Mashairi


Buriani Issa na Salala

1. Bisimilahir Rabani, Wahariri nipokeeni,
Rambi rambi za Gongoni, pia Tabora mjini,
Machozi mengi machoni, Ulamaa kwaherini,
Buriani Sheikh wetu, Issa pia Salala.

2.Sheikh Issa katutoka, Salala amemfata,
Huzuni imetufika, msiba ulotupata,
Machozi yalitutoka, habari tulipopata,
Buriani Sheikh wetu, Issa pia Salala.

3. Ni Ijumaa hakika, Sheikh Issa katutoka,
Hakika umeitika, wito wake Rabuka,
Machozi yatiririka, maSheikh wametutoka,
Buriani Sheikh wetu, Issa pia Salala.

4. Khatibu wa Ijumaa, kabla hujaondoka,
Ulisalisha jamaa, usia ulikutoka,
Hapo ndipo ulikoma, hadi ulipoondoka.
Buriani Sheikh wetu, Issa pia Salala.

5. Mwembechai ni sababu, kanda uliangalia,
Na kifo kikakusibu, dunia ukakimbia,
Ukatutoka muhibu, ukaenda kwa Jaalia,
Buriani Sheikh wetu, Issa pia Salala.

6. Muda mfupi hakika, Salala alipotutoka,
Salala alitutoka, mwezi wa nne hakika,
Mji ulisisimka, machozi yalitutoka,
Buriani Masheikh, kiama tutaonana.

7. Hao ni Maswahiba, wa chanda na kidole,
Tofauti kwao haba, wakarimu na wapole,
Leo tena roho zakaba, Gongoni nawapa pole,
Buriani Masheikh, kiama tutaonana.

8. Salala kenda na presha, pia Issa Imemsibu,
Hakika imetutisha, Tabora nzima karibu,
Hakuna aliyebisha, Mola ametujaribu,
Buriani Masheikh, kiama tutaonana.

9. Kalamu naweka chini, majonzi tele moyoni,
Alley nawausieni, mlobaki subirini,
Kaburi zao ni jirani, wote sisi tu njiani,
Buriani Masheikh, Issa pia Salala.

Alley Mselem,
S.L.P. 935, Tabora.
--
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook