AN-NUUR ni gazeti
lililoandikishwa kisheria kama magazeti mengine na linaloendeshwa kwa kufuata
sheria zinazohusika. Ndio maana lilipoanza lilikuwa likichapwa katika Mtambo
wa Serikali Printpak na sasa huchapwa na mtambo wa Modern Printers unaomilikiwa
na Uhuru Publications.
Tuna kila sababu ya kuamini kuwa 'Modern' wamekuwa wakifanya kazi zao kwa kufuata kanuni za kibiashara. Lakini kubwa zaidi wamekuwa makini na waungwana wasiowatizama watu kwa sura zao, vyama vyao vya siasa wala dini zao.
Kwa msimamo huo ndio maana imekuwa ni jambo la kustua kwetu kuona tunapewa taarifa ghafla ya kusimamisha uchapaji wa gazeti letu kwa madai ya kuwa na kazi maalum. La shangaza zaidi ni kuwa hiyo kazi maalum haikusitisha kuchapwa magazeti mengine. Na ndipo tukashawishika kutafuta ukweli zaidi na kupata taarifa kuwa kumbe "Kazi maalum" yenyewe ni kuwazuia AN-NUUR wasichape. Na kama wapashaji habari wetu walivyodokeza shinikizo lenyewe limetoka kwa mamlaka moja ya serikali ngazi ya mkoa ikidaiwa kwamba kutoka kwa gazeti kutavuruga Maulidi.
Kama taarifa hizi ni za kweli tunalazimika kuuliza je; Maulidi hii ina nini! Je, ni Maulidi ya kisiasa, Maulid ya kichama, maulidi ya serikali; ya Mkuu wa Mkoa au kwa ajili ya Waislamu? Kama si ya kisiasa na kichama na kama kweli kwamba baadhi ya viongozi wa siasa wameweka shinikizo kuzuia AN-NNUR isitoke kwa kuhofia itavuraga maulid hayo; Serikali au watu wa siasa wamehusika vipi na maulidi hayo? Na kwanini idhaniwe kuwa AN-NUUR itavuruga. Kosa lake nini! Je ni kumripoti Bwana Said Hilal akikiri mbele ya waandishi wa habari kuwa viongozi wa Msikiti ndio waliowaita polisi kuwaswaga wanawake waliokuwa ndani ya Msikiti!
Tunaamini kuwa serikali yetu ni ya kiungwana ndio maana haikukubali kufitinishwa na wananchi kwa tendo lile la polisi kuwakamata wanawake waliokuwa ndani ya Msikiti, na hivyo ikaamuru waachiwe mara moja.
Linaloleta utata zaidi ni kuwa shinikizo hili linakuja wiki moja tu baada ya kuchapishwa hotuba ya Mh. Rais Benjamin William Mkapa jambo linalotufanya tujiulize; je; hujuma hii inayoelekezwa kwetu ni kilelezo kuwa kuna watu imewakasirisha! Au ni kwa kuchapisha kwetu yale aliyoyasema Mh. Kitwana Kondo Bungeni! Na kama ni hivyo aliyoyasema kimsingi yanatofauti gani na yale yaliyowasilishwa kwa Mh. Rais na akayapokea pale Diamond Jubilee!
Pengine hujuma hii inayoelekezwa kwa AN-NUUR ni katika jitihada zinazodhaniwa kuwa zitasaidia kuwavuta watu wengi wahudhurie maulid hayo yanayotarajiwa kuhudhuriwa na Rais wa Zanzibar.
Lakini AN-NUUR husomwa na maelfu ya wananchi Waislamu kwa Wakristo. Kama wananchi hawa wakilikosa gazeti siku ya leo kama yalivyomatarajio yao; na kama watatambua kuwa viongozi hao walioalikwa kwenye Maulidi wamekuwa ndio sababu ya wao kukosa gazeti, kama ni kweli lilikuwepo shinikizo toka kwa viongozi wa Serikali ngazi ya Mkoa, je; walikusudia nini! Kuwachonganisha viongozi hao na wananchi! Na kwa kuwachonganisha viongozi hao na wananchi wanakusudia wao wapate manufaa gani ya kisiasa! Lakini hata kama wanalo lolote watakalonufaka, je ni lazima iwe kwa gharama ya kuwafanya wananchi wawachukie baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa Serikali yao!
Tunalazimika kuendelea kuhoji kwamba kama habari hizi za kuwepo shinikizo la kuizuia An-nuur kwa hoja ya kuinusuru Maulidi ya Msikiti fulani ni sahihi; je; Maamuzi haya ni ya kichama (CCM) na Serikali ngazi za juu, na lengo lake nini. Kama ni kuinusuru Maulidi kama habari zilivyozagaa je; CCM na Serikali; Maulidi ya Msikiti huo yanawahusu vipi; je, hiyo ni moja ya hafla za Chama, Je, hiyo ni moja ya hafla za Serikali!
Na kama CCM na Serikali yake ngazi za juu haihusiki na maamuzi hayo, haioni kuwa imejengwa fitna ya kujenga chuki baina yake na wananchi!
Lakini kama pia viongozi wa CCM na Serikali ngazi za juu hawahusiki tunapaswa kuzidi kujiuliza nguvu ya waliochukua hatua hiyo imetoka wapi. Je, ni maelekezo na maombi kutoka kwa viongozi wa Msikiti husika! Ukizingatia kuwa Msikiti si taasisi ya CCM wala Serikali je, ni nguvu gani imetumika hata viongozi hao wa kisiasa wakahiari kutoa shinikizo lililo kinyume na Sheria na Mamlaka yao! Je, ni kulipa fadhila kwa baadhi ya Masheikh waliotumika katika kadhia ya Mwembechai!
Japo serikali haina dini
lakini viongozi wake walio Waislamu wana haki ya kuhudhuria Maulidi kama
wale walio Wakristo wanavyohudhuria hafla za dini yao. Lakini hatudhani
kuwa ni kuwatendea haki viongozi hao endapo tutawaalika kwenye maulidi
zetu baada ya kuyajengea mazingira ya kuwafitinisha na wananchi.
--
|
|