Katibu wa Sheikh Mbukuzi akamatwa usiku


KATIBU wa Shura ya Maimamu na Imamu wa Msikiti wa Taqwa jijini Jumanne Ramadhani amekamatwa na polisi usiku wa kuamkia jana nyumbani kwake Mwananyamala.

Kwa mujibu wa mke wa Katibu huyo polisi wapatao 12 walifika mahali hapo saa sita usiku wakavunja mlango na kuanza kuwashambulia waliokuwemo.

Mama huyo ameeleza kuwa askari hao waliingia kila chumba cha nyumba hiyo wakapekuwa kabla ya kuanza kumpiga Katibu huyo, mkewe na shemeji yake kisha kuondoka naye.

Naye Imamu wa Msikiti wa Chihota, Tandika Sheikh Ali Mtawazi ameripotiwa kukamatwa na polisi usiku wa kuamkia juzi.

Imedaiwa kuwa sababu za kukamatwa Sheikh huyo ni hatua yake ya kumkaribisha Sheikh Mbukuzi kuhutubia waumini wa Msikiti huo wiki mbili zilizopita.

Hatua ya Imamu huyo imedaiwa kutowapendeza viongozi wa Bakwata ambao inasemekana walimripoti polisi kabla ya kukamatwa.

Lazaro imesema ni hali ya kusikitisha kuona yule anayetoa kauli kuihadharisha nchi na janga ndiye anayeitwa mchochezi na mvurugaji wa amani.

"Tunasema kuwa dhulma zilizoelezwa na Sheikh Mbukuzi kwa niaba ya Maimamu ndio hali halisi iliyopo hapa nchini", imedai Kamati hiyo mbele ya Waandishi wa habari jana katika majengo ya Msikiti wa Mwenge Jijini.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati hiyo Bi Fatma Lazaro alisema alichokizungumza Sheikh Mbukuzi ni ufafanuzi wa yale yaliyomo kwenye risala iliyosomwa na Alhaj Madabida mbele ya Rais Mkapa katika Baraza la Idd mwaka huu.

"Tukifanya maandamano ya amani kosa, tukizungumza bungeni udini, tukizungumza na waandishi wa habari kosa, sasa basi tufanyeje jamani? Hivi kwa vielelezo hivi, ni nani anayekusudia kuvuruga amani? Bila shaka ni serikali", alisema kwa uchungu mama huyo.

Kina mama hao pia wamedai kushangazwa na hatua ya serikali kumkumbatia Mufti wa Bakwata wakati Waislamu wenyewe hawamtaki.

Kuhusu suala la Mwembechai wamesisitiza kuundwa tume huru kuchunguza chanzo na wahusika waliosabaisha mauaji ya raia wasio na hatia.

Kadhalika wamelitaka jeshi la polisi kuzingatia kanuni na taratibu zake badala ya walichokieleza kusukumwa na vyombo vya habari au chuki binafsi dhidi ya jamii fulani ya Watanzania.

Sheikh Juma Mbukuzi alikamatwa juma moja lililopita baada ya kuzungumza na vyombo vya habari akihadharisha hatari inayoweza kulikumba Taifa kutokana na sehemu fulani ya Watanzania kukandamizwa kidini na kijamii.

Sheikh huyo alionya kuwa hali hiyo ya ukandamizaji inaweza kuligawa Taifa katika matabaka ya makabwela ambao ni Waislamu na walionacho ambao ni Wakristo.

Kauli hiyo ilitafsiriwa na vyombo vya dola kuwa ni ya uchochezi kwa mujibu wa sheria ya magazeti (Newspaper act) ya mwaka 1976 kifungu Na. 3.

Hata hivyo wakati vyombo vya dola vikitaharuki kwa na kauli ya Sheikh Mbukuzi waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania wamehadharisha kutokea umwagaji wa damu katika dayosisi ya Pare wilayani Mwanga.

Huko nyuma Maaskofu wa Kanisa Katoliki walitishia kumwaga damu kama mihadhara waliyodai kukashifu dini yao isingezuiwa.

Tamko hilo la umwagaji wa damu lilisainiwa na Askofu Josephat Lubulu kwa niaba ya Maaskofu wote wa Kanisa Katoliki.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook