KUTOKA MAGAZETI YA ZAMANI
 
 

Mpango wa kuipatia Dodoma maendeleo ya haraka

SERIKALI inatayarisha mpango maalum ambao utauwezesha mkoa wa Dodoma kuwa na maendeleo ya haraka, Waziri wa Mambo ya Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Bwana Paul Bomani aliliambia Bunge jana.

Bwana Bomani ambaye alikuwa akitoa hotuba ya kujibu hotuba za baadhi ya Wabunge walizozitoa kuhusiana na Mpango wa Maendeleo katika mwaka 1970/71 ambao ulitolewa mbele ya Bunge kabla ya makadirio ya matumizi ya serikali hayajatolewa, alisema kwamba serikali haijawahi kutosheka na maendeleo ya mkoa wa Dodoma.

Waziri alikubaliana na baadhi ya Wabunge kwamba wananchi wa Dodoma wanatekeleza vyema mpango wa sasa wa maendeleo ijapokuwa mpango huo bado utaubakiza mkoa huo nyuma ya mikoa mingine ambayo inapambana na matatizo kidogo.

Bwana Bomani alisisitiza kuwa tatizo la maji litakabiliwa kwanza kabla ya matatizo mengineyo. Akaonya "Ijapokuwa tunapenda Dodoma iendelee, lazima mtambue kwamba ni lazima utengenezwe mpango amabo hautazuia kufanyika mipango mingine iliyokwisha kusudiwa kufanywa katika mpango wa maendeleo ya miaka mitano.

Kuhusu mashauri ya Wabunge ya kutaka zijengwe barabara ya viwanda vingi zaidi, Bwana Bomani alisema kwamba jambo hilo si ombi jipya, kila mbunge anapenda zijengwe barabara na viwanda vingi sehemu yake. "Ni vigumu kufanya hivyo kwa wakati mmoja, lakini napenda kuwahakikishieni kwamba serikali inaelewa matatizo haya na yatatatuliwa", alisema Bwana Bomani.

Bwana Bomani alizidi kuwaambia Wabunge kwamba serikali imenzisha utaratibu mpya katika kutekeleza mpango wa maendeleo nao ni kuuchunguza kila baada ya wakati.

Alisema utaratibu huu utaiwezesha serikali kufahamu ni jambo gani linalotakiwa kufanyika katika miaka miwili ya kwanza ya mpango huo.

Bwana Bomani kisha aliwasifu wananchi wa Mtwara kwa juhudi zao za kuanzisha vijiji vya ujamaa. "Juhudi zao zinaipa moyo serikali na Watanzania kwa ujumla. Wananchi wa Mtwara wameonyesha mfano mzuri ambao wenzao katika mikoa mingine hawana budi kuiga", alisema.

Aliwakumbusha Wabunge juu ya uamuzi wa Kamati Kuu ya TANU wa kuchunguza maendeleo ya uchumi wa vijiji vya ujamaa kabla ya kuanzisha mpango wowote wa uchumi. "Jambo hili ni lazima kwa sababu badala ya kuwaletea uchumi wanavijiji wanaweza kutumbukizwa katika hali ya umaskini", alionya.

Juu ya ujenzi wa barabara ya Lindi/Kibiti, Bwana Bomani alilihakikishia Bunge kwamba barabara hiyo imo katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano na itajengwa katika muda huo. Alisema kwamba upimaji umeshanyika.

Bwana Bomani aliliambia Bunge kwamba wakati wa ziara yake katika Japan, alifanya mazungumzo na wataalamu wa serikali ambao aliahidi kuwatuma wataalamu zaidi kuja kushughulikia mpango huo.

Akijibu usemi wa baadhi ya Wabunge kwamba barabara hiyo haitajengwa kwa vile serikali inasubiri kupata mkopo kutoka katika Benki ya Dunia, Bwana Bomani alisema kwamba mkopo huo ni lazima ili kuwezesha mipango mingine itekelezwe.

Juu ya shauri la kutaka kiwanda cha mbolea kijengwe Tanga badala ya Dodoma, Bwana Bomani alisema kuwa Tanga imependekezwa kwa sababu ya nafuu ya kuwasili nyenzo kutoka Ulaya kwa urahisi kwa njia ya bahari. Pia alisema kuwa kiwanda cha saruji kilichopangwa kujengwa Mbeya kitajengwa kama ilivyokusudiwa.


Tusitishwe na binadamu, Nyerere
 

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa pili wa Chama Cha Mapinduzi mwezi jana walimchagua Mwalimu Julius K. Nyerere kwa wingi wa kura ili aendelee na wadhifa wake wa kuwa Mwenyekiti wa CCM katika kipindi kingine cha miaka mitano ijayo.

Mwalimu Nyerere alipata kura 1726 kati ya 1737 za wajumbe waliohudhuria mkutano huo na kuwa zilipigwa kwa siri kwa mara ya kwanza. Kura tisa zilipinga na ni kura mbili tu ziliharibika.

Katika uchaguzi huo huo Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi alichaguliwa kuwa Makamu wa Mwenyekiti wa Chama kwa wingi wa kura 1715 zilizomkubali na kura kumi na tisa zilikataa, Kura tatu ziliharibika.

Mkutano huo wa kawaida ulioanza tarehe 20 Oktoba, mwaka huu na kumalizika tarehe thelathini uliwachagua wajumbe mbalimbali wa kushika wadhifa wa Chama Cha Mapinduzi kitaifa. Baada ya kutangazwa Mwenyekiti mpya Mwalimu Nyerere aliwashukuru wote waliofanikisha mkutano huu.

Katika hotuba yake Mwalimu aliwataka wajumbe na Watanzania kwa jumla kuwa na msimamo ule ule wa kujenga Ujamaa hapa nchini, na wasibabaike wala kukubali kuvurugwa na mahasidi wa siasa na umoja wetu tulio nao. Mwalimu alisisitiza Mwenyezi Mungu ndiye mwenye uwezo juu ya viumbe wote wala sio mtu mwingine kututisha.



Ujamaa uchungwe Tanganyika

UJAMAA ni lazima uchungwe nchini Tanganyika. Hivyo alivyosema Regional Kamishna wa Mkoa wa Tanga Mheshimiwa Jumanne Abdallah wakati alipofungua kiwanda kipya cha wazalendo cha kuvunja mawe huko Kange Tanga.

Kiwanda hicho ni cha Mabwana Salehe Kibwana na O.B.E. Makatta Mwinyimtwana, Omari Sebo, Saidi Kitwana, Mzee Sababu na Mzira Ahmedi.

Ponda mali

Wazalendo hawa wote waliwahi kufanya kazi katika idara ya posta na sasa wamepumzika wakila pensheni zao. Hawakutosheka, wakaona kuwa haifai kukaa kimya wakitambua starehe za ponda mali kufa kwaja. Wakajiunga wakaanzisha ushirika wao.

Wakamwendea Kampuni ya Bird & Co. ili kuwapatia sehemu fulani katika shamba lake, akawapa sehemu fulani. Wazalendo hao wakachanga fedha, wakafungua kiwanda chao.

Mkopo

Kama serikali inavyoahidi kuwasaidia wowote wanaojiunga ili kuendeleza nchi, ikatoa mkopo wa shilingi 20 elfu. Ndipo jamaa wakajenga kiwanda cha kuvunjia mawe, kutengeneza matofali ya mchanga yaliyochanganywa na simenti.

Kampuni yao inaitwa Tanga African Quarry Company. Kiwanda kilipokamilika, wakamwita Mheshimiwa Bwana Jumanne Abdallah akifungue. Juzi Jumamosi tarehe 15 akachukua mkasi kukata uzi wa kuonyesha kuwa kinafanya kazi.

Wajiunge

Mashine ikatiwa moto, mawe yakaanza kusagwa. Mheshimiwa Mjumbe wa Baraza la Taifa, Bwana Lemaitre akatoa oda ya kwanza ya kutaka lori moja la kokoto.

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook