BARUA
 
Mlinda amani anapoitwa mchochezi!

Ndugu Mhariri

NI jambo la kushangaza sana kwa mlinda amani anapodokezwa kwamba kuna hali ambayo si nzuri inaweza kutokea baadaye kwa sababu hizi na hizi baada ya kumshukuru mtoa taarifa hizo, unamkamata kwa matisho na majigambo.

Hivi sio serikali yetu inayojigamba ni ya uwazi na ukweli? Itakuwaje ikipewa ukweli kwamba Waislamu wamechukia kudhulumiwa na kukandamizwa kwa kuwa wao ni Waislamu, serikali ya ukweli iukatae ukweli huo.

Mhe. Rais alishaambiwa ukweli huo na ni alama kwamba Waislamu hawaridhiki na nchi jinsi inavyoongozwa tangu tupate uhuru. Viongozi wa serikali ni Binadamu na binadamu hawezi kukamilika ndio maana wakakumbushwa.

Mhe. Rais aliwaomba wananchi tumsaidie kuwafichua wala rushwa na kutolewa taarifa za dhulma zinazofanyiwa wananchi. Hivyo rushwa na dhulma inaweza ikafanywa na mwananchi wa kawaida, kiongozi, mtawala. Itakuwaje akisaidia Mhe. Rais kuwa chanzo cha mmomonyoko Tanzania ni baadhi ya wananchi kubaguliwa kwa misingi ya dini yao na kudhulumiwa iwe ni kosa la jinai.

Amesema kweli Allah (s.w.) kuwa dhulma haidumu. Na huu msemo ni wa kuzingatia sana. Sikubaliani na kauli ya Kadinali Pengo kwamba kuna watu wanaotumiwa na nchi za nje ili kuvuruga amani.

Huo si ukweli na sikutegemea kiongozi kama huyo angelifikia kusema maneno kama hayo na ukweli wanaufahamu bila haki hakuna amani. Vitisho, kebehi havitaisaidia jamii.

Mwisho, serikali imuachie Sheikh Juma Mbukuzi. Maneno aliyoyasema siyo yake ni ya Waislamu wa Tanzania na wakina Mbukuzi wapo wengi wenye uchungu na dini yao.

Kuendelea kukamata kamata viongozi wa dini pia linaathari kubwa katika nyoyo za binadamu wapenda haki. Rafiki akupendae ni yule anaekuleza matatizo yako na jinsi ya kuyaondoa. Mnafiki hukusifu na kukupaka mafuta kwa mgongo wa chupa.

Nina imani serikali itazingatia maoni ya wananchi. Narudia binadamu hakamiliki anahitaji kwa wengine msaada hata wa maoni.

S. Hamid,
Moshi.

Hii ni propaganda

Ndugu Mhariri

NAOMBA nafasi nitoe mawazo yangu kupitia gazeti la AN-NUUR.

Baada ya Waislamu wa Jijini na wa mikoani kutangaza azma yao ya kuandamana ili kupinga hatua ya serikali kumuweka ndani Sheikh Juma Mbukuzi, baadhi ya mitaa ya Jijini yalibandikwa matangazo yaliyodakwa na baadhi ya vyombo vya habari yakitangaza Fat'wa iliyodaiwa kuwa imetolewa na Waislamu kuwaua viongozi wa Bakwata.

Hii ni moja ya mbinu ya madhalimu kuwachanganya watu na kuwaandalia mazingira ya kuonekana wabaya katika jamii nzima.

Pili, matangazo haya yametolewa baada ya Waislamu kutoa matangazo yao ya kuandamana kama haki yao kikatiba siku ya leo, ili iwe ni sababu ya kuharibu maandamano hayo.

Tunawaomba waandaaji wa propaganda hizi wajue kuwa Waislamu wa leo sio wa jana.

Munawar Mussa,
Morogoro.

Wafungwa Waislamu tupewe fursa ya kuswali

Ndugu Mhariri

SISI Waislamu wa gereza la mahabusu Morogoro kwanza tunatoa kilio chetu kwa uongozi wa Kitaifa Magereza Tanzania.

Kutokana na kupigwa marufuku kufanya ibada kila siku kama maamrisho yanavyosema na kupangiwa kufanya ibada Ijumaa tu.

Ukiangalia sababu ambazo zimefanya mkuu wa gereza mahabusu kutoa amri hiyo hazina msingi wowote hasa ukiangalia jela zote hapa Tanzania kuna Waislamu na Wakristo na Wapagani. Zipo taratibu ambazo zimewekwa kupewa selo yaani bweni la kulala ambalo huwa kwa waumini iwe Mkristo atakuwa na bweni lao na Waislamu hivyo hivyo.

Sasa kwa sisi Waislamu kukatazwa kufanya sala tano halafu kuambiwa eti Ijumaa ndio tuswali hicho tumekataa.

Maana hatuoni sababu za kulazimishwa kufanya ibda Ijumaa tu.

Ni makosa gani sisi Waislamu tumeyafanya mpaka atuzuie kusali?

Sisi Wafungwa,
Gereza la Mahabusu,
Morogoro.

Sheikh Mbukuzi hana hatia

Ndugu Mhariri

KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 18 inatamka: Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na mawazo yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati".

Ibara ya 20 inaendelea kutamka: "Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo".

Ni hivi karibuni, Sheikh Juma Mbukuzi, ambaye ni Amir wa Shura y Maimamu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alikutana na waandishi wa habari na kutoa taarifa rasmi juu ya dhulma wanayofanyiwa Waislamu ndani ya jamii ya Watanzania.

Shura ya Maimamu imeithibitishia serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania iko tayari kusaidia kuonesha matatizo ya Waislamu, ili kuepusha vurugu inayoweza kutokea kama matatizo hayo yakifichwa fichwa. Pia taarifa yao rasmi ni kumbukumbu ya kudumu kuwa viongozi wa Waislamu wanatumia na wataendelea kutumia Katiba ya nchi juu ya uhuru wa kutoa mawazo.

Ni jambo lenye kutia machozi kuona kwamba taarifa hiyo haikuzingatiwa. Badala yake kumkamata Amir, Sheikh Juma Mbukuzi na kumfungulia mashitaka kortini ati mashitaka ya uchochezi. Kumkata Amir na kumfungulia mashitaka ni sawa na kusema kuwa polisi wamekiuka Katiba ya nchi, ambayo inatoa uhuru wa mawazo - uhuru ambao Amir aliutumia na ambao ataendelea kuutumia siku za usoni kwa faida ya watu wote wanaopenda amani. Kamata, tia ndani na fungua mashitaka ni nyenzo isiyofaa haswa kwa wakati wetu huu wa uwazi na ukweli.

Huu ni wakati muafaka wa kuiweka juu Katiba ya nchi kuliko kitu chochote. Bila ya kuiheshimu Katiba hii kitakachofanyika ni ukandamizaji kwa raia wasiyo na hatia. Sheikh Juma Mbukuzi ni raia mwema na hana hatia, bali ni raia anayeamini katika misingi ifuatavyo:

Anapoona baya katika jamii, anazuia kwa mkono wake. Anapoona baya katika jamii, anasema dhidi ya baya hilo. Kama la kwanza na la pili ni gumu kwake, basi anachukia lakini huu ni udhaifu mkubwa.

Polisi wafute mashitaka dhidi yake, kwani mashitaka hayo hayana nguvu dhidi ya Katiba ya nchi, rejea Ibara ya 18 na ya 19. Kifungu cha sheria kinachokwenda kinyume na Katiba hakina budi kufutiliwa kwa mbali.

Abubakari S. Marwillo,
Dar es Salaam.

Nani ataongoza sala ya maombi

Ndugu Mhariri

KATIKA siku za hivi karibuni, wahamasishaji mbalimbali wenye nyadhifa na jinsia tofauti ndani ya jamii yetu wanachagiza/wanahamasisha haja ya kusahau kinachoitwa tofauti za imani za kidini, kikabila na hata hali za maisha ili kwa pamoja Watanzania waungane kufanya maombi kwa ajili ya Mwalimu Nyerere ili apate afya njema.

Hilo ni wazo jema, hasa tukizingatia ukweli kuwa Mwenyezi Mungu Muumba ndiye mwenye nguvu juu ya vyote.

Hata hivyo, ninawatanabaisha wahamasishaji wa wazo hilo kuwa, ni lazima kuikubali hali halisi kwamba wakati waumini Wakristo wana hakika ya kuwa pamoja na viongozi wao katika hayo "maombi" Waislamu walio wengi waadilifu watabakia viwanja vya mahakama za Kisutu kumsubiri Amir wao kiongozi Sheikh Juma Mbukuzi na wengine watakuwa wakiisubiri mamlaka ieleze kwa nini inamsaka Sheikh Ponda Issa Ponda.

Kitukuu wa Mwajuwa,
Dar es Salaam.

Ufumbuzi si kamatakamata

Ndugu Mhariri

Ni muda mrefu sasa Waislamu wamekuwa wakilalamika kuwa wanadhulumiwa na serikali iliopo madarakani, dhulma wanazodai ni pamoja na kubanwa katika kutekeleza ibada zao mbalimbali.

Serikali imekuwa inawaingilia mara kwa mara. Waislamu wameshuhudia serikali ikisimama upande wa dini nyingine pindi wawapo mahakamani.

Vile vile mambo ya kijamii bado ufugaji na uenezaji wa nguruwe katika maeneo ya watu mchanganyiko unafanyika holela pote nchini pasina kuzingatia sheria za miji na sheria za ufugaji.

Uuuzwaji wa pombe holela na ufunguaji wa maduka ya kawaida ya kuuzia unazidi kuenea, mpaka maeneo yanayouza vyakula, mahospitalini wagonjwa hawapumziki kutokana na kelele za walevi. Mitaani hali ndio inatisha.

Waislamu wamelalamika muda mrefu na wameomba mara kwa mara kutaka kukutana na viongozi wa serikali kuielezea hali hii, bila mafanikio, lakini malalamiko yao yapo katika ofisi zote za watawala wa nchi hii akiwemo Mhe. Rais wa nchi.

Kinatuuma zaidi Waislamu ni kule kupuuzwa madai yetu na kuonekana hayana msingi, wakati Paroko Lwambano wa Mburahati alipoitisha serikali juu ya mihadhara aliyoiita ya kashfa, serikali ilitekeleza vile alivyotaka na hatimaye Waislamu wameuawa pale Mwembechai na mpaka leo pamoja na Waislamu kudai iundwe Tume huru kuchunguza hili tukio bado wanapuuzwa.

Mwanafunzi Chuki Athumani alipigwa risasi na kupata kilema cha maisha kwa madai aliyoyaeleza Waziri wa Mambo ya Ndani eti alikuwa na makaratasi ya uchochezi. Risasi kapigwa, masomo amepoteza na mpaka sasa hajapelekwa kutibiwa nje ya nchi.

Huyu mwanafunzi ni taifa la kesho, asiyetibika hapa nchini. Pamoja na kukaa hatiani zaidi ya miezi minne.

Waislamu wanapoamua kuandamana kwa amani, wanazuiwa na kupigwa pasina sababu yoyote ya kisheria na viongozi wa polisi wanadai eti kutatokea fujo kwenye maandamano. Lakini bora ubabe huo ungewahusu na Wakristo.

Katiba iko wazi, maandamano ni haki ya kikatiba, watu wapate kujielezea na kutoa dukuduku lao, ina maana viongozi wa polisi katiba ya nchi hawaijui?

Ufumbuzi wa matatizo si kuwakamata wale wanaoishauri serikali kuchukua tahadhari au si kuzuia maandamano ya kuonesha hisia zetu za kuonewa au kudhulumiwa. Tendo la kuwaita washauri wema ni wachochezi au wakorofi au wanaotumiwa ni la hatari.

Dawa Ni kuyapokea madai yao, tusije kupoteza gharama kubwa kwa vikao vya usuluhishi baadaye.

Ummu Hamza,
P.O. Box 2318,
Tanga.

Tanga

--
Juu RUDI

Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook