Mzee Ponda awataka watendaji wa serikali wajiepushe na dhulma


BABA wa Katibu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu Bwana Ponda Issa Ponda, Mzee Issa Ponda amewataka watendaji wa serikali na vyombo vyake kuchunguza mambo kwa makini na moyo safi badala ya kukurupuka kwa jazba au chuki ambako hupelekea kuchukuliwa hatua ambazo mara nyingi huwa za dhulma na uonevu dhidi ya baadhi ya raia.

Aidha, amesema viongozi kutokuwa waadilifu ni chachu ya machafuko yanayoweza kuliangamiza Taifa.

Mzee Issa Ponda aliyasema hayo Jumamosi iliyopita wakati akizungumza na ANNUUR ilipomtembelea nyumbani kwake mtaa wa Kawawa Ujiji Kigoma.

Mzee huyo alionya kuwa ipo hatari ya nchi kugawanyika iwapo wenye dhamana ya uongozi watashindwa kusimamia haki na usawa kwa wananchi wote bila ya kubagua.

Mzee Issa aliliambia gazeti hili kuwa matarajio Watanganyika kabla ya uhuru yalikuwa kujenga taifa jipya litakaloongozwa na wananchi wenyewe kwa kuzingatia haki na usawa.

"Wale wenye dhamana hivi sasa wasidhani haya yaliyopo yalikuja yenyewe, ni jitihada iliyofanywa huko; wasione vinaelea vimeundwa", aliasa mzee huyo ambaye ni miongoni waliokuwa mstari wa mbele katika harakati za kudai uhuru.

Akikumbushia historia ya mapambano ya uhuru, Mzee Issa alisema yeye ni katika waasisi watano wa mwanzo kabisa wa chama cha TANU mkoani Kigoma.

Alisema TANU ilipokelewa Kigoma kwa mara ya mwanzo kwa njia ya mazungumzo ya mtu na mtu.

"Niliwakuta jamaa zangu wanne wakijadili habari ya TANU na uhuru ingawa niliona kama ni mazungumzo yasiyowezekana lakini niliungana na jamaa hao", alisema mzee huyo mwenye umri wa miaka 78 hivi sasa.

Aliwataja wenzake washiriki wa mazungumzo hayo kuwa ni Ali Kosta, Msafiri Muwanda, Majuto Goba na Marzuku Msazi.

Kuhusu kuenea kwa TANU na wazo la uhuru mkoani Kigoma Mzee Issa alisema harakati zilipamba moto baada ya kufanyika kwa mikutano kadhaa iliyohutubiwa na wajumbe wawili kutoka Dar es Salaam Bwana Oscar Kambona na Bwana Kasela Bantu.

Alisema hotuba za viongozi hao wa TANU Taifa ziliwahamasisha wakazi wa Kigoma ambao baadaye walifungua ofisi eneo la Ujiji iliongozwa na Katibu wake wa mwanzo Suleiman Mtumwa.

Hata hivyo, Mzee Issa alisema Katibu huyo aliondolewa katika uongozi baada ya kugundulika kuwa alikuwa akitumiwa na serikali ya kikoloni.

Alisema TANU ilipata nguvu zaidi mkoani Kigoma baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa Mwalimu Nyerere kutembelea mkoa huo ambapo yeye na wenziwe wanne walipewa jukumu la kumtembeza maeneo mbalimbali ya Ujiji ikiwa ni pamoja na kumzungusha ziwani (Tanganyika) kwa mtumbwi (ngalawa).

"Nakumbuka ilikuwa saa tatu asubuhi siku ile tulipomchukua Mheshimiwa (Nyerere) hadi ziwani tukampakia katika mtumbwi mimi nikiwa mmoja wa wapiga makasia", alieleza kwa ufasaha Mzee huyo maarufu mkoani Kigoma.

Aliongeza kuwa "baada ya kumzungusha ilitoka rai kuwa Mheshimiwa anyweshwe maji kwa kasia ili asiweweseke na mimi ndiye niliyemywesha maji hayo.

Mzee Issa pia alimueleza mwandishi kuwa yeye ni miongoni mwa wanachama wa TANU waliohudhuria mkutano wa kuamua kushiriki au kutoshiriki kura tatu mwaka 1958.

Alisema ingawa hakuwa mjumbe aliyeteuliwa kimkoa alikwenda kwenye mkutano huo (kwa nauli yake) ili apate fursa ya kushiriki tukio lile la kihistoria.

Kuhusu kusakamwa kwa mwanae na vyombo vya dola, Mzee Isa alisema yeye hashangazwi na hilo kwa kuwa Qur'an imeweka wazi dhulma za watawala wanaokaidi amri za Mwenyezi Mungu.

"Mimi namuunga mkono huyu bwana mdogo kwa sababu hicho anachokipigania ndicho nilichomfundisha na katika kufanya hivyo nafahamu matokeo yake", alisisitiza.

Pamoja na maelezo hayo Mzee Issa aliwaasa Waislamu kushikamana kikamilifu na mafunzo ya dini yao ambako kutawafanya waibuke washindi dhidi ya maadui zao.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook