Bakwata yaagana rasmi na Waislamu
Historia inaonyesha siku zote kuwa vibaraka hawatabiriki. Kwa mfano katika miaka ya themanini Wamarekani na ujanja wao wote walipata mshituko mkubwa pale kijana wao Manuel Noriega - Kijana waliyempandikiza kuitawala Panama kwa ajili ya kulinda maslahi yao katika mfereji wa Panama baada ya mauaji ya rais Umar Torijos aliyekuwa mpinzani mkubwa wa maslahi hayo, alipowageuka.
Walishituka kwa sababu walidhani walikuwa wakimjua vizuri Noriega. Dhana hiyo ilitokana na ukweli kwamba Noriega alikuwa jasusi wao wa siku nyingi kupitia shirika lao la ujasusi la CIA na waliamini kuwa majasusi wa shirika hilo ni maroboti ambayo yalishauza utu wao na roho zao kwao.
Jirani zaidi na hapa nyumbani, yanayoendelea hivi sasa kule Congo (Zaire) ni mfano mwingine. Rais Museveni wa Uganda na Bwana mkubwa wa Rwanda, Generali Pauli Kagame kwa pamoja walipanga kuipata Zaire kupitia mgongoni mwa rais wa sasa wa nchi hiyo Bwana Laurenti Kabila.
Wakati Museveni yeye akielekeza zaidi macho yake kwenye utajiri mkubwa unaopatikana Congo Generali Kagame alijikita zaidi kwenye ndoto yake (na Watutsi wenzake)ya kupanua himaya ya Kitutsi eneo la maziwa makuu.
Wote wawili walijua wakisha msimika Kabila ndani ya Ikulu ya Kinshasa, basi mchezo utakuwa umekwisha. Lilikuwa kosa , kwani baada ya miezi michache tu baada ya Kabila kukalia vizuri kiti aliwageuzia wote wawili kibao na kutangaza hadharani kuwa serikali yake ilikuwa haihitaji Waganda na Wanyarwanda nchini humo.
Matokeo yake ni kuwa Museveni na Kagame hawakuwa na chaguzi, bali kutafuta 'vibaraka' wengine na kuzua vita mpya kwa lengo la kumung'oa Kabila.
Mifano ya aina hii ni mingi sana ulimwenguni na wala hamna namna yoyote ile ambayo mtu anaweza kuinukuu yote
Mwaka 1968 jumuiya za Kiislamu zilivunjwa na kuundwa BAKWATA na kuilazimisha juu ya vichwa vya Waislamu Baada ya hapo kazi ya kuusambaritisha Uislamu na kuwaswaga Waislamu ikawa mteremko.Mpini ukawa umepatikana na shoka lililohujumu miti msituni.
Qur'an ilipochanwa Mwanza hakuna mwingine ila Mufti wa BAKWATA aliyesimama akatangaza hadharani kuwa kilichochanwa si Qur'an bali ni 'Kijiyasini'. Waislamu walipochoshwa na najisi ya nguruwe na wakaamua kuondoa kadhia hiyo kwa mikono yao, hakuna mwingine bali BAKWATA aliyesimama hadharani na kuiomba dola kuwachukulia Waislamu hatua kali kabisa ili kesho na keshokutwa wasije wakapata ujasiri wa kuteketeza viwanda vya pombe.
Walipotoka Waislamu wakakusanya nguvu zao kujiundia taasisi za maendeleo yao kama mashule n.k. , BAKWATA wakawa msitari wa mbele kuiomba dola kuzuia juhudi hizo kwa kuwa wao BAKWATA hawajatoa kibali.
Mazingira ya kisiasa ya miaka ya sitini, sabini na hata themanini - yakiwa ni ya udikteta wa chama kimoja, yalirahisisha sana kuusambaratisha Uislamu katika mataifa kama ya Urusi, China, Tanzania n.k. kupitia kwenye taasisi rasmi.
Hata hivyo kusambaratika kwa udikteta wa chama kimoja mwanzoni mwa miaka ya tisini kumetoa mwanya mkubwa wa kusambaratika kwa Uislamu wa kuchongwa . Kwa mfano haikuchukua zaidi ya miezi miwili baada ya rais wa zamani wa Urusi Michael Gorbachev kutangaza kuruhusiwa kwa mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini humo kabla ya BAKWATA la huko kuitaka serikali kuwarejeshea Waislamu msahafu wao wa Othman na kuirejesha misikiti ambayo ilikuwa imegeuzwa majumba ya makumbusho.
Na huko Uchina kufuatia mabadiliko makubwa ya kiuchumi yaliyofanywa na marehemu Deng Tsiao Ping baada ya kifo cha Mao ze Dong, BAKWATA la huko limekuwa msitari wa mbele kufanikisha juhudi za Waislamu wa huko kuujenga upya Uislamu kama ulivyofundishwa na Mtume (S.A.W.).
Jambo la kufurahisha ni kwamba hata hapa Tanzania Waislamu wameamka na kupania kuimarisha Uislamu wao. Mabadiliko ya kisiasa yaliyojitokeza, hata hivyo hayajaweza kuusambaratisha mfumo wa dola ambao tangu mwanzo umejengwa katika kuupa fursa zaidi ukiristo na kuufifisha Uislamu.
Hata hivyo kwa kiwango kikubwa mabadiliko hayo yameudhoofisha mfumo huo. Kwa mfano leo hii ni vigumu sana kwa dola kuzuia harakati za Waislamu kijiletea maendeleo yao, kwa kuitumia BAKWATA. Leo hii kila Muislamu anayejielewa anajua kuwa BAKWATA si chombo chenye nguvu zozote za Kisheria.
Jambo la ajabu ni kwamba BAKWATA imeamua kujitoa muhanga dhidi ya Waislamu bila sababu zozote za msingi. Kujitokeza kwa BAKWATA hivi karibuni kulaani juhudi za Waislamu kuleta haki na usawa ndani ya nchi yetu, kuna maanisha kuwa BAKWATA imeamua kuagana rasmi na Waislamu.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |