ILI dua iwe "Mustajaba" ni lazima pasiwe na pazia baina ya mja na Mola wake. Lakini pia "khushui" imekuwa ni hitajio muhimu wakati wowote ambapo mja humuelekea Mola wake kwa dua. Ndio maana Qur'an imehimiza watu kufanya visimamo vya usiku na kufanya maombi yao kabla ya swala ya Alfajir.
Nyakati hizo mja anakuwa ameepukana na wahaka wa shughuli za kidunia na mazingira yanayomzunguka yametulia.
Japo ni katika tabia ya waja wema kufanya visimamo vya usiku, lakini tunadhani huu ni wakati wa kufanya kampeni maalum kuwahimiza Waislamu wote kuipata sunnah hii muhimu katika kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.
Waislamu hivi sasa tumekabiliwa na wakati mgumu; hakuna nusura bila ya msaada wa Mwenyezi Mungu. Tuitafute nusra hii kwa visimamo vya usiku; Itkaaf na Dua kabla ya swala ya Subhi.
Abu Aziz aliikabili serikali akaeleza yale yote yanayowasibu Waislamu huku akihoji kwanini Waislamu waliuliwa pale Mwembechai. Hakuna aliyejali busara yake ya kuitanabaisha serikali juu ya uonevu wanaofanyiwa Waislamu.
Ponda Issa Ponda naye alitekeleza wajibu wake kuelezea mlolongo wa historia ya madhila wanayofanyiwa Waislamu kinyume cha sheria na katiba ya nchi.
Badala ya kufuatwa ushauri wa kuunda tume huru ya uchunguzi na kuwafikisha mahakamani waliowaua Waislamu, akawa anasakwa yeye, huku wachochezi wa kweli, Paroko Lwambano na askari wauaji, wakiachiwa huru na kupandishwa vyeo.
Umma wa Waislamu haukukata tamaa, kamati ya akina mama ikiongozwa na Fatma Lazaro ilifanya ziara takriban nchi nzima kuelezea kadhia ya Mwembechai na madhila mengine yanayowasibu Waislamu. Na kote walikopita walisisitiza suala la tume ya uchunguzi na wauaji kufikshwa mahakamani. Hakuna aliyejali.
Kamati ya Alhaj Madabida ilifanya hivyo hivyo tena mbele ya Mhe. Rais. Ni kimya hadi leo.
Juzi Amir wa Shura ya Maimamu kaona akumbushie yale ambayo tayari yashafikishwa, jaza yake ni kuwekwa ndani.
Waislamu wanataka watoke kwa pamoja waeleze hisia zao kutoridhika na hali hii wanaambiwa mkitoka mtakiona, rungu la dola limeshanyanyuliwa tayari kuzua mtafaruku.
Hii ni hali ngumu na ya kutisha kwa Waislamu. Ni hali ambayo kuikabili kwake kunahitaji kujitoa muhanga kwa mali na kwa nafsi. Lakini juu ya yote Dua kwa Allah ili tupate msaada wake.
Ni kwa muktadha huu tunawaomba, tunawanasihi na kuwahimiza Waislamu wote wazidishe visimamo vyao vya usiku huku wakimsikitikia Allah juu ya hii hali inayotukabili.
Wazungu wapiga picha Madrasa na kukimbia
WAZUNGU wanne wakiongozwa na mama mmoja Mtanzania Septemba 1, mwaka huu wamedaiwa kupiga picha Madrasa "Omari Islamic School" ya mjini Tabora na kukimbia.
Kiongozi wa Madrasa hiyo Sheikh Kurwa Shauri ameliambia gazeti hili kuwa watu hao walifika katika Madrasa hiyo wakiwa katika magari mawili aina ya Toyota yenye namba za usajili TZD 2722 na AR 214.
Amesema kufuatia tukio hilo alichukua hatua ya kupeleka taarifa katika Kituo cha Polisi hata hivyo watu hao walitoweka mahali hapo haraka.
Sheikh Kurwa amewahadharisha
Waislamu kuwa makini na picha zilizochukuliwa na watu hao hasa zitakapooneshwa
kuombewa msaada na mtu yoyote.
--
|
|