HOTUBA hii ya Ijumaa ilitolewa katika Msikiti wa Mwinyikheri Akida uliopo mtaa wa Bibi Titi Muhammed jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa Septemba 10, 1999 na Imam Sheikh Ahmad Haydar.
"ENYI watu hakika Mola wenu ni mmoja na wote mmetokana na Adam na Adam ameumbwa na udongo. Hakuna Mwarabu bora kuliko Muajemi na Muajemi bora kuliko Mwarabu isipokuwa kwa kumcha Mwenyezi Mungu".
Hii ni sehemu ya hutuba ya Bana Mtume Muhammad (s.a.w.) aliyoitoa katika Hija ya kuaga na inayoitwa hutuba ya kuaga iliyowavutia na kuwapendeza Waislamu wengi kwa kuhusika kwake na mambo mbalimbali yanayohusu dini ya Islamu. Waislamu waliokuwa wakimsikiliza inakadiriwa kuwa watakuwa elfu kumi. Na imeitwa hutuba ya kuaga kwa sababu aliianzia kwa kusema hivi: "Enyi watu nisikilizeni niyasemayo kwa sababu huenda tusionane tena mimi na nyinyi katika mahala hapa na katika mji huu. Na aliyowaambia ndivyo ilivyotokea aliaga dunia.
Na Bwana Mtume alitumia neno Enyi watu na hali kuwa aliyokuwa akiwahutubia wote walikuwa Waislamu, hakutumia neno Enyi Waislamu, kwa sababu hayo anayowaambia kama ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa watu wote duniani na Nabii wa mwisho yanawahusu watu wote wanaomsadikia na wasiomsadiki.
Hutuba yake hiyo inatuambia kuwa watu wote Mola wao ni mmoja naye ni Allah (s.w.) na watu wote wanatokana na asili moja ni ya baba yetu Adam (a.s.) na yeye ameumbwa na kutokana na udongo kwa hivyo watu wote wanaume na wanawake tumeumbwa na udongo. Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'an takatifu: "Enyi watu mcheni Mola wenu ambaye amekuumbeni katika nafsi (asili) moja. Na akamuumba mkewe katika nafsi ile ile na akaeneza wanaume wengi na wanawake kutoka katika wawili hao (Qur'an 1:4). Kwa hivyo basi ni marufuku na haramu katika Uislamu kubaguana kwa rangi au kabila. Mwenyezi Mungu alipotuumba kwa rangi nyeusi au nyeupe hakusudii kuna ubora wa rangi bali ni dalili na alama za uwezo wake na ihsani zake. Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'an takatifu: "Na katika alama zake (za kuonesha uwezo wake) ni kuumba mbingu na ardhi na kutofautiana lugha zetu na rangi zenu, kwa yakini katika hayo zimo alama kwa wenye ujuzi". (Qur'an 30, 22).
Ubaguzi wa rangi umeanzishwa na watu wasiomugopa Mwenyezi Mungu na wasiowaheshimu binadamu wenziwao. Ubaguzi duniani umeanza karne hazipungui ishirini na tano zilizopita.
Wagiriki walikuwa wanaamini kuwa wao ni viumbe vya Mwenyezi Mungu teule na wasiokuwa wao walikuwa wanawaita Barbara. Mmoja miongoni mwa mwanachuoni wao aliyeishi kabla ya Mtume Isa (a.s.) kwa miaka mia tano jina lake Arosto aliandika katika kitabu chake alichokiita Siyasa - haya yafuatayo: "Hakika miungu imeumba mafungu mawili ya watu. Fungu la kwanza limepewa akili kubwa na matakwa nao ni Wagiriki. Na wameumba kwa sifa hizo ili wawe Makhalifa wa Mungu ardihni na mabwana wa wasiokuwa wao. Na fungu la pili wameumbwa na kupewa nguvu za mwili nao ni Barbara. Na wameumbwa kwa sifa hii pungufu ili wawe watumwa wa fungu la kwanza lililo teule".
Waromania pia waliamini kuwa sawa na Wagiriki. Wao ndio wenye haki ya kuhukumu dunia. Na wasiokuwa wao ni Barbara na watumishi, walihalalisha utumwa kwa mateka wanaowateka vitani au wanaoshindwa kulipa madeni yao.
Wayahudi waliteremshiwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.) vitabu vitatu vitakatifu kupitia Mitume yao mitatu vinavyowahusu Wayahudi tu. (i) Zaburi kwa Mtume Dawood (a.s.). (ii) Tawrat kwa Mtume Musa (a.s.) na Injili kwa Mtume Isa (a.s.). Juu ya kufanyiwa hivyo na Mwenyezi Mungu walikuwa wanajiona na kusema kuwa wao ni viumbe teule vya Mwenyezi Mungu.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'an takatifu: "Na Wayahudi na Wakristo wanasema: "Sisi ni watoto wa Mwenyezi Mungu na wapenzi wake, sema: "Basi kwa nini anakuadhibuni kwa ajili ya dhambi zenu? Bali nyinyi ni watu tu katika aliowaumba humsamehe amtakaye (asipotubia) (Qur'an 5, 18). Wayahudi walikuwa wanamgeuza asiyekuwa Myahudi mtumwa atakaposhindwa kulipa deni la Myahudi.
Ndugu Waislamu, Mji wa Makka ni mtakatifu kwa karne nyingi sana kuanzia enzi za Mtume Ibrahim (a.w.) kwa kuujenga Msikiti wa kwanza kabisa wa kuabudiwa Mola (s.w.). Ulikuwa wakati biashara ya utumwa ikifanyika. Zilikuwepo soko tatu za biashara hiyo. Soko la kwanza liliitwa Ukaadh la pili Dhiylmajaaz na la tatu Dhiymajana.
Katika soko la Ukaadh aliuzwa mmoja wa maswahaba wa Mtume Muhammad (s.a.w.) kabla ya kupewa Utume kwa muda mfupi Swahaba huyo ni Bwana Zayd bin Haarith (r.a.) alifuana na mama yake bibi Saada binti Thalaba kutoka nyumbani kwao kwenda kuwatembelea jamaa zao, na bado alikuwa mdogo hajafikia baleghe. Njiani alitekwa nyara na majangili ya Al Kays bin Jisr na kumuuza sokoni. Aliyemununua ni Hakiyam bin Hizam bin Khuweyeid kwa dirhamu miya nne, alimnunulia shangazi yake bibi Khadija binti Khuweylid mke wa Mtume Muhammad (s.a.w.) na mama wa watoto wake.
Bwana Mtume anapewa Utume na Mwenyezi Mungu Zayd (r.a.) alikuwa mwenyeji nyumbani kwa Mtume na alimuamini na kubakia kuishi na Mtume ijapokuwa baba yake mzazi alimtaka baada ya kufanikiwa kwa kumtafuta siku nyingi arejee kwake. Zayd (r.a.) alikataa baada ya kushauriwa na Mtume.
Alipotaka kuowa Bwana Mtume alimuozesha mtoto wa shangazi yake bibi Zaynab bint Jahsh na kuzaa naye mtoto mmoja Bwana Usama bin Zayd (r.a.). Na kwa muda mrefu watu walikuwa wanamuita Zayd bin Muhammad na Bwana Mtume hawakazi mpaka Mwenyezi Mungu mwenyewe atakapowakataza katika Qur;'an takatifu: "Wala hakuwafanya watoto wema wa kupanga kuwa wana wenu hasa, hayo ni maneno yenu ya vinywa vyenu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anayesema kweli naye huongoza njia (ya uwongofu) Waiteni kwa ubini wa baba zao maana huo ndio uadilifu mbele ya Mwenyezi Mungu (Qur'an 33, 4-5) Zayd (r.a.) alishiriki pamoja na maswahaba wenzake katika mapambano ya vita mbalimbali dhidi ya makafiri wa Makka walioupiga vita Uislamu, Wayahudi na Warumi. Bwana Mtume (s.w.) alimpa Uamiri wa kwanza wa jeshi la Waislamu akifuatiliwa na Bwana Jaafar bin Abiytwalib na Bwana Abdallah bin Rawala katika vita ya Muta Waislamu walipombana na Warumi. Na huko alipokufa shahidi.
Hekima ya Mwenyezi Mungu inaonekana wazi ya utekelezaji kwa vitendo vya kuonyesha usawa kati ya watu, ubora uliopo kati yao ni kumcha Mwenyezi Mungu aliyoutekeleza Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.) kwa swahaba wake Zayd (r.a.) kwa kumleya nyumbani kwake sawa na watoto wake mwenyewe, kuitwa kwa jina lake kama baba yake mzazi, kumuozesha mtoto wa shangazi yake bila ya kujali kuwa aliuzwa na kununuliwa.
Kwa hivyo basi Uislamu unapinga utumwa na ubaguzi wa rangi kutokana na Qur'an takatifu na Hadith za Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.) watu wote ni swa. Amesema Mwenyezi Mungu (s.w) katika Qur'an takatifu. "Na hakika tumewatukuza wanaadamu na tumempa vya kupanda barani na baharini na tumewaruzuku vitu vizuri na tumewatukuza kuliko wengi kuliko wengi tuliowaumba kwa utukufu ulio mkubwa (Qur'an 17, 70) Uislamu umeharamisha sababu zote zinazowafanya watu kuwa watumwa, kama vita vya aina yoyote ile, kwa sababu mateka waligeuzwa watumwa utekaji nyara wa baharini na nchi kavu.
Ndugu Waislamu. Dini ya Uislamu katika kutokomeza utumwa na kuwafanya watu ni swa imelazimisha Waislamu kutowa Zaka mafungu moja katika mafungu manane ni la watumwa. Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'an: Zaka hupewa mafakiri, maskini na wanazitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao juu ya Uislamu na katika kuwapa uungwana watumwa na katika kuwasaidia wenye deni...(Qur'an 9, 60). Na Mwenyezi Mungu amewataka wanaomiliki watumwa wawakubalie kujikomboa kwa kuandikiana nao mkataba wa kuwalipa na akasema: " Na wale wanaotaka kuandikiwa (wapate uungwana) katika wale iliyowamiliki mikono yenu ya kuume, basi waandikieni kama mkiona wema kwao na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu aliyokupeni (Qur. 24, 33). Uislamu umefanya kujikomboa kwa makosa anayoyafanya Muislamu ni kumpatia mtumwa uhuru wake. Kama vile kumuua Muislamu pasi na kukusudia. Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'an takatifu: "Na mwenye kuuwa Muislamu kwa kukosea basi ampe uungwana mtumwa wake mmoja aliye Muislamu. Vile vile malipo ya viapo na Al dhihaar ni kuwagomboa watumwa (Qur'an 5, 89 na 58,3).
Dini ya Islamu imwaamrisha wenye kumiliki watumwa au watumishi wa nyumbani waishi nao kwa wema. Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.) alimlaumu swahaba wake aitwaye Abdadhari Alghaffariy kama ilivyopokelewa na Maimamu mawili wa Hadith Bukhariy na Muslim wakati Abaadhariy alipomuabisha kwa rangi yake nyeusi : "Ewe Abaadharriy bado unazo kasumba za kijahiliya ndugu zenu ni watumishi wenu, Mwenyezi Mungu amewafanya kuwa chini yenu, na yeyote yule ndugu yake yuko chini yake amlishe anachokula yeye na amvishe anachovaa yeye, na wala asimtume kwa jambo asiloliweza kulifanya na kama akimtuma kufanya asiloliweza basi na amsaidie".
Khalifa wa kwanza wa Islamu Bwana Abubakar Al Siddik (r.a.) kwa imani yake kubwa na ukaribu wake alimgomboa Bwana Bilal bin Rabah (r.a.) aliyekuwa mtumwa wa kafiri mashuhuri mjin Makka Umaya bin Khalaf, na akawa huru kwa kugombolewa huko, na akawa akiadhini wakati wa sala. Alisema Khalifa wa pili Bwana Omar bin Al Khatab (r.a.) baada ya ugombozi huo: "Abubakar Bwana wetu amemgombowa Bwana wetu". Bwana Bilal (r.a.) alikuwa ni mtu wa Ethiopia, mweusi alikuwa mtumwa wa Khalaf bin Wahab alipokufa Khalaf mtoto wake Umaya alimrithi bwana Bilal (r.a.) kama mtumwa, na alisilimu na kumuamin Mwenyezi Mungu mmoja na kumsadiki Mtume Muhammad (s.a.w.). Alipojuwa Umaya kuwa Bilal (r.a.) amesilimu alimuadhibu sana ili asiendelee kuwa Muislamu. Vile vile Bwan Omar bin Al Khatab (r.a.) aliamrisha apigwe mtoto wa liwali wa Islamu nchini Misri Bwana Abdallah bin Amru bin Al Aas (r.a.) kwa kumpiga mtoto wa Kikristo bila ya kumkosea, baada ya hapo alisema Bwana Omar (r.a.) "Kwanini mnawafanya watu watumwa na hali wamezaliwa na mama zao waungwana".
Ndugu Waislamu. Wazungu wa Ulaya waliwavamia (Red Indians) nchini Marekani na kuwauwa na kuwadhulumu nchi yao. Kwa sababu wananchi halisi wa Marekani ni Red Indians walivyofanikiwa kuwanyang'anya na kugawana mashamba wakaja Afrika kufanya biashara ya utumwa. Wakawauwa watumwa na kuwapeleka Marekani kwa kuwalimia mashamba yao na kufanya kazi katika migodi yao ya dhahabu na almasi. Alipochaguliwa Rais Abraham Lincoln (1860-1865) aliwasaidia sana Wanegro wenye asili ya Afrika kwa kuwagomboa na utumwa. Rais Lincoln aliuawawa na mashabiki wa ubaguzi wa rangi anayependelea Wanegro wawe watumwa tarehe 14/4/1865.
Msimamo wa dini ya Islamu
wa kupinga utumwa na ubaguzi wa rangi ni imara wa haki kwa kila mtu sawa
na mwenzake, aliyebora ni anayemcha Mwenyezi Mungu. Amesema Mwenyezi Mungu
katika Qur'an takatifu: "Enyi watu kwa hakika tumekuumbeni nyote kwa yule
mwanamume mmoja (Adam) na mwanamke mmoja (Hawa) na tukakufanyieni mataifa
na makabila mbalimbali ili mjuwane tu. Aliyebora mbele ya Mola ni mcha
Mungu (Qur'an 49, 13.)
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |