Maoni yetu


Msikubali kuyumbishwa


MIONGONI mwa hazina waliotuachia wazee wetu katika harakati zao za kuikomboa nchi hii ni mbinu za kuitambua mipini na mashoka na namna ya kuyashughulikia yote mawili.

Wakati wananchi wakiimarisha TANU wakoloni walianzisha na kuipa nguvu UTP. Lengo likiwa kuwafanya wananchi wapambane wenyewe kwa wenyewe wale wa TANU na UTP.

Hata hivyo wazee wetu yote hayo waliyaona; hawakupoteza nguvu zao kupambana na mipini bali waliimarisha nguvu zao kulikabili shoka na mwenye shoka lake.Toka Amir wa Shura ya Maimamu azungumze na waandishi wa habari na hatimaye kukamatwa na polisi, vyombo vya habari vimekuwa vikioanisha kukamatwa kwake na kauli iliyotolewa na Bakwata.

Picha inayojengwa ni kuwa serikali imemkamata kutekeleza maelekezo na ombi la Bakwata.

Kama Waislamu wataimeza propaganda hii kinachotarajiwa ni kuwa wataelekeza hasira zao kwa Bakwata, wapambane wenyewe kwa wenyewe.

Waislamu wanajua tatizo lao si Bakwata bali aliyeianzisha na anayeendelea kuilazimisha juu yao.

Aidha, tatizo lao sio yule anayetoa kauli inayotangaza kiwango cha ' ukibaraka' wake bali yule anayewadhulumu Waislamu na akadhani atawanyamazisha kwa kuwatumia vibaraka.

Azma hii ya kuwapeleka Waislamu kusiko ni ya hatari kwani yaweza kuwafanya washughulikie na watu wasio husika; watu wasio na uwezo wala uzito wowote.

Kama ipo hatari ni hii ya Waislamu kuuliwa na mpaka leo wauaji wasifike mahakamani.

Lakini kama Rwanda wangekubali kuyumbishwa, leo Askofu mtuhumiwa wa mauaji ya halaiki asingekuwa mahakamani. Lakini hawakuyumba walishikilia wauaji wafikishwe mahakamani na leo wako kizimbani.

Kwa Waislamu wa Tanzania tunaamini nao hawatakata tamaa kwani waliowaua hawapo juu ya sheria wala katiba. Na wala hawana nguvu inayozidi nguvu ya wananchi.

Si jambo la kunong'ona tena kwamba ipo dhulma dhidi ya Waislamu. Na alichosema Sheikh Mbukuzi ndicho kile kile alichoelezwa Rais Mkapa na Kamati ya Alhaj Madabida na kuahidi kushughulikia.

Walichotahadharisha Waislamu ndicho inachotahadharisha Jumuiya ya Kimataifa na kuilaumu serikali ya Tanzania kwa kuyakalia madai ya Waislamu bila kujali kuwa hatua hiyo yaweza kuilipua nchi.

Wanachosema Waislamu ni kuwa dhulma ipo ndio maana mpaka leo Lwambano na polisi waliowaua Waislamu hawajakamatwa. Bali anakamatwa yule anayeikumbusha serikali iwakamate wachochezi na wauaji hao!

Waislamu wanaziona hali zao na nafasi zao makazini na huko mitaani. Kwa lugha yoyote itakayotumika wao ni tabaka la chini. Na yeyote atakayeisemea hali hii haiwakilishi nafsi yake binafsi bali huwakilisha hisia na yale yaliyopo kwa Waislamu.

Kama upo uzushi au uongo katika madai ya Waislamu hilo ndilo la kujibiwa.

Shura ya Maimamu ipo na Waislamu wenyewe wapo watazungumza na kutoa maelezo.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook