Barua ya wazi kwa Rais Mkapa:
 
Waislamu wamechokozwa vya kutosha
 

Mheshimiwa Rais;

NAPENDA kuchukua nafasi hii kuitanabaisha serikali juu ya madhila yanayokithiri dhidi ya Waislamu na Uislamu. Pamoja na madhara yake.

Madhila haya yamekuwa yakiletwa na viongozi wa dola na watendaji wengine wa serikali kwa makusudi kutokana na chuki zao binafsi juu ya Uislamu.

Huhitaji ushahidi wa kisayansi kutambua kuwa muuaji wa Waislamu pale Mwembechai anahitajika kufikishwa mahakamani, huhitaji ushahidi wa kisayansi kutambua kuwa Bw. Lwambano ana shitaka la kujibu kwa kuchochea mauaji pale Mwembechai, na haihitaji kuwa mwanasayansi kutambua kuwa ni kosa kwa askari polisi kuingia Msikitini (ama sehemu takatifu) na viatu.

Shere wanayochezwa na walivyokwishachezwa Waislamu juu ya imani yao imekuwa ni kubwa kupita kiasi, dharau inayooneshwa na iliyokwishaoneshwa inazidi kujenga mioyo na imani za Waislamu katika kuitetea dini yao isiharibiwe.

Mbinu zinazotumika katika kuwanyamazisha Waislamu katika Tanzania zinazidi kuongeza hamasa za Waislamu katika kuietetea dini yao. Si propaganda, vitisho, vifungo, ama mauaji yanayoweza kuzima vuguvugu la kuusimamisha Ufalme wa Allah (s.w.) hapa duniani. Mbinu hizo ni dhalili na dhaifu sana na zaidi ya hapo zinazidi kuwaonesha Waislamu ukweli wa wapinzani wao.

Ni vema serikali ikafahamu wazi kuwa uchungu wa kuondokewa na ndugu zetu bado haujakwisha, ni vema ifahamike kuzidi kuyakalia malalamiko ya Waislamu ni sawa na kuweka msumari wa moto kwenye kidonda. Mbegu inayopandwa ni mbaya na imezidi kumwagiliwa na mti kumea na hapo tutakapoanza kuchuma matunda yatakuwa ni machungu.

Kuendelea kuwabana Waislamu mashuleni, maofisini, mitaani na sasa hadi Misikitini ili wasitekeleze yale waliyoamriwa na Mola wao ni kuzidi kumwagia petroli kwenye moto ulikwisha waka.

Katika sehemu yoyote hapa duniani hakuna hata mmoja aliyekuwa mkandamizaji na mnyanyasaji ameweza kuishi milele na unyanyasaji huo. Na hali hizo huwa zinafikisha mahali watu wakaona kifo ni bora kuliko maisha.

Kuzidi kumkamata kiongozi wa Waislamu (Amirul Mu'uminiin) na kumfanya gunia la mazoezi ya polisi kukamata kwa sababu tu amesema yale yaliyo kweli kunazidi kuonesha umma wa Kiislamu ukweli na uwazi gani iliyonao serikali ya awamu ya tatu.

Kuzidi kumsakama Ponda Isa Ponda kwa kusema ukweli dhidi ya serikali kunazidi kuonesha viwango vya dhulma iliyopo nchini.

Kuzidi kuisimika Bakwata na kuifanya kuwa ndio msemaji pekee wa Waislamu hapa Tanzania ni kuzidi kujenga fitna iliyokubwa miongoni mwa wananchi na pia kwa serikali.

Kuendelea kuzidhihaki sheria za Kiislamu kuwa zimepitwa na wakati na watu wasio na elimu nako ni kuleta uchokozi ulio dhahiri dhidi ya Waislamu.

Hali hizo hapo juu zinaonesha dhahiri kabisa uchochezi usio mipaka. Tafsiri ya amani kwa Uislamu na Waislamu ni pana sana, haishii katika hali ya kutokuwa na vita tu. Tafsiri ya amani kwa Muislamu hamfikishi yeye kukaa na kubweteka na kuwa kama mjinga. Amani ya kweli hupatikana pale ambapo hapana ukandamizaji wala uonevu. Amani halisi itapatikana pale ambapo haki itatendeka kwa kila upande. Amani ya kweli itapatikana pale ambapo fursa sawa bila upendeleo zitatolewa kwa wananchi wote bila kujali tofauti zao.

Waislamu Tanzania hawapiganii kutaka upendeleo bali wanachohitaji ni uadilifu wa serikali na watendaji wake kwa raia wote. Hivi sasa umefika wakati muafaka kwa manyanyaso ya dola dhidi ya viongozi wa Waislamu yasitishwe ili kuleta mshikamano.

Hivi sasa umefika wakati mzuri wa kujenga madaraja kwa chuma cha pua na sio maboksi yatakayolowana wakati wa mvua. Sasa ni muda muafaka wa kuyaandaa mambo kwa akili huru bila kutumia hila kutafuta tatizo ama matatizo ya Waislamu. Ni muda wa kuacha propaganda na kutumia vyombo vya habari katika kuupotosha ukweli kwa maslahi ya muda mfupi tu hapa duniani.

Sio muda wa kuendelea kujenga misamiati ya nitayashughulikia, natafuta ushahidi wa kisayansi, bali ni kutenda yale yanayotakiwa kutendwa ili kuleta utangamano Tanzania. "Matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno".

Ni mimi
Abu Musa Tamimu,
Dar es Salaam. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook