Serikali yashutumiwa kwa kukiuka haki za binadamu
 

SERIKALI ya Tanzania imeshutumiwa kutokana na rekodi yake mbaya ya ukiukaji wa haki za binadamu ambayo inaonesha kutumika nguvu za dola zisizo za lazima dhidi ya raia, kuwaweka watu kizuizini kinyume cha sheria na ucheleweshaji wa kesi za watuhumiwa.

Makao Makuu ya Shirika la Kimataifa la haki za binadam yaliyoko Uingereza katika ripoti yake imetaja matukio kadhaa yanaoonesha ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na serikali ya Tanzania.

Ripoti hiyo imelaani mauaji yaliyofanywa na polisi Mwembechai jijini mwezi Februari mwaka jana, kuwaweka ndani na kupigwa watuhumiwa pasipo mashitaka, kuteswa wazee, watoto na wanawake na kuwaweka ndani waandamanaji.

Matukio mengine yaliyotajwa na ripoti hiyo ni pamoja na lile la kuwekwa ndani wanachama 18 wa Chama cha CUF wanaodaiwa kutaka kuangusha serikali ya Zanzibar.

Hali mbaya iliyopo magerezani pia imetajwa na shirika hilo kuwa ni miongoni mwa matendo ya kinyama yanayofanywa na serikali ya Tanzania.

Likinukuu ripoti hiyo ya AMNESTY gazeti moja la kila siku litokalo kwa lugha ya Kiingereza toleo lake la juzi limesema uchafu uliokithiri katika mahabusu na selo za magereza nchini husababisha milipuko ya magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu na kuhara damu.

"Nusu ya mwanzo ya mwaka wa jana wafungwa 47 walikufa katika gereza la Mbeya", imeeleza taarifa hiyo.

Ripoti ya AMNESTY imetolewa huku tayari kukiwa na shutuma kama hizo dhidi ya serikali ya hapa nchini.

Jopo la wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam limeishutumu serikali kwa hatua zake za mabavu dhidi ya raia wasio na hatia.

Wanataaluma hao walizifananisha hatua hizo na zile zilizochukuliwa na polisi wa Afrika Kusini enzi za makaburu dhidi ya Waafrika.

Mbali na uchambuzi wa kisomi uliotolewa na jopo la wanataaluma hao, Kamati , watu binafsi na jumuiya mbalimbali zimeendelea kuishutumu serikali kwa kutochukua hatua zozote dhidi ya ukiukwaji huo wa haki za binadamu uliofanywa na vyombo vya dola.

Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu ilitoa waraka ulioelezea chanzo cha tukio la Mwembechai na kutoa ushauri kwa serikali, hata hivyo serikali haikuwa tayari kuupokea badala yake iliamua kumsaka Katibu wa Kamati hiyo Sheikh Issa Ponda.

Waraka wa Abu Azizi uliosambazwa duniani kote pia uliishutumu serikali kwa hatua za kinyama zilizofanywa na polisi na uliishauri iunde tume kuchunguza jambo hilo.

Katika mfululizo huo wa shutuma dhidi ya serikali, zilikuwemo zile zilizotolewa na baadhi ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano ambao kwa upande wao walimtaka Spika wa Bunge aunde Tume ya Wabunge, kama inavyofanyika katika matatizo mengine, kuchunguza kadhia hiyo.

Hata hivyo katika hali ilioonesha kuwashangaza wengi, Spika hakuwa tayari kutekeleza kwa hoja kwamba Bajeti ya Bunge isingeweza kuruhusu kushughulikia jambo hilo.

Wakati Shirika la Kimataifa likiishutumu Tanzania kwa ukiukwaji wa haki za binadamu, wananchi wa Tanzania hasa Waislamu bado wanasubiri ahadi ya serikali kushughulikia kadhia ya Mwembechai ambayo imeiweka nchi katika rekodi mbaya duniani.

Jumuiya nyingi za kimataifa zimekuwa zikilifuatiliwa kwa karibu suala la Mwembechai.

Wakati huo huo Mwanasheria maarufu nchini Dk. Abdallah Saffari amelaumu utaratibu wa kurundika watuhumiwa rumande uliopo hapa nchini kwa kusema kwamba magereza hujazwa na mahabusu ambao hunyimwa dhamana kwa visingizio mbalimbali huku kesi zao zikiendelea kuahirishwa mahakamani.

Dk. Saffari amesema kesi nyingi ambazo watuhumiwa huwekwa rumande zingeweza kumalizwa bila ya kuhusishwa magereza.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook