AWALI ya yote, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Mhariri wa AN-NUUR, nawapa pole wasomaji wangu kwa usumbufu walioupata kwa kuikosa makala ya chakula na lishe kwa wiki mbili (toleo Na. 219 na 220).
Katika nchi zilizopiga hatua kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia, na zile zenye serikali makini kuhusu mambo ya usafi na afya kwa ujumla, si rahisi kukuta vinyesi kwenye vyakula na maji ya kunywa.
Hata hivyo, katika nchi zenye maendeleo duni katika sayansi na teknolojia, na zile zenye serikali zilizoshindwa kusimamia usafi na mambo mengine ya afya kwa ujumla, ni jambo la kawaida kukuta vinyesi katika vyakula na maji ya kunywa.
Kinyesi kinachotoka kwa binadamu au mnyama mgonjwa huwa kina vijidudu vinavyosababisha maradhi. Mfano wa vijidudu hivyo na maradhi vinavyosababisha kwenye mabano ni Salmonella typhi (homa ya matumbo), Vibrio Cholerae (Kipindupindu), Shigella (kuhara damu), Entamoeba histolytica (kuhara damu).
Chakula kinaweza kuchafuliwa na kinyesi kama watu hawatanawa mikono vizuri mara baada ya kutoka chooni (choo kikubwa), na wakakishika chakula hicho. Pia inzi ni chanzo kingine cha uchafuzi wa chakula.
Kwa upande wa maji ya kunywa, yanaweza kuchafuliwa na kinyesi kama chanzo cha maji hayo kiko karibu na choo (cha shimo) au mfereji wa maji machafu. Maji ya bomba pia yanaweza kuchafuliwa na kinyesi kama bomba limepasuka na nguvu ya maji (pressure) ni ndogo, na wakati huo huo bomba hilo liko karibu na choo au limekutana na mfereji wa maji machafu.
Tukiizingatia hali ya Tanzania na mlipuko wa magonjwa (kipindupindu, kuhara, kuhara damu na homa ya matumbo) unaotokea mara kwa mara, ni wazi kuwa maji na vyakula vyetu vinachafuliwa na vinyesi. Kwa hiyo, mambo yafuatayo hayana budi kutekelezwa kikamilifu.
Kwanza, serikali kuu na zile za mitaa na vijiji ni vyema kama watalivalia njuga suala la usafi na afya kwa ujumla. Uchafu uliozagaa hasa katika jiji la Dar es Salaam, Manispaa na miji mbalimbali ni aibu kwa Taifa na ni hatari kwa afya zetu.
Pili, wananchi wahakikishe kuwa mazingira yao yanakuwa safi na vyoo viwe mbali na vyanzo vya maji.
Tatu, maji ya kunywa lazima yachemshwe, hata kama yamepatikana bombani.
Nne, serikali ijitahidi kutia dawa maji yanayotumika kwa ajili ya kunywa na yale ya viwandani (viwanda vya vyakula).
Tano, wananchi lazima wapike vyakula vyao vizuri, na viliwe vyakula hivyo hali ya kuwa ni vya moto. Mwiko kula kiporo bila ya kukipasha moto.
Pia matunda na mboga mboga zinazoliwa bila ya kupikwa, lazima zioshwe vizuri tena kwa kutumia maji yaliyochemshwa. Jambo hili ni zito kwa baadhi ya wananchi, lakini wakumbuke gharama na hatari ya maradhi ni kubwa kuliko uzito wa kufanya haya tunayoyashauri.
Vile vile, maziwa (mabichi) lazima yachemshwe kabla ya kunywewa.
Sita, vyombo vinavyotumika kwa ajili ya vyakula, lazima vioshwe vizuri na vikaushwe kabla ya kuvihifadhi.
Saba, mazingira ya kuandaa chakula (jiko) na mahali pa kulia lazima pawe safi.
Nane, serikali isimamie kikamilifu viwanda vya vyakula na maji (Mineral water). Pia iwaelimishe na kuwasimamia mama ntilie, wenye hoteli, migahawa, maduka, bucha na kadhalika.
|
|