Migomo na maandamano ni matokeo ya ukandamizaji


LINAPOTAJWA neno gaidi, bila shaka inatujia taswira ya mtu aliye dhamiria kutumia silaha kinyume cha sheria, akihatarisha na kudhuru maisha ya wengine na mali zao kwa lengo la kukidhi kiu cha matashi yake au kikundi cha watu bila ya kujali maslahi ya kijamii. Kwa ujum lakikomo cha harakati zote za magaidi ni mauwaji yanayoliweka taifa katika mparaganyiko wa vurugu na maisha ya wasiwasi.

Kwa maneno machache ugaidi ni dhuluma dhidi ya haki za wengine na zaidi kuliko zetu. Kwa muktadha huu, mtu au kikundi chochote cha watu wanaoanzisha, kuendesha na kuunga mkono harakati za kuwadhulumu wengine; mtu au kikundi cha watu hao ni magaidi.

Mfumo wa kibaguzi uliokuwa ukifuatwa na Serikali ya makaburu wa Afrika ya kusini ulikuwa ni utaratibu wa dhulma. Kwa maneno mengine ulikuwa ni ugaidi dhidi ya wazalendo ambao walinyimwa haki zao za kibinadamu za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa sababu ya rangi yao. 'Racial purity' ni sera ya kigaidi iliyotumika kuwagawa wanadamu katika uweusi (blacks) uchotara (coloured) na uweupe (whites).

Jeshi la makaburu lilikuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa linamkita na kumvunjavunja kila mzaledo aliyeonyesha kuchoshwa na unyama wa mfumo wa kigaidi uliokuwepo. Askari waliamini kuwa ni haki yao kumkong'ota yeyote aliyeendesha harakati za kuungo'oa udhalimu. "When I hit, I see nothing but a man and am offense" yaani Wakati ninapoamkita 'muhalifu' sioni chochote isipokuwa mtu na lile 'kosa' alilofanya". Huu ndiyo msimamo wao wakati huo.

Wote twafahamu kwamba Wazalendo wale hawakuwa na kosa lolote lile zaidi ya kudai haki, usawa, uadilifu na kuthaminiwa utu wao. Lakini jambo hili machoni pa magaidi wa kikaburu lilionekana kuwa ni uhatarishaji wa amani na usalama wa Taifa. Hivyo kila aliyepinga 'racial purity' alielekezewa nguvu za dola bila ya huruma.

Kwa kuwa si katika maumbile ya mwanadamu kukubali kukanyagwa kichwa daima dumu, ilifikia wakati wazalendo waliona kuwa ni bora mwili wake uwepo ndani ya ya ardhi kupitia mapambano kuliko kuendelea kutembea juu yake akiwa na thamani ndogo sana kuliko mbwa wa mzungu.

Migomo, maandamano, milipuko ya mabomu na mauwaji pamoja na uharibifu mkubwa wa mali uliofanywa na wazalendo katika kuonyesha hisia zao au wakati wa kukabiliana na pigapiga ya polisi wa makaburu ni matokeo ya sera ya kibaguzi (racial purify.

Kinachostaajabisha ni pale makaburu walipohalalisha ugaidi wao, wakaufambia macho na kufanya jitihada za makusudi za kuwarushia shutuma wazalendo kuwa wanatumiwa na wakomunisti na watu wamlengo wa kushoto (leftist) kuanzisha mgomo, maandamano na vitendo vya kigaidi (sabotage). Hata kama tukijaali madai hayo ni ya kweli bado mantiki inatuonyesha kuwa chanzo cha ugaidi ni waliohalalisha dhulma. Kama ni magaidi basi wao ndio nambari wani.

Wakati wa utawala wa kibaguzi gazeti moja nchini Afrika ya Kusini liliwahi kumripoti daktari wa Kiyahudi Margaret Isaacson aliyeonekana kukiuka miiko ya nchi wakati alipotumia njia ya mdomo kwa mdomo katika kumsaidi kupumu mtoto wa kizalendo (black) alipokuwa taabani. Daktari huyo akaambiwa kuwa ana matatizo ya kutotofautisha rangi (she was colour blind). Hilo ndilo kosa lake maana haikuwa haki kutumia njia hiyo kukiokoa kitoto cheusi.

Msimamo wa Makaburu ulikuwa wazi, hawakuweka katiba iliyotangaza usawa, haki na uadilifu kwa watu wote halafu watende kinyume chake. Unafiki wa namna hii hawakuutaka. Sera yao ilikuwa wazi kuwa 'blacks' hawana haki sawa na whites na 'coloured' hawana haki sawa na 'whites'. Hawakuhitaji ubalakala wa kuweka kamba inayojinadi kutoa haki kwa wote.

Hakuna marefu yasiyo na ncha. Pamoja na kufanya ukachero wa kitaifa na kimataifa, kutembeza vipigo, kamata kamata, tesatesa, fungafunga, na nynganyonga; dhulma haikufua dafu. Ikafikia hatua ambayo magaidi walilazimika kuweka chini manyanga na kuzima ngoma.

Vuguvugu linaloendelea nchini linaonyesha kuwepo kwa magaidi japo si kwa sura ile ya makaburu. Wapo magaidi waliopania kuifanya katiba yetu kuwa gofu ili haki, usawa na uadilifu vibakie kwenye maandishi. Tubakie kuinukuu tu kwa maneno kuwa tunayo katiba inayompa kila mtu uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini, kuitangaza na kufanya ibada.

Wapo magaidi waliojifunga kibwebwe waliodhamiria kuihujumu katiba kiutendaji ili kuendeleza sera ya kibaguzi iliyo mithili ya ile ya 'racial purity". Kama nilivyoeleza awali kuwa ugaidi ni mbaya kwa kuwa ni dhulma inayozaa mauwaji, uharibifu wa mali na kutoweka kwa maisha ya furaha na amani katika jamii.

Dhana kuwa nchini mwetu kuna magaidi ilishatangulia kusemwa na mhe. Rais, ambaye alitumia anuani ya wavunja madaraja. "Maana siku hizi zipo dalili za wazi za baadhi ya wenzetu kuanza kuvunja madaraja hayo kwa kupuuza yale yanayotuunganisha na kutukuza yale yanayotutofautisha udini, ukabila, ubaguzi wa rangi au jinsia, na eneo analotoka mtu.

Tanzania ni nchi inayotawaliwa, na mambo yake kuendeshwa kwa misingi iliyowekwa na katiba, sheria na kanuni mbalimbali, uhuru wa kila mwananchi wa kuamini na kuabudu kupitia dini aipendayo, nao unatokana na haki za kimsingi za raia zilizowekwa na katiba."Lakini bado katika dunia hii hakuna uhuru wa asilimia 100 uhuru ambao hauna mipaka yoyote ile. Kwa mfano pamoja na uhuru wa kuabudu, haiyumkini mtu akaingia msikitini kuswali na viatu, au akiwa hana udhu kwa sababu tu kudai haki ya kuabudu atakavyo.' "Haya ni maneno ya hekma sana.

Kanuni na sheria za nchi zinatuelekeza kuwa mtu au kikundi cha watu wakitukana na kukashifu mtu au kikundi fulani, vipo vyombo vya sheria ambayo waliotukanwa au kukashifiwa wanapaswa kuelekea huko kuyawasilisha madai ya kuumizwa hisia zao. Huko hupatikana maana ya tusi au kashifa na kupima yaliyodaiwa kuwa ni matusi au kashfa kwa mujibu wa maana iliyotolewa, na hatimaye kutolewa hukumu.

Mwaka jana Paroko Lwambano alitoa tamko la kushinikiza serikali kwa madai yasiyofikishwa kwenye vyombo vya sheria kwamba kuna wanaomtukana Yesu misikitini. Bila ya kuzingatia kanuni taratibu na sheria za nchi wahadhiri wa Kiislamu walikamatwa na kilele cha zoezi hilo kuuliwa Waislamu hadharani pale mwembe chai.

Ilitegemewa kuwa watendaji wa serikali wawe vigezo katika kuendesha mambo kwa mujibu wa sheria na katiba. Cha ajabu ni pale inapodhamiria kuwa uchapaji kazi wa dola katika kushughulikia Uislamu na Waislamu ni wa kutumia nguvu kinyume cha katiba na sheria za nchi. Kama hivi sivyo basi iwekwe wazi kuwa ni kifungu gani cha sheria au katiba kilichowaruhusu polisi kuwahukumu Waislamu kifo cha risasi pale mwembechai.

Wapo magaidi wanaolihujumu taifa letu kwa kutumia viti walivyokalia na kutumikia katiba na sheria zisizo rasmi. Magaidi wamekuwa Wakishutumiwa kwa kuwa wanatumia silaha za moto kufanya mauaji kinyume cha sheria. Ni katika msingi huo tunawahesabu walio watungua risasi Waislamu kuwa ni magaidi. Hili tunathibitishwa na ukweli kwamba mpaka sasa hajatokea kiongozi aliyewahi kuhalalisha ugaidi huo ndani ya katiba au sheria za nchi.

Katika sakata ya mwembe chai, Polisi walivunja msikiti wakaingia na mabuti yao kwa 'jeuri ya chama' na kutembeza mkong'oto kwa akina mama wa Kiislamu. Wale askari udhu walichukua saa ngapi na ni sheria ya dini gani waliyotumia kunajisi msikiti kwa mabuti. Kama ndani ya Katiba tuonyeshwe na kama ni kanuni za upolisi tuonyeshwe.

Wapo magaidi! Wanapotokea baadhi ya viongozi wa nchi kuyapongeza mauaji na unyama waliofanyiwa Waislamu, watu hao tuwaiteje ikiwa imedhihiri kuwa kile wanachokipongeza na kutendo kilichokiuka katiba na sheria zetu? Hawa ndio magaidi wanaovunja madaraja yanayotuunganisha. Na hapa ndipo yanaposadifu maneno ya mhe. Rais. "Maana siku hizi zipo dalili za wazi za baadhi ya wenzetu kuanza kuvunja madaraja hayo kwa kupuuza yale yanayotuunganisha, na kutukuza yale yanayotutofautisha - udini, ukabila, ubaguzi wa rangi au jinsia na eneo analotoka mtu."

Kweli dalili zipo wazi! Maana tukisema kuwa wale mapolisi waliwatwanga risasi waislamu kwa ruhusa ya katiba na sheria za nchi, tutakuwa tunawasingizia. Au tukisema kuwa serikali ilichukua hatua za kuwapongeza wauwaji na kukaa kimya dhidi yao bila ya kuchukua hatua za kisheria kwamba ilizingatia katiba na sheria, hapo tutakuwa hatukufanya uadilifu.

Wapo magaidi! Wanaobomoa madaraja ili kutufikisha kwenye machungu ya Rwanda, Burundi na Yugoslavia. Ni hivi majuzi tu tuliwasikia wakichemka kwa hoja ya udini kutokana na kuwasilishwa hoja ya wanafunzi kuvaa hijabu mashuleni na Ibada ya sala. Kilichozungumzwa na Prof. Kapuya hakipingani na katiba ya nchi, lakini kutokana na ilivyozoeleka alionekana kuwa anakiuka miiko kama ilivyokuwa kwa daktari Margaret Isaacson.

Hakumbukwa kuwa vyombo vya habari viliwahi kumripoti katibu mkuu wa CCM Bw. Philip Mangula akidai kuwa ulikuwepo mpango wa kuvuruga uchaguzi ambapo watu (Waislamu) pamoja na kuhongwa kofia na kanzu watafanya vurugu misikitini. Hizi ndizo siasa za udini zilizolenga kuwapaka matope Waislamu. Na hatuna yakejeli za nmna ni kuvunjika kwa madaraja.

Ningependa niyanukuu tena maneno ya mhe Rais katika hotuba yake, kuwa wapo wanasiasa magaidi wanaokusudia kutuvunjia madara. Leo wapo wanasiasa au viongozi wa wengine wa jamii wanaozungumzia wazi wazi lugha ya udini, ukabila na majimbo. Tusiwapuuze na wala tusiwaonee haya, tufungue macho yetu tuone yanayotokea nchi jirani na nyingine."

Ushabiki wa kuyashangilia yale yanayopandikiza mbegu ya chuki kama walivyofanya wabunge Wakristo walioonyesha chuki dhidi ya Uislamu matunda yake daima hayawi matamu kwa mtu binafsi na kwa taifa letu. Vile vile ushabiki kama ule uliofanywa na baadhi ya viongozi Serikali waliowapongeza wauwaji wa Waislamu pale mwembe chai, ni ushabiki mbaya sana.

Kuwa na katiba safi na sheria hakuwezi kutuzuilia kutukinga na yaliyotokea Burundi, Rwanda, Somalia na Yugoslavia. Hii ni sawa na mtu anayeumwa Malaria anayemiliki dozi ya ugonjwa huo lakini haimsaidii kwa kutembea nazo. Manufaa ya katiba yanapatikana pale isipofanywa kuwa gofu.

"Kama hatutaki, basi sisi wenyewe tusishabikie wapandaji mbegu hizo na wala sisi wenyewe tusikubali kulaghaiwa tukajikuta tumeshiriki kupanda mbegu hizo! Tuwatenge na kuwazomea wapandaji wa mbegu hizo." Haya tuwaepukeni magaidi.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook