SUALA la amani na utulivu katika jamii haliwezi kutenganishwa na uhuru, usawa na haki za raia katika jamii. Aidha, uadilifu na kuchunga amana ya uongozi kwa viongozi ina umuhimu wa pekee katika kuimarisha na kudumisha amani, upendo na umoja miongoni mwa watu wa makundi mbalimbali katika jamii.
Ilivyo kawaida wananchi wenyewe wa dini , makabila na koo mbalimbali hawana chuki miongoni mwao. Huishi pamoja mitaani wakishirikiana na kusaidiana kwa shida na furaha.
Hali itaendelea kuwa hivyo muda wa kuwa viongozi wa nchi watawatizama watu wote kama wananchi wenye haki sawa kama ambavyo inatarajiwa kuwa ishaelezwa kwenye Katiba na sheria za nchi.
Endapo uadilifu utawashinda viongozi matendo yao yakadhihirisha upendeleo, sumu hii haitoishia kuathiri mahusiano baina ya viongozi na wananchi, lakini pia yatathiri maelewano baina ya makundi mbalimbali katika jamii.
Haitoshi wala haisaidii kwa viongozi wa kisiasa kutangaza kuwa nchi haina sera wala sheria za kuwabagua wananchi. Muhimu ni utendaji wao. Kauli haisaidii kama haitafsiriwi na vitendo.
Lakini haitoshi pia wala haisaidii kwa viongozi kutoa shutuma na makemeo makali kila leo kwamba watu wasivuruge amani iwapo baadhi ya watu watakuwa na sababu za msingi za kuhisi kuwa wanaonewa; wananyanyaswa na hawatendewi haki.
Na mambo katika jamii yoyote ile huchochewa na kuharakishwa na mambo yafuatayo: Uonevu, ukandamizaji, dhulma na ubaguzi.
Hata hivyo haitarajiwi athari ya vichocheo hivi ikazuka ghafla. Kama vile ambavyo joto huyaathiri maji kidogo kidogo na kuanza kutokota na kufoka inapofikia nyuzi za joto 100 (100 oC). Vivyo hivyo huwa machafuko katika jamii. Huchukua muda hadi kufikia hatua ya wananchi "kulipuka" na kuvaa joho lao la uwananchi kujifungua minyororo wanayohisi inawapora utu wao na heshima yao.
Mara nyingi wanasiasa na vyombo vya dola wamekitafsiri kipindi hiki cha kujikusanya na kujiimarisha kwa athari za uonevu kama ni ishara ya ushindi na mafanikio ya utumiaji wa mabavu dhidi ya malalamiko na madai ya wananchi.
Wanachoshindwa kuelewa ni kuwa maadhali moto unaendelea kuwaka hakuna namna ya kuyazuia maji yasichemke ifikapo 100 oC.
Kwa binadamu anayetawaliwa na kuongozwa na matamanio ya nafsi yake, lililo muhimu kwake ni maslahi yake binafsi hata yakiwa ya muda mfupi na yenye maangamizi kwa wengine na kwa nchi ukitizama maslahi ya kudumu kwa wote.
Hawa ndio wanaoridhia dhulma iendelee ili muradi tu wao ndio wanaofaidika kutokana na mfumo uliopo. Hutamani hivyo hata kama athari ya mfumo huo hatimaye ni kuliangamiza Taifa. Hao hata ukiwatajia mifano hai kuwa sababu zilizopelekea Burundi na Rwanda ya leo ni haya haya wanayoyafanya Tanzania leo wanajifanya hawakuelewi.
Lakini haiyumkini kwa
mtu ambaye hutanguliza busara zake, uwezo wake wa kufikiri na akawa ni
miongoni mwa "Ulul'albaab" akautanguliza ubinafsi wake dhidi ya
maslahi ya kudumu ya Taifa.
--
|
|