TAHARIRI


Iliahidiwa damu itamwagika

Kweli imeshamwagika


Mwaka 1993 Maaskofu wa Kikatoliki walitoa Tamko lililodai kuwa damu ipo mbioni kumwagika na kwamba baada ya kimya kirefu tamko hilo lilikuwa la kuanza kazi.

Kazi gani wangeanza kufanya hawakutaja. Uhusiano wa kuanza kwao kazi na tishio hilo la kumwagika damu pia haukufafanuliwa. Na serikali haikuona sababu ya kuwakamata na kuwahoji juu ya tamko hilo.

Hata hivyo, kubwa katika tamko hilo ilikuwa serikali kushutumiwa kuwa imeshindwa kudhibili mihadhara ya Waislamu waliyodai kuwa inakashifu Ukristo.

Tokea wakati huo serikali haikuishia tu kutoa matamko makali ya kuwashutumu wahadhiri wa Kiislamu bali pia kutuma polisi na kuwakamata Waislamu wanaosema Yesu si Mungu.

Mara kadhaa Waislamu wamevamiwa katika Misikiti yao, kupigwa, kuwekwa ndani na hata kuharibiwa vifaa (vipaza sauti).

Pamoja na kuwa viongozi wa Makanisa ndio waliokuwa wakidai kuwa wanakashifiwa lakini haikutokea hata siku moja wao kusimama mahakamani. Bali serikali ndiyo muda wote imekuwa mlalamikaji na mwendesha mashitaka.

Hata hivyo, viongozi wa Makanisa hawakuridhika na hatua hizo hivyo wakaendelea kuichagiza serikali.

Onyo lingine likatolewa Februari mwaka jana na serikali kuambiwa iache ubabaishaji.

Serikali iliomba radhi kwa kutokufanya yale ambayo Maaskofu na Mapadri waliyatarajia na ikaahidi kuchukua hatua madhubuti.

Haikupita muda shaba zikalia Mwembechai "Piga shaba; piga yule na yule". Damu ya Waislamu ikamwagika. Toka Waislamu wale wameuliwa tunadai sheria ifuatwe walioua wafikishwe mahakamani; serikali imepiga kimya huku baadhi ya viongozi wa Makanisa wakidai kuwa hata jiwe ni silaha. Wakitoa mfano wa Daudi na Goliath!

Lakini ukiendelea kuhoji zaidi; "Kwanini damu ile ya Waislamu iishie kufukiwa kwa mchanga" hutapata jibu ila utajikuta uko rumande.

Pengine tungesaidiwa kuitafsiri hali hii inawakilisha nini katika jamii yetu. Utawala wa kisheria, utawala wa haki, uadilifu, ubaguzi, uonevu, usawa mbele ya sheria au nini!

Katika vita vya Maumau inadaiwa kuwa Mzungu mmoja alisema: "Watu hawa weusi ni wakatili kama wanyama. Hebu fikiria mmoja wao alinipiga wakati nikimuua".

Je! Kukamatwa Waislamu na kuwekwa ndani ni kutokana na kuguna kwao au kuhoji kwanini wameuliwa na waliowaua hawafikishwi mahakamani?
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook