ANNUUR yakwamishwa kuchapwa
 

UPO wasiwasi kwamba baadhi ya viongozi wasingependa kuliona gazeti hili likiendelea kuwapa habari wasomaji wake ambapo kutoka kwake leo ni nusra ya Allah baada ya kukataliwa kuchapwa katika mazingira ya kutatanisha.

Katika mlolongo huo wa kujaribu kuzima juhudi za gazeti hili kuwapasha habari wasomaji wake, asubuhi ya jana wakati yakifanyika maandalizi ya mwisho kuelekea mtamboni ghafla lilipokea barua ya mchapishaji inayodai kushindwa kuchapa kutokana na kazi maalum alizopokea.

"Tunasikitika kuwaarifu kwamba tumepewa kazi maalum ambayo inatufanya tushindwe kuchapa gazeti lenu la ANNUUR", imedai sehemu ya barua hiyo yenye Kumb Na. MNP/60/Vol.1/6 ya tarehe 12/08/1999 iliyosainiwa na Meneja Mradi.

Hata hivyo ANNUUR ilipotaka kujua kama kazi hiyo "maalum" ingeweza pia kukwamisha utokaji wa magazeti mengine yanayochapwa na mchapaji huyo ilielezwa kwamba magazeti yangechapwa isipokuwa ANNUUR.

Kwa upande mwingine taarifa ambazo gazeti hili imezipata kuhusiana na danadana hiyo zilifahamisha kwamba ili Maulid ya Msikiti mmoja jijini yanayotegemewa kufanyika leo yawepo kama ilivyopangwa, uongozi wa Msikiti huo kwa kusaidiwa na "mamlaka ya dola" umejaribu kudhibiti kile kilichodhaniwa jitihada za kuvuruga zinazofanywa na maadui.

Maulid ya Msikiti huyo yanatarajiwa kufanyika leo ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar Dk. Salmin Amour.

Taarifa ambazo ANNUUR haijaweza kuzithibitisha zinasema kwamba ili kufanikisha Maulid hayo wamiliki wa kiwanda husika walipewa shinikizo linalosemekana kutoka kwa kiongozi mmoja wa mkoa ambalo lilidai kuwa gazeti hili lingechapisha makala yenye lengo la kuvuruga sherehe za Maulid zilizoandaliwa na Msikiti huo, kwa hivyo gazeti hili lisichapishwe.

Hata hivyo, ANNUUR ilipowasiliana na wamiliki wa kiwanda hicho walikana kuandika barua hiyo.

"Kiwanda kile kina menejimenti yake na kina jitegemea, sisi tunachoangalia ni faida na hasara sio kuingilia utendaji", alidai Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya uchapishaji.

Jitihada za kuwasiliana na viongozi wengine waliohusishwa na kadhia hiyo kupata ufafanuzi haikuweza kufanikiwa.

Kutoka kwa toleo hili ni jitihada za ziada zilizofanywa na watendaji wa gazeti hili. Huenda toleo hili likawa la mwisho kutokana na harakati zinazofanywa dhidi ya gazeti hili.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook