafudisha waumini juu ya habari ya vitabu vingine, Sheikh Jaha alijibu kuwa Waislamu wanapaswa kuamini vitabu vinne ambavyo ni Qur'an, Taurati, Zaburi na Injili.
Kuhusu madai kuwa fujo zilitokea katika mahubiri ya washitakiwa, Sheikh Jaha alionekana kushangazwa na taarifa hiyo na alisema alichokiona yeye ni utulivu na amani iliyokuwepo wakati wa mahubiri hayo.
Baada ya maelezo ya Sheikh Jaha Hakimu alimtaka mwendesha mashitaka achezeshe mkanda uliodaiwa kuwa na maneno ya kashfa, hata hivyo mwendesha mashitaka huyo alijibu kuwa hakujiandaa kwa hilo.
Shahidi wa mwisho upande wa mashitaka alikuwa mzee Rashid Juma mkazi wa Katunguru. Katika ushahidi wake alidai kuwafahamu washitakiwa kwa kuwa ni wahubiri waliofika kijijini kwao.
Alisema kuwa yeye hakuwa balozi kama ilivyodaiwa na mwendesha mashitaka bali alikutwa kwa Sheikh na maaskari waliokwenda kufanya upekuzi.
Mzee Rashid aliiambia mahakama kuwa maaskari hao walipomuona aliwasikia wakitamka "hata huyu mzee anafaa tu".
Maaskari hao walimwambia na yeye aingie ndani ya chumba kilichofanyiwa upekezi, hata hivyo Mzee Rashid alidai kuwa hakujua kilichokuwa kinatafutwa.
Mwisho wa upekuzi huo Mzee Rashid alisema aliona maaskari hao wakiongozwa na kamanda wa polisi wa wilaya wakichukua kanda 26 na kumtaka ahakikishe kama ziko idadi hiyo na kisha aweke sahihi kwenye karatasi.
Baaada ya kutia sahihi askari hao waliondoka kurudi Sengerema.
Akijibu swali la Hakimu kama aliona fujo yoyote katika mahubiri ya washitakiwa, shahidi huyo alijibu kuwa hapakuwa na fujo yoyote hata baada ya wanafunzi wa Chuo cha Biblia kuuliza maswali na kujibiwa.
Aidha, alidai kuwa hakusikia lugha yoyote ile ya kashfa zaidi ya kusema yale yanayoaminiwa na waumini waliokuwepo kwenye mhadhara huo.
Kesi inaendelea kwa upande
wa washitakiwa kutoa ushahidi wao.
Jumuiya ya Wanafunzi Waislamu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo imelaani matumizi ya nguvu yasiyo lazima yaliyofanywa na vyombo vya dola kuwazuia Waislamu wasionyeshe hisia zao.
Aidha wanafunzi hao Waislamu wamelaani tabia ya Serikali ya CCM kushughulikia masuala ya Waislamu baada ya maafa kutokea. Wakitoa mfano wa tukio la hivi karibuni la maandamano, walisema kuwa kikao kilichoitishwa na Makamu wa Rais pamoja na masheikh ambao kimsingi hawakuwakilisha hisia za Waislamu; kingeweza kufanyika kwa kuihusisha Shuura ya maimamu kabla ya tukio kama kweli Serikali ilikuwa na nia njema.
Katika tamko lao rasmi juu ya hatua zilizochukuliwa na polisi kuzuia maandamano ya Waislamu, wanafunzi hao walilaani kitendo cha Waziri Mkuu na Spika wa Bunge kutowakemea pale pale Wabunge walioonyesha hisia za udini ndani ya Bunge.
Katika kuhitimisha tamko
lao wanafunzi hao wamesema kuwa kwa vile Mh. Rais Mkapa amesema kuwa suala
la uvaaji wa Hijaab na Swala ya Ijumaa kwa wanafunzi Waislamu si suala
la kuombewa ruhusa kwa vile ni haki yao; kinachotarajiwa ni kuachiwa wale
waliokamatwa na kuwekwa ndani huku wakinyimwa dhamana.
Sheria imekiukwa - Kwikima
Mamia ya Waislamu katikati ya wiki iliyopita walijawa na furaha pale Jaji Kwikima alipowakilisha maelezo ya washtakiwa 15 wa kesi ya kufanya Muhadhara wilayani Nzega.
Hali hiyo ilitokea katika mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Tabora.
Akitoa maelezo yake Jaji Kwikima alimueleza Mh. hakimu kuwa mashtaka juu ya washtakiwa 15 yalikosewa "Sheria imekiukwa hivyo mashtaka hayo hayaeleweki" alisema.
Jumla ya washtakiwa 15 kwa pamoja wanashtakiwa kwa kosa la kufanya mkutano usiokuwa halali, kosa la pili ni kusema Yesu si Mungu wala si Mwana wa Mungu na Mungu hana mshirika na Wakristo wanakula nguruwe ni makafiri, kwa kutamka hivyo kumeathiri imani ya Kikristo"
Akifafanua ni namna gani mashtaka hayo hayaeleweki Jaji Kwikima alieleza kuwa, haiwezekani muda huo huo wamekula njama na wakati huo huo wakatenda kosa! Pia alisema jambo la pili ni kudai kwa pamoja kuwa wanatamka Yesu si Mungu wala si Mwana wa Mungu na Wakristo wanakula nguruwe ni Makafiri" kama wote walitamka hivyo kwa pamoja ina maana walikuwa wakiimba? alihoji Jaji Kwikima.
Jaji alielezea kuwa haiwezekani kwa kutamka hivyo kumeathiri imani ya Dini ya Kikristo, "Dini haiwezi kuathirika, isipokuwa mtu binafsi angepeswa kuathirika" alisema.
Baada ya kusema hayo alitaka muendesha mashtaka atoe uthibitisho huo (alieathirika ni nani) aidha Jaji huyo aliimbia mahakama sheria imekiukwa, washtakiwa baada ya kukaa siku 60 katika hiyo kesi; ikiwa maelezo ya R.C.O ya kwa nini ameahirisha kesi baada ya siku 60, hivyo alidai washtakiwa waachiwe huru. "Nawachukuwa wateja wangu (washtakiwa) hawana kesi ya kujibu, wala hawana hatia kwa kuzingatia kifungu cha sheria Namba 225" - Dk. Bilali alimnukuu Jaji Kwikima.
Hata hivyo hakimu alimuomba Jaji Kwikima ampe muda wa kwenda kusoma hivyo vipengele vya sheria alivyo vitaja Jaji ili atoe maamuzi; kesi imeahirishwa mpaka tarehe 7/8/99.
Kufuatia hali hiyo polisi kutoka Nzega iliwatia hofu sana baada ya Jaji Kwikima kuwakilisha maelezo yake, na kuwafanya mamia ya Waislamu waliohudhuria kesi hiyo kushangilia kwa furaha.
Waumini hao (washtakiwa)
walikamatwa mjini Nzega kwa tuhuma za kutoa mahubiri yaliyodaiwa kuwa ni
ya kashfa dhidi ya dini nyingine na kuwekwa rumande miezi miwili mfululizo
mapema mwaka huu.
WAISLAMU mkoani hapa wamevitaka vyombo vya habari kuacha chuki vinaporipoti masuala yanayowahusu Waislamu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi, baadhi ya Waislamu hao wamelaumu jinsi waandishi wa habari walivyokuwa wakiripoti kadhia ya Waislamu wanaoshikiliwa na polisi kwa madai ya kufanya maandamano jijini wiki iliyopita.
Mmoja wa Waislamu hao ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alitoa mfano wa baadhi ya magazeti yalivyoripoti tukio la kukamatwa kwa Waislamu hao kutoeleza ukweli kuwa watu wengi walikamatwa kwa sababu ya kuonekana ni Waislamu na sio kwa sababu ya madai ya kufanya maandamano.
Mwananchi huyo ambaye alidai alikuwepo jijini wakati wa vurugu hizo za polisi alisema watu wengi walikamatwa kwenye eneo la tukio kwa sababu tu walikuwa wamevaa kanzu na baraghashia.
Aidha, alisema alishangaaa kuona kile kitendo cha polisi kuwafuata wanawake waliokuwepo ndani ya Msikiti na kuwakamata pamoja na baadhi ya Waislamu kupigwa na polisi kutokupewa uzito wowote na magazeti hayo kuliko kile cha kuonekana Waislamu wamevunja sheria.
"Natumaini wanawake hao ndio wale waliochujwa baada ya kuonekana hawakuhusika ingawa kuachiwa kwao kulielezwa vinginevyo ili kupotosha ukweli", amesema.
Aliongeza kuwa japokuwa wanawake hao walielezwa kuwa waliachwa kwa kuonekana walishurutishwa na waume zao kushiriki kwenye maandamano hayo ukweli ni kuwa waliachiwa kama vile walikamatwa kwa kuingiliwa ndani ya nyumba ya ibada ambako akukuwa na maandamano na waandishi wa habari walishuhudia hilo.
Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Nasoro ambaye pia aliongea na mwandishi wa habari hizi alisema anashangazwa na baadhi ya magazeti kuandika tukio la Waislamu kwa kuangalia upande mmoja tu wa tukio.
Alisema magazeti hayo yamekuwa hayaangalii upande wa Waislamu una haki gani katika kadhia nzima iliyotokea na badala yake kuwaonyesha Waislamu kuwa wana hatia moja kwa moja kwa kutaka kuwagawa wananchi.
"Kuna gazeti moja (nalihifadhi) liliandika wazi kuwa watu hawa wanataka kuwagawa Watanzania bila hata kujali hisia za Waislamu kuhusiana na tukio hilo. Hivi ndivyo magazeti yanavyoripoti habari zake na kutoa hukumu humo humo au ni kwa Waislamu tu?", alihoji mwananchi huyo.
Wananchi mbalimbali wameonyesha
kukerwa na jinsi magazeti hayo yalivyokuwa yakiripoti habari hizo bila
kujali hisia na haki ya Waislamu na kueleza kuwa, kwa kiwango kikubwa yalionyesha
chuki za kidini.
SHEIKH Omar Bashir amewataka Waislamu wasifadhaishwe wala kuhuzunika kwa Sheikh Mbukuzi na Waislamu wengine kuwekwa ndani kwani Waislamu hao hawana wanachopoteza. Alisema malipo wanayopata Waislamu hao wakiwa ndani ni makubwa sana kiasi kwamba ingetakiwa kila Muislamu atamani na aone raha kuwekwa ndani.
Sheikh Omar Bashir ambaye alikuwa akiongea baada ya swala ya Ijumaa wiki iliyopita amesema kuwa isiwashughulishe Waislamu hata kama Waislamu wale walioko ndani watakufa.
Alisema hao tayari malipo yao yako kwa Allah (s.w) kwani Muislamu hapotezi kitu. Akishinda mapambano ni kheri na akiuliwa (akishindwa ), ni kheri pia.
Alisema la kuwashughulisha Waislamu ni vipi nao watafikia hatua ya kujitoa muhanga kwa ajili ya dini yao. Hata hivyo Sheikh Omar Bashir aliwahimiza Waislamu watoe michango kwa ajili ya kuwasaidia walioko ndani pamoja na familia zao.
Aidha Sheikh Bashir amewataka
Waislamu wasishangae kuwaona watu waliojitwika usheikh na uimamu wakitumiwa
dhidi ya Waislamu wenzao. Alisema watu hao wapo katika zama zote na wataendela
kuibuka na vitimbi mbali mbali. Alisema watu hao hawaoni waendako kana
kwamba hawana macho hivyo Waislamu wawaone si watu wa muhimu kwao.
WAISLAMU mjini Tanga wamelaani vikali kitendo cha polisi kuvamia msikiti wa Qubaa na kusababisha vurugu na wasiwasi kwa waumini wa msikiti huo.
Wamesema kitendo hicho kinanesha kiburi cha polisi cha kuendeleza ubabe dhidi ya Waislamu.
Mwanzoni mwa wiki hii polisi kadhaa waliuvamia msikiti wa Qubaa uliopo barabara 15 mjini hapa mara tu baada ya sala ya adhuhuri na kusababisha tafrani kubwa kwa kile walichodai kwamba walikuwa wakimtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Kutetea haki za Waislamu Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda.
Watu walioshuhudia tukio hilo waliliambia gazeti hili kuwa polisi hao wakiwa na gari lenye namba za usajili STH 1775 waliuvamia msikiti huo na kujitumbukiza na viatu ndani ya msikiti
Walisema kitendo hicho kilikuwa cha uchokozi uliowafanya Waislamu waliokuwemo ndani ya msikiti kuanza kuwakaripia polisi hao watoke nje huku wakishikilia kuwa wanataka kumkamata Sheikh Ponda ambaye waliambiwa kuwa angehutibia msikitini hapo.
Hata hivyo waumini wa msikiti huo walidai kuwa mtu waliyetaka kumkamata alikuwa mgeni aliyetokea wilaya ya Muheza ambaye alijitambulisha kuwa alikuwa miongoni mwa Waislamu waliokamatwa katika vurugu za Mwembechai ambaye alilazwa Muhimbili kwa zaidi ya miezi minne kabla ya kuachiwa huru
Walidai kuwa mgeni huyo ndiye aliyekuwa akizungumza na waumini wa msikiti huo kuomba wamchangie fedha ili kupata nauli ya kumrejesha Dar es Salaam.
Waumini hao walizidi kudai kuwa baada ya polisi hao kukabiliwa na upinzani kutoka kwa waumini hao walitishia kuwa wangemkamata kwa nguvu mgeni huyo hata hivyo waumini nao walijibu kuwa wangetumia nguvu kuwazuia.
Waliongeza kuwa baada ya mabishano makali huku umati wa watu ukiwa umejaa eneo la msikiti, polisi waliondoka mahali hapo.
Katika kile kilichoonesha
kutaka kujikosha dhidi ya kitendo hicho cha polisi, kamanda wa Polisi mkoani
hapa Bw. Alfred Tibaigana alinukuliwa na vyombo vya habari juzi akidai
kuwa polisi walikwenda kwenye msikiti huo ili kudhibiti usalama baada ya
kupata habari kuwa kulikuwa na mtu ambaye angehutubia hapo kuhusu vurugu
za Mwembechai.
--
|
|