Muasisi wa TANU asikitishwa na viongozi
 

MUASISI wa Chama kilichodai uhuru wa nchi hii TANU Ujiji Kigoma Mzee Issa Ponda (78) ameelezea kusikitishwa kwake na jinsi viongozi wasivyojali malalamiko ya wananchi.

Mzee Issa amesema wananchi wangetegemea serikali waliyoichagua ishughulikie yale yanayowakera ikiwa ni pamoja na kuwaandalia mazingira ya kujiletea maendeleo.

Amesema hali hiyo haipo badala yake Wananchi wamekuwa wakihimizwa kushiriki chaguzi ambazo huwaweka madarakani watu ambao wameshuhudiwa kugeuza dhamana hizo kuwa fursa ya kujinufaisha wao na walio karibu nao kikabila au kidini.

Mzee Isa amesema mikutano ya siasa kabla ya uhuru ilikuwa ikilaani sera za serikali ya mkoloni ambazo hazikuwa zikijali matakwa na hisia za wananchi walio wengi ambapo amesema zilikuwa zikiwaathiri badala ya kuwanufaisha.

Mzee huyo ameshangazwa kuona yale yale ya kabla ya uhuru yakiendelea katika serikali huru.

Huko nyuma mzee Issa alimweleza mwandishi, Waislamu walikuwa wakilalamika kutokutendewa haki katika masuala ya elimu na haki nyingine za kiraia.

"Serikali ya mkoloni ilikuwa ikipuuza malalamiko hayo hali iliyotufanya tudai uhuru, ni mambo haya haya ya kuonewa yaliyotuhamasisha", mzee Issa alieleza.

Katika masuala ya dini mzee Isa alieleza kuwa ujiji ilisifika kwa kutoa wajuzi wengi wa dini ya Kiislamu.

Alisema yeye alipata kuwa wakala wa mauzo ya vitabu vya dini vilivyokuwa vikiandikwa na kuchapishwa na aliyekuwa Kadhi wa Zanzibar na Ulamaa maarufu wa dini ya Kiislamu wa Afrika Mashariki Almarhumu Sheikh Abdallah Farsy.

Akizungumzia harakati za uhuru Ujiji, mzee Issa alisema TANU iliingia Kigoma mwaka 1955 wanachama wa awali ni yeye na wenziwe wanne.

Harakati za TANU zilishamiri mkoani humo miaka miwili baadaye baada ya vikao kadhaa vya siri na hatimaye mikutano ya hadhara iliyohutubiwa na wanasiasa maarufu kutoka Dar es Salaam.

Mzee Issa amesema alishiriki vikao mbalimbali vya chama hicho Ujiji na nje ya Ujiji ikiwa ni pamoja na mkutano maarufu uliofanyika Tabora mwaka 1958.

"Baadhi ya vikao hasa mwaka 1959 nilikuwa nikimbeba kwenda naye huyu bwana mdogo (Ponda) wakati ule kalikuwa na miaka mitatu", ameeleza mzee Issa huku akisikitika kuwa mambo mengi ameyasahau.

Hata hivyo alisema wengi walioshiriki harakati hizo hivi leo familia zao zinataabika

Alilaumu mkoa wa Kigoma kuachwa nyuma kimaendeleo tangu nchi ipate uhuru.

"Inahuzunisha Kigoma kuwa hivi, hakuna shughuli za kufanya, vijana wengi hawana kazi, hali hii mpaka lini?", amelalamika mzee huyo.

Malalamiko ya Mzee Issa yanaelekea kushabihiana na kile alichokizungumza Amir wa Waislamu Jijini Sheikh Juma Mbukuzi kuwa sehemu fulani ya raia huenda ikafanywa ijihisi ukabwela katika nchi yao.

Kigoma ni moja ya mikoa nchini iliyo na Waislamu wengi hasa eneo la Ujiji. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook