Ukandamizaji ulichochea machafuko Soweto- 5
 

HARAKATI za wazalendo zilishamiri zaidi baada ya wafanyakazi weusi kuanzisha migomo. Mgomo wa siku tatu uliathiri vibaya viwanda katika eneo la Witwaterand na katika jiji la Cape.

Mgomo huo uliwaogopesha sana wawekezaji wa nje.

Maandamano makubwa yalifuatia baada ya mgomo yaliyounga mkono madai ya wanafunzi juu ya kuachiwa walioko viziuzini na kusitishwa kwa mauaji.

"Zaidi ya wafanyakazi wazalendo 500,000 walishiriki maandamano hayo jijini Johanesburg na Cape Town peke yake", liliandika jarida la Sechaba la 1977.

Wanafunzi nao waliandamana katika mtaa wa Eloff katikati ya jiji mnamo Septemba 28.

Vikaratasi vilivyokuwa na maandishi ya "tunakwenda mjini Eloff!!! katika pepo ya weupe" vilitawanywa mjini Soweto wakati wa maandamano hayo.

Vikaratasi hivyo viliwataka wanaandamanaji waelekee mahali yalipo majengo na mali za serikali katikati ya jiji la Cape Town.

"Maandamano ya kimapinduzi ya wazalendo yameleta wasiwasi mkubwa kwa weupe". "Tumenunua bunduki sasa tusonge mbele, Vorster asijidanganye kuwa atasimamisha jitihada zetu za kujikomboa", yalidai baadhi ya makaratasi yaliyosambazwa katika maandamano hayo.

"Tuelekee mjini! Twende Johannesburg! Twende Eloff waandamanaji waliimba huku wakipiga mayowe kudai wao ni kundi la wanadamu wanaoakandamizwa.

Mbiu yao ya vita ilikuwa Vorster "huwezi kutusimamisha".

Polisi ilifahamu mpango wa maandamano na ilijaribu kuyazuia yasiweze kupenya katika jiji la Johanesbugr. Walifanikiwa kuwazuia baadhi ya waandamanaji, hata hivyo wengi wao walifaulu kuendelea.

Ilikuwa majira ya saa mbili ya Septemba 23, vijana waliokisiwa kufikia 1500 wa mjini wa Soweto walifaulu kujikusanya katika kituo cha gari moshi wakilenga kuelekea katikati ya jiji.

Vijana hao wakiwa wamebeba mabango "waachiwe walioko vizuizini" waliandamana kuelekea mtaa wa Eloff eneo lenye maduka na shughuli nyingi katikati ya Johannesburg. Huko waliungana na wafanyakazi weusi, na hata wanafunzi Wazungu wa Chuo Kikuu cha Witwaersand waliunga mkono maandamano hayo.

Polisi wa kuzuia fujo wakitumia risasi za mipira na mbwa walisimama kuwazuia waandamanaji. Walisita kutumia risasi za moto katika eneo hili la "weupe".

Wanafunzi waandamanaji walipigwa na kuumwa na mbwa kisha walizolewa katika makarandinga hadi vituo vya polisi.

Maandamano hayo yaliisha baada ya saa moja na nusu huku watu 880 wakiwa wamekamatwa. Sambamba, polisi ilizuia maandamano mengine yaliyofanyika Soweto na Alexandra ambako risasi za moto zilitumika.

Dosari iliyojitokeza katika maandamano ya Soweto ni ile ya baadhi ya watu walioshiriki maandamano kuwa wahuni, walevi na wahalifu ambao walitumia fursa ya machafuko kupora bidhaa na mali mbalmbali mitaani.

Hata hivyo, hili lilikuwa la afadhali sana kuliko ukandamizaji wa serikali.

Matokeo na mafunzo yaliyopatikana katika machafuko.

Waraka wa Chama cha Kikomunist cha Afrika Kusini ziliandika juu ya tathmini iliyofanyika baada ya machafuko ya Soweto ambayo ilionesha kuwa "ulimwengu na utawala wa kibaguzi ulifahamu ya kuwa watu walifikia kiwango cha kukataa kuendelea kufanywa makondoo wanaopelekwa machinjioni, hawakuwa tayari kuwaachia wengine wawaamulie. Mapambano ya Soweto yalisaidia kuwafanya wazalendo wawe hadhiri kisiasa. Yaliinua kiwango cha utayari wa kujitoa muhanga katika harakati za ukombozi".

Kwa mujibu wa takwimu rasmi (za serikali) watu 575 wakiwemo Wazungu watano waliuawa katika machafuko ya Juni 16, 1976 mpaka Februari 28, 1977, liliripoti gazeti la Star la jijini Johannesburg Februari 29, 1980.

Hata hivyo, duru nyingine zilifahamisha kwamba idadi kamili ya watu waliouawa katika machafuko ya Soweto haifahamiki.

"Takwimu za serikali kuhusu mauaji ya Soweto zilificha ukweli", ameandika Z. Nkosi katika The African Communist.

Jarida moja linalochapishwa na International Defence na Aid Fund for Southern African lilikadiria zaidi ya watu 10,000 waliuawa katika machafuko ya mwaka 1976 katika kitongoji cha Soweto.

Mapambano ya Soweto yalianzishwa na wanafunzi wakiongozwa na Jumuiya yao ya SSRC, walikuwa waanzilishi na waendeshaji wa kampeni na utekelezaji. Lalamiko lao kubwa lilikuwa kwanini Kiafrikana kifanywe lugha rasmi ya masomo sambamba na mfumo wa elimu kandamizi. Yalilipua hasira iliyojengeka miongoni mwa wakazi weusi wa mijini ambao walionekana kama makabwela waliostahili kukandamizwa na utawala wa weupe.

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook