Ukandamizaji ulichochea machafuko Soweto - 4


Wazalendo walioishi kinyonge nchini mwao miongo kadhaa walitambua ukombozi uko baina ya uhai na umauti. Ilikuwa hapana budi kujitoa muhanga wa nafsi kuyakabili mateso, majeraha, vifungo na vifo kupigania usawa.

Hali hii inaweza kuzinyemelea nchi zilizoonekana kuwa mstari wa mbele kuwapinga wabaguzi wa Afrika ya Kusini huku zenyewe zikipita njia ile ile. Kajisemea kweli Mhusika "mfungwa namba 6" katika Tamthilia maarufu Kaptula la Marx kuwa "tukitoka jela tutakomesha uongozi wote wa kinafiki". Endelea...

Kadiri utawala wa makaburu ulivyodumisha ubabe, vitisho na ukandamizaji, ndivyo wazalendo hususan wanafunzi walivyoendelea kuhamasika kupigania ukombozi. Harakati zilipamba moto katika vitongoji vyote vya wazalendo hao.

Maandamano makubwa yalipangwa kufanyika Agosti 23 hadi 25. Uhamasishaji wa chini chini ulifanyika siku za mapumziko Jumamosi Agosti 21 na Jumapili Agosti 22.

Vikaratasi vilivyokuwa na maneno "Azikwelwa madoda" yaani "kaeni majumbani" vilisambazwa maeneo yote ya kitongoji cha Soweto. Karibu kila nyumba ya mzalendo ilipata kijikaratasi hiki.

Mbali ya kuwataka watu wagome kwenda kazini karatasi hiyo pia ilikumbusha migogo ya miaka 1950 na kuelezea mafaniko ya kila hatua ya harakati.

Siku ya kwanza ya mgomo Agosti 23 asilimia 80 ya wafanyakazi waliitikia wito wa "Azikwelwa Madoda".

Gazeti la Rand Daily Mail liliripoti kwamba mgomo wa halaiki ulihusisha wafanyakazi wa kawaida na maafisa.

" Viwanda vya nguo takriban 300 vilifungwa kufuatia mgomo huo. Baadhi ya viwanda hivyo karibu wafanyakazi wote hawakufika kazini.

Ili kuficha ukubwa wa mgomo ule Kaburu Kruger kupitia redio ya Taifa alidai ni kikundi cha watu wachache kilichochea mgomo ule kwa kutawanya vijikaratasi vya uchochezi.

Alidai jumuiya ya ANC ambayo ilipigwa marufuku ilihusika na uchochezi huo.

Johannesburg Chamber of Commerce iliripoti kwamba mgomo huo uliwaathiri zaidi wenye viwanda, wauzaji wa jumla na makampuni ya bima.

Tofauti na machafuko ya mwanzoni mwa Agosti, sasa wazalendo walifahamu kile walichopigania na kila mmoja alikuwa tayari kwa matokeo yoyote.

Wafanyakazi wengi wa viwandani na maofisini hasa makarani wa utumishi waliunga mkono harakati za ukombozi huku wakijua kufanya hivyo kungehatarisha ajira zao.

Licha ya kuwepo vitisho na wasiwasi kutoka kwa watawala hakuwepo mzalendo halisi wa Soweto aliyehiari kukandamizwa kwa kuogopa virungu na risasi, gereza au kupoteza kazi.

Katika baadhi ya sehemu walionekana wafanyakazi wachache wakielekea makazini chini ya ulinzi mkali wa polisi. Hata hivyo wengi wa wafanyakazi hao walikuwa wahamiaji.

Migomo iliendelea Septemba 13 ambapo ilikadiriwa zaidi ya wafanyakazi 175,000 waligma kufanya kazi.

Septemba 14 polisi ilianza kuwashambulia watu hasa vijana.

Kufuatia hatua hiyo ya polisi vurugu zililipuka tena ambapo reli ziliharibiwa pamoja na majengo kadhaa ya serikali.

Watu 12 waliripotiwa kuuawa katika vurugu hizo. Wazalendo wa Soweto walifanikiwa kujenga mshikamano uliowawezesha kutoa upinzani mkali kwa polisi. Vivyo hivyo hali ilikuwa ngumu zaidi katika mji wa Alexandra ambako wafanyakazi wote waliitikia wito wa "Azikwalwa Madoda" Septemba 14.

Polisi kwa hasira ilianzisha msako wa nyumba kwa nyumba kuwasaka "wachochezi" na "wakorofi" huku ikiwaamrisha watu kwa nguvu kwenda makazini.

Wale waliopinga amri hiyo walikamatwa na kupelekwa vituoni.

"Zaidi ya watu 800 walikamatwa katika msako huo hali iliyolipua machafuko makubwa katika nji wa Alexandra", ameandika Dk. Valentin katika Life and Struggles of a South Afican Township.

"Harakati za ukombozi Afrika Kusini zilizoanza kwa maandamano ya wanafunzi Juni 16 ziliingia katika awamu mpya iliyowaunganisha wazalendo wote katika kambi ya makabwela, wanaokandamizwa katika nchi yao".

Sera za ukandamizaji ziliibua harakati za kitabaka zilizoiingiza nchi katika machafuko makubwa.

Septemba 15 karibu wafanyakazi 200,000 waligoma kwenda makazini katika jimbo la Transvaal.

Hata wafanyakazi wahamiaji walishiriki mgomo huo kutokana na kuchukizwa na mateso ya serikali dhidi ya wananchi wanyonge. Machafuko zaidi yaliripuka katika kitongoji cha Tambisa mnamo Septemb 20 ambako vilitawanywa vikaratasi vilivyowataka wafanyakazi wasiende makazini kuunga mkono wito uliotolewa katika miji ya Soweto na Alexandra.

Vikaratasi vilivyosambazwa vilikuwa na maneno yaliyodai " Sisi jamii ya weusi hatuna cha kupoteza katika mgomo huu zaidi ya minyonyoro yetu. Tuwatetemesha wakandamizaji! Mbiu yetu ni hii: "Ukandamizaji uangushwe!!! Nguvu iko kwa Umma!!!

Itaendelea toleo lijalo.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook