Serikali kuwasuluhisha Wakristo waliotangaza kumwaga damu
 

WAZIRI Mkuu Bw. Frederick Sumaye anatazamiwa kuyasuluhisha makundi ya waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri ambayo yalitangaza kumwaga damu wiki mbili zilizopita wilayani Mwanga kufuatia mzozo katika Dayosisi ya Pare.

Kwa mujibu wa habari zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari, Waziri Mkuu anakwenda Mwanga kufuatia barua iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Walutheri wa Mwanga Bw. Onesmo Sabuni ambayo ilitoa onyo kuwa damu ingemwagika katika vurugu zinazoendelea katika Makanisa yao.

Vurugu hizo zimeripotiwa kutokea baada ya waumini waliojitenga na Dayosisi ya Pare kuzuiwa kuanzisha Dayosisi ya Mwanga.

Sehemu ya barua ya waumini hao ilidai kuwa kama si busara ya wana Dayosisi ya Mwanga Wilaya hiyo ingekuwa uwanja wa vita.

Awali mgogoro huu ulivyoibuka baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa waumini hao waliwahi kupambana wakafyekeana migomba na mahindi pamoja na kukatakata mifugo.

Wakati Waziri Mkuu akichukua hatua ya usuluhishi kumaliza vurugu katika Dayosisi ya Pare ambayo waumini wake wametangaza kumwagika damu, serikali hivi karibuni imemweka rumande Amir wa Waislamu Sheikh Juma Mbukuzi akidaiwa kutamka maneno ya uchochezi ikiwa ni pamoja na kuhadharisha kuwa damu inaweza kumwagika kama serikali haitachukua hatua ya kushughulikia madai ya Waislamu.

Sheikh Mbukuzi alitamka maneno hayo katika mkutano na waandishi wa habari Septemba 15, mwaka huu Msikiti wa Mkwajuni Jijini.

Kabla ya kukamatwa Amir Mbukuzi Bakwata ilidaiwa kutoa tamko juu ya uhalali wa Shura ya Maimamu ambapo baraza hilo lilidai ya kuwa Amir wa shura hiyo ni muhuni anayetakiwa kuchukuliwa hatua haraka.

Kwa muda mrefu Waislamu nchini wamekuwa wakiituhumu serikali kuwa inawapendelea Wakristo katika masuala mbalimbali ya kidini na kijamii.

Viongozi wengi wa serikali wamedaiwa kuwa na muelekeo wa kuwajali zaidi viongozi na waumini wa dini ya Kikristo hata kufikia kutekeleza baadhi ya madai yao ambayo huwa dhidi ya waumini wa dini nyingine.

Baadhi ya matukio ambayo yamekuwa yakidaiwa kuwapendelea Wakristo ni pamoja na kukamatwa mara kwa mara kwa wahubiri wa dini ya Kiislamu kwa kuhubiri Yesu si Mungu.

Tukio kubwa katika mfululizo huo ni lile la Paroko Lwambano kuitaka serikali kuwachukulia hatua wahadhiri wa Kiislamu ambao alidai wanakashifu dini ya Kikristo.

Madai ya Paroko Lwambano yalitekelezwa kwa kuuliwa Waislamu katika Msikiti wa Mwembechai mwezi Februari mwaka jana.

Kwa upande mwingine baadhi ya watu hudai kuweko kwa hatua za vyombo vya dola zinazoashiria chuki walizonazo baadhi ya watendaji wa vyombo hivyo dhidi ya Waislamu.

Aidha, matamko mbalimbali yamekuwa yakitolewa na viongozi wa juu wa nchi kuwakemea Waislamu kuwa ni watu wa vurugu wasiopenda amani miongoni mwao na kwa waumini wa dini nyingine.

Wakati huo huo, Maimamu wamedai kubaini harakati za vyombo vya dola zenye muelekeo wa kujenga mazingira ya kutaka kuwahujumu Waislamu hivyo wamelazimika kuahirisha maandamano ambayo yalipangwa kufanyika leo (Ijumaa Oktoba 1, 1999).

Harakati hizo maimamu hao wamedai kuwa ni pamoja na kuandaliwa watu kufanya fujo wakati wa maandamano sambamba na taarifa za ubandikaji wa makaratasi yanayodaiwa kutoa vitisho kwa Kamanda wa polisi bwana Alfred Gewe na Mufti wa Bakwata Sheikh Hemed Bin Jumaa.

" Kama taarifa hizo zimelenga Waislamu, ifahamike kuwa sisi hatuna ugomvi na mtu wala baraza, tunataka serikali ijibu malalamiko yetu, hizo ni propaganda zenye lengo la kuwaonesha Waislamu kuwa ni watu hatari wenye kustahili kushambuliwa na vyombo vya Dola bila huruma", amedai Sheikh Shaaban wa msikiti wa Mwenge jijini wakati akihojiwa na Mwandishi wa habari hizi kuhusiana na vitisho hivyo juzi.

Aidha Imamu huyo aliiomba serikali ishughulikie malalamiko ya Waislamu kama inavyofanya kwa Waumini wa dini nyingine badala ya kutafuta visingizio vya kukwepea majukumu.

Mwanzoni mwa wiki hii vyombo vya habari viliripoti taarifa kwamba katika baadhi ya sehemu za jiji zimebandikwa makaratasi yenye kutoa vitisho dhidi ya viongozi wa Bakwata na jeshi la polisi.

Makaratasi hayo ambayo yamedaiwa kubandikwa na watu wasiojulikana yameonekana katika baadhi ya kuta katikati ya jiji na eneo la mbagala. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook