HABARI zilizotawala vyombo vya habari wiki hii ni zile za kukamatwa na kufunguliwa mashitaka ya uchochezi kwa Amiri wa Shura ya Maimamu wa Dar es Salaam Sheikh Juma Mbukuzi. Sababu hasa ya kukamatwa Sheikh Mbukuzi kama inavyodaiwa na vyombo vya habari ni kwamba alizungumza maneno ya kichochezi katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Septemba 15, mwaka huu Msikiti wa Mkwajuni, Dar es Salaam. Mwandishi Said Rajab anaelezea zaidi.
SHURA ya Maimamu ndiyo iliyowaalika waandishi wa habari kwa lengo la kufikisha ujumbe wake kwa ummah. Shura ya Maimamu imefuata taratibu zote zinazokubalika kisheria na kiitifaki katika kuzungumza na ummah kupitia vyombo ya habari. Lakini kilichotokea vyombo vyote vya habari vimeshindwa kabisa kuripoti kile alichosema Amir wa Shura. Badala yake kwa kutumia chuki zao za kidini wakamgeuza Mbukuzi mwenyewe kuwa habari kwa kumpa 'negative publicity'. Vyombo vya habari vyenye dhima ya kuelimisha ummah vimepotosha kwa makusudi lengo la mkutano wa Sheikh Mbukuzi na waandishi wa habari.
Katika hotuba nzima ya Amir Mbukuzi wao wameona neno "kumwaga damu" tu. Wahenga walisema: "Kweli ili kweli, lazima iwe kweli na yote". Vyombo vya habari havikumtendea haki Sheikh Mbukuzi kwa kuripoti hotuba yake nusu nusu na kinyume na maudhui ya hotuba yenyewe. Walikuwa na nia ya kumgombanisha Sheikh Mbukuzi na umma wa Watanzania. Huu ni uchochezi uliopea!
Kuna baadhi ya magazeti makubwa tu na yenye heshima yaliyokuwa na kazi ya kumuandama Sheikh Mbukuzi muda mrefu kabla hata ya mkutano wake na waandishi wa habari. Nia na madhumuni ikiwa kuandaa mazingira mazuri ya Sheikh Mbukuzi kukamatwa au kuhujumiwa bila ya wananchi kustushwa. Lengo hili lilitimia na wakaruka na vichwa vya habari vikubwa kama Ukweli, hekima na busara iliyokuwa ndani ya hotuba ya Sheikh Mbukuzi wao hawakuizingatia. Nia yao ilikuwa Mbukuzi na wala sio usahihi wa aliyoyasema Mbukuzi. Hawa siyo wachochezi! Au uchochezi ni kuzungumzia haki za Waislamu tu?
Mara tu baada ya magazeti kutimiza kazi yake wakadakia BAKWATA kama kawaida yao. Lakini wanajifanya ni wasemaji wa Waislamu wa nchi nzima. Ni Baraza la ajabu linalodaiwa ni la Waislamu lakini halilindi, halidumishi wala halihifadhi maslahi ya Waislamu. Uhodari wao uko katika kuhujumu na kupingana na Waislamu wenzao.
Bakwata ilitoa kauli ya kumshutumu Sheikh Mbukuzi na kuitaka serikali imchukulie hatua kali. Bakwata siyo usalama wa taifa wala Wizara ya Mambo ya Ndani lakini inaishauri serikali iwachukulie Waislamu hatua kali kwa kifua cha Bakwata. Huu siyo uchochezi? Tangu lini chombo cha Waislamu kikawaangamiza Waislamu wenzao?
Hatimaye serikali kupitia jeshi lake la polisi ilimkamata Sheikh Juma Mbukuzi Ijumaa ya Septemba 19, mwaka huu. Uchochezi wa magazeti na Bakwata umesababisha Mbukuzi atiwe ndani na kufunguliwa mashitaka.
Hivi kusema kweli ni uchochezi! Kuwaamsha watu wapiganie haki za msingi kikatiba ni uchochezi! Kutangaza dhulma unazofanyiwa ni uchochezi! Kama hivyo ndivyo basi ukweli na uwazi una maana gani?
Waislamu lazima wajifunze kutofautisha kati ya Bakwata na Shura ya Maimamu. Bakwata haikuundwa na Waislamu wenyewe kwa hiyo haliwakilishi Waislamu wa nchi hii. Kauli yao yoyote dhidi ya Waislamu itakuwa ni uchochezi na kuwaponza Waislamu.
Vyombo vya habari vinaonyesha uadui wa wazi kabisa dhidi ya Waislamu. Waislamu lazima wawe makini sana wanapofanya mahojiano na waandishi wa habari. Wajuwe wanazungumza na maadui zao na kamwe wasitegemee salama kutoka kwao. Lakini hali kama hii siyo nzuri na lazima ikomeshwe. Tusingependa kabisa nchi yetu itumbukie katika zogo kati ya waandishi wa habari na wananchi kwa sababu matokeo yake si mazuri kwa wanahabari.
Waandishi na vituo vya habari
kila siku vinavamiwa na wananchi wenye hasira katika nchi nyingine kwa
sababu ya kuandika habari za kichochezi. Hata majirani zetu Kenya wanajuwa
ugumu wa janga hili. Ofisi za gazeti moja maarufu zilishawahi kuchomwa
moto kwa sababu hiyo.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |