BARUA



Bwana Julius Nyaisanga unaitukana taaluma yako

Ndugu Mhariri,

Ama kwa hakika baadhi ya watangazaji wa ITV wanachafua kwa habari zao za uzushi Bw. J.Nyaisanga katika taarifa ya haari ya saa mbili Alhamisi wiki iliyopita usiku alisema kuwa walioandamana Ijumaa iliyopita ni watu wanaojiita "Waislam wenye siasa kali".

Ni nani katika waandamanaji wale aliwahi kutamka kuwa wao ni Waislamu wenye siasa kali au Imani kali. Chuo gani hicho cha Uandishi wa habari kilichowafunza kuwa uwazulie watu; au ndio sera uliyopewa na Bosi wenu?

Mariamu Juma,
Kariakoo,
Dar es Salaam



Wabunge, huu sio udini?

Ndugu Mhariri,

Ninaomba nafasi nieleze yanayonikera. Neno "Udini" limeibuka siku za karibuni kila unapotajwa Uislamu hapa nchini , au hata zile hisia kuwa hili linalozungumzwa linalenga kutafuta haki ya Waislamu. Hijab ni Udini; haki ya kufanya ibada siku nyingine yoyote ambayo sio Jumamosi au Jumapili ni udini; usawa kazini/masomoni n.k. ni udini au unyeti!

La kushangaza na kuhudhunisha zaidi, ni kwamba viongozi Waislamu katika Taasisi za dini au Serikalini ndio wa kwanza BILA AIBU na BILA KUONA KUWA WANAKUFURU, kupiga debe na kuunga mkono maovu wanayofanyiwa Waislamu na Serikali ya nchi hii.

Mambo ambayo Serekali haisemi ni udini au ni unyeti ni haya:

(i) Vatican City kuwa na Ubalozi nchini. Roman Catholic ni maneno mawili tofauti. "Roman" ni kitu kinachohusiana na Roma (connected to Rome) na "Catholic" ni kitu kilichotapakaa ulimwenguni (universal). Hivyo, kwa kifupi ni "Himaya ya Kiroma iliyotapakaa ulimwenguni". Hiyo ni dini, na ndiyo maana kofia ya Papa imeandikwa maneno "VICARIUS FILII DEI" yaani: Vicarious = Makamu; Filii = Mwana; Dei = Mungu. Kwa ufupi Papa ni Makamu wa Mwana wa Mungu (Makamu wa Yesu), hivyo haki ya ubalozi nchini ipo.

(ii) Wimbo wa Taifa yaani "Mungu ibariki Afrika....." na dua inayosomwa na Spika wa Bunge la Jamhuri yaani "Ee Mungu Mwenyezi wa milele.....", vyote vipo ndani ya kitabu cha Katoliki kiitwacho "CHUO KIDOGO CHA SALA NA NYIMBO" ukurasa wa 12 na 86.

(iii) Kufanya siku za Jumamosi na Jumapili kuwa siku za mapumziko ili kuwaandalia Wakatoliki na Wa-protestant wafanye ibada zao bila bugdha.

(iv) Picha ya mwanamke ya Leseni ya kuendesha gari hairuhusiwi kichwa chenye ushungi, ila mwenye ushungi awe ni "Sister" wa Kikristo au awe Kalasinga bali si vinginevyo.

(v) Kuruhusu "kiti moto" (Nyama ya nguruwe) kuuzwa na kuchomwa/kuliwa na kufaga hao nguruwe hadharani bila kujali sheria za nchi.

Selemani Shaabani
Dar es Salaam.



Wataendelea kuvamia Misikiti na viatu mpaka lini?

Ndugu Mhariri

WAISLAMU lazima tuchukue uamuzi wa haraka kukomesha tabia ya polisi kuingia Misikitini na maviatu yao ambayo yanatia najisi sehemu zetu za ibada.

Waliingia Msikiti wa Uwanja wa Ndege Morogoro, Msikiti wa Buzunga Mwanza, Mwembechai Dar es Salaam, Masjid Nuur Sinza Dar es Salam, Msikiti wa Mtoro Dar es Salaam, wameingia Msikiti wa Manyema Dar es Salaam na Masjid Quba Tanga.

Lazima tuchukue hatua za kukomesha ukafiri huu usirudiwe tena,

Mbwana Jumaa,
Tanga.



Barua ya wazi kwa walioita polisi Msikitini

Ndugu Mhariri

NASHINDWA kutoa salamu kwa vitendo vya aibu walivyovifanya kwenye Msikiti wetu wa Manyema.

Hivi Bwana huyu anatutafuta nini Wamanyema? Tumekuwa na viongozi wetu wengi mababu waliotangulia hawakuwahi kuingiza polisi na viatu vyao ndani ya Msikiti wetu.

Mmetumwa na nani? InshaAllah Mungu atawaonesha.

Mwamvita Mrisho,
Dar es Salaam.



CCM itueleze wapinzani wao ni nani, CUF au Waislamu?

Ndugu Mhariri,

Napenda kuchukua fursa hii kwa kutoa dukuduku langu katika gazeti letu tukufu la An-nuur.

Mimi nimekuwa nikikerwa ,mno na hawa watu wanaojiita wana-CCM kwani mara zote wanapokuwa katika mikutano ya hadhara hawaishi kusema Waislamu badala ya kusema vyama pinzania ni jambo la kushangaza sana. Kwa mfano wakati wa kampeni za ubunge Ubungo kada mmoja alitembelea mkutano mmojawapo badala ya kutoa sera za chama akawa anamkashifu Amiri wetu mkuu Dar es Salaam. Kwa kusema eti nasikia wana kaamiri kao, mngeniita mimi komandoo niwaonyeshe! sasa yote hayo yamekujaje? Kwanza kama ni udini wanao wao, Mwenyekiti Mkiristo, katibu, Spika wa bunge, Waziri Mkuu, sijui Baba wa Taifa, ilimradi kila sehemu wanayo wao sasa vipi waseme eti CUF ina udini?

Mama Zawadi,
Dar es Salaam.



Viongozi Manyema someni Qur'an

Ndugu Mhariri

JULAI 29, 1999 Waislamu waliokuwa katika Jihadi ya kupinga njama za Wabunge Wakristo walishambuliwa na vikosi vya polisi na walijihami kwa kuingia Msikiti wa Manyema.

Katika hali ya unyama viongozi wa Msikiti huo wakawaita polisi na kuwatoa wanawake wa Kiislamu kwa polisi.

Viongozi hawa walifanya hivi kwa kujidai wao ni viongozi wa Msikiti kwa vile hutoa baadhi ya huduma kwa Waislamu hapo Msikitini.

Kutokana na uoni finyu juu ya dhana ya uongozi wa Msikiti mimi nimeamua kuwasadia aya ya Qur'an ili wajione kama wao kweli ni viongozi wa Msikiti:

"Wanaoamirisha Misikiti ya Mwenyezi Mungu ni wale wanaomuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na kusimamisha sala na kutoa zaka na hawamuogopi yoyote ila Mwenyezi Mungu; basi hao ndio wanaotarajiwa kuwa miongoni mwa walioongoka.

Je, mnafanya kuwanywesha maji mahaji na kuuamirisha Msikiti Mtukufu ni sawa na (kazi ya) wale walioamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na wakaipigania dini ya Mwenyezi Mungu? Hawawi sawa mbele ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu". (9:18-19)

Suleiman Wahabi,
Zanzibar.



Masheikh vibaraka, fahamuni Amir wetu hahitaji ridhaa yenu

Ndugu Mhariri,

Napenda kuchukua nafasi hii katika gazeti hili takatifu ili niweze kuwatanabahisha wale wote vibaraka hasa wale wanaotoa maneno machafu yenye kuwafanya Waislamu wawe na mori zaidi ya mapambano dhidi ya wenye kuwadhulumu Waislamu na wote wenye kujifanya Waislamu kumbe ni vibaraka tu.

Kumkana Amiri wa Dar es Salaam Sheikh Juma Mbukuzi ni kujisumbua bure kwa sababu Sheikh Juma sio kwamba kajichagua mwenyewe. Sheikh Juma Mbukuzi amechaguliwa na sisi Waislamu wote tunamkubali na tutashirikiana pamoja nae mahali popote wakati wowote na moja ya dalili yenye kuonyesha kwamba tunamkubali ni maandamano ya hivi karibuni kwa sababu maimamu wote wa Dar es Salaam ndio walioyaandaa chini ya Amiri Mkuu Sheikh Mbukuzi na sisi Waislamu tukaitikia wito wa Amiri wetu licha ya Serikali ya CCM kututishia lakini sisi hatukutishika.

Ama kusema Sheikh Hemed bin Juma ndio Amiri ni uzushi mtupu kwa sababu Waislamu tunatambua ni Sheikh wa Bakwata tangu ilipovunjwa jumuiya ya Waislamu Afrika mashariki na kati (EAMWS).

Khamisi K. Khamisi,
Dar es Salaam.



Akinamama mtahadhari

Ndugu Mhariri,

Napenda kuchukua fursa hii kwenye gazeti lako hili tukufu la AN-NUUR, kuwatahadharisha akinamama na hicho kinachodaiwa mikopo ili kuwaondoa akinamama kwenye umaskini! Je hiyo mikopo ilikuwa ikisubiri kukaribia uchaguzi mkuu tu wa mwaka 2000 ndio itufikie ni jambo la kushangaza mno.

Hivyo nachukua fursa hii kuwatahadharisha akinamama wenzangu wawe macho na "hongo' kama hizo.

Mama Haji,
Dar es Salaam.
--
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook