BINADAMU kama alivyo, anayaamini mno yale anayoyaona kuliko yasiyoonekana. Hali hii hupelekea yeye kujiamini na kuamua kutumia akili yake tu katika mazingira yake yote, bila kuzingatia mahali alipo na mahali anapokwenda. Kuwepo kwa Mwenyezi Mungu, kuja kwa Mitume na Mtume wetu (s.a.w.) akawa ndiyo kikomo cha Mitume wote, kuwepo kwa pepo na kuwepo kwa moto baada ya maisha yetu hapa duniani ni mambo kwake asiyoyataka kuyasikia na kuyapa uzito wowote. Katika maeneo mbalimbali ya maisha huu ni uasi.
Adam ni binadamu wa kwanza kuumbwa na alikuwa Mtume. Lakini alihalifu amri ya Mwenyezi Mungu. Je, Mwenyezi Mungu alifanya nini juu ya hili? Mwenyezi Mungu alichukua hatua kama alivyotufahamisha katika Qur'an tukufu sura ya ng'ombe aya 38 na aya 39 kama hivi ifuatavyo:
"Tukasema: Shukeni humo nyote na kama ukikufikieni uwongozi utokao kwangu, basi watakaofuata uwongozi wangu huo hakutakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika".
"Lakini wenye kukufuru na kuyakadhibisha maneno yetu hao ndio watakaokuwa watu wa motoni, humo watakaa milele".
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu anatutakia mema wanadamu anaendelea kutufahamisha katika sura ya tatu aya ya tatu na nne:
"Amekuteremshia kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake . Na aliteremsha Taurati na Injili".
"Zamani - ziwe uwongozi kwa watu. Na akateremsha vitabu vingine vya kupambanua baina ya haki na batili. Hakika wale waliozikufuru aya za Mwenyezi Mungu watakuwa na adhabu kali, na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu (na) mwenye kulipa".
Binaadamu amekwishapata upambanuzi wa haki na batili. Lakini mara nyingi huwa anapuuza ya Mungu na kufuata matamanio yake. Kwa kufuata matamanio yake huwa anapotosha binaadamu wenzi wake. Kwa mfano baadhi ya binadamu katika nafasi ya uongozi wa nchi wameandika nadharia zao na miongozo yao wakiwa na malengo makuu kuwa watampiku Mwenyezi Mungu na kufaulu.
Nadharia zao na miongozo yao haikufaulu bali imesababisha matatizo mengi hapa duniani. Miongoni mwa matatizo ni kuongezeka kwa maradhi, njaa, uduni wa maisha na kuchanganya batili na haki na kuvifanya sawasawa.
Hakuna raha duniani tena, malipo ya moto tunayaonja kabla ya siku hiyo maalum mbele ya mahakama ya Mwenyezi Mungu. Pamoja na taabu zote hizi, binaadamu bado hajakubali kama nadharia zake zimeshindwa kumfaa binadamu, bali anatafuta mbinu mpya kuzidumisha. Hana anathubutu kutumia nguvu kuhakikisha anayoyataka yanaendelea kuwepo na yule anaendeleza mwongozi wa Mwenyezi Mungu anapigwa vita na hata maisha yake yanaweza kuwekwa hatarini. Haya yote ni upuuzi mtupu.
Ipo sababu ya msingi inayonilazimisha kusema na kuamini kuwa ni upuuzi mtupu, kwani Mwenyezi Mungu amebainisha binaadamu katika mafungu mawili, katika maisha yetu ya kila siku.
Waumini wana sifa za pekee ambazo binadamu walio katika hasara hawawezi kuwa nazo wala kuzipata. Wana imani isiyoyumba juu ya Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Mtume (s.a.w.). Wana matendo mazuri yanayolingana na imani yao na yenye manufaa kwa binaadamu wenzao. Wana subira katika mambo yao na wana nguvu na mipango mizuri kwa upande wao.
Hawaridhiki na haya tu. Huwa ni marafiki sana na elimu inayomfaa mwanadamu katika mazingira yake na kesho akhera. Mtume (s.a.w.) amesema ili usiangamie inakubidi uwe katika mafungu manne, na ukiwa katika fungu la tano umeangamia. Mafungu manne yanatajwa kama hivi ifuatavyo: Au mwenye kujua, au mwenye kutafuta kujua, au mwenye kusikiliza, au mwenye kupenda.
Siku moja Mtume (s.a.w.) aliingia Msikitini ambapo aliwakuta watu katika mafungu mawili. Fungu la kwanza lilikuwa linasali na fungu lingine lilikuwa linasoma. Mtume akajiunga na wasomaji. Hii inadhihirisha kuwa elimu ni chombo muhimu sana kwa waumini.
Jukumu kubwa la waumini siku zote ni kuuufahamisha Uislamu kwa binadamu. Ili hili lifanikiwe ni lazima waumini wawe na Istiqama. Mafundisho ya Istiqama yanapatikana katika kitabu cha Riyadh Swaliyn kilichoandikwa na Imam Nawawi (r.a.) katika mlango wa utekelezaji. Je, Istiqama ni kitu gani? Istiqama ni utekelezaji juu ya sharia zote za Uislamu.
Mtume aliulizwa atoe kauli juu ya Uislamu ni kitu gani. Akajibu: Uislamu ni kumwamini Mwenyezi Mungu na kuusimamisha. Maneno matupu yasiyekuwa na matendo hayana nafasi katika Uislamu. Kusimamisha Uislamu siyo kuchukua panga na kulitumia dhidi ya asiyokuwa Muislamu bali ni safari ndefu yenye mambo mengi ya kufanya. Kwa mfano Sayyidna Umar (r.a.) amesema: Uislamu ni jamii.
Ebu tuiangalie jamii. Jamii yetu ina mahitaji mengi, mahitaji ya mwili na ya kiroho. Bila kuwepo hatua za makusudi zikisaidiana na uwongozi thabiti, basi jamii haiwezi kutimizwa hayo mahitaji. Wala si kweli jamii inaweza kutoshelezwa na serikali. Imenilazimu kusema hivyo kwani serikali nyingi siku hizi zimejiweka baidi na watu, iwe mijini na vijijini. Huu sasa ni wakati muafaka wa kuunda vyama vya hiari kwa ajili ya maendeleo mbalimbali na tuepuke na fikra ya kutegemea vyama vya hiari vinavyopokea maelekezo kutoka nje.
Hatuwezi kwenda mbele katika mambo ya maendeleo kama sisi siyo wa kweli katika maneno na matendo. Mwenyezi Mungu anatusuta au kutuuliza: Je, mnasema msiyoweza kuyatenda? Jaribu kumwepuka yule anayesema sana kuliko kutenda kwa sababu hana ridhaa na Mwenyezi Mungu.
Hatuwezi kuingia peponi kwa maneno tu. Kwa mfano, wengi wetu wamelielewa vibaya tamko "Laa ila haila llaa". Wengi wanaamini tamko hili ni tiketi ya kuingia peponi. Tamko hili ni sahihi kama tukiwa tayari kusimamisha sheria ya Mwenyezi Mungu na wala siyo vinginevyo.
Hili jambo ni zito na linatutaka tuambizane haki na wakati huo huo tuwe na subira. Subira haina maana ya kubweteka, bali ni kuchambua haraka hali halisi ya wasiwasi na kumshinda adui. Hili tukiliacha, basi inatosha kusema binadamu wote ni wenye hasara.
|
|