Mshitakiwa anaweza kukata rufani dhidi ya amri ya kulipa fidia iliyotolewa na mahakama katika shauri la jinai (F. 348(3), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Mbali ya mlalamikaji, fidia inaweza kutolewa hata kwa mshitakiwa ambaye hakuonekana na hatia iwapo mahakama yanaona mashitaka dhidi yake yalikuwa hayana msingi (F. 347, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Fidia hiyo ni kwa usumbufu na hasara iliyopatikana.
Hata hivyo ni nadra sana mshitakiwa kulipwa fidia kwa mujibu wa fungu hili la sheria.
Amri nyingine
Mbali na adhabu mbalimbali zilizoelezwa kwa kifupi juu ya mahakama pia yanaweza kutoa amri nyingine nyingi dhidi ya mhalifu kufuatana na mazingira ya kosa lenyewe. Mathalan yanaweza kuamuru mali inayohusika na kosa lenyewe irejeshwe kwa mwenyewe kama yupo (F. 357(a), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h..j). au ishughulikiwe kama mali isiyo na mwenyewe.
Katika makosa mengine kama ya usalama barabarani, mahakama yanaweza kumnyang'anya mshitakiwa leseni ya udereva (Sheria ya Usalama Barabarani, Na. 30, 1973)
Amri nyingine muhimu sana ni kuachiwa kwa masharti au bila ya masharti (F. 38, Kanuni ya Adhabu, i.h.j) . Amri hii ni maarufu kwa jina la kifungo baridi. Yaani iwapo kutokana na mazingira ya shauri lenyewe kama vile uzito wa kosa au tabia ya mhalifu, mahakama yataona sio vyema kutoa adhabu, basi yanaweza kumwachia mhalifu bila ya masharti. Au yanaweza kumwachia kwa masharti kama vile asitende kosa jingine katika kipindi fulani. Mahakama yanawajibika kumwelewesha mshitakiwa kuwa iwapo atavunja masharti hayo yaliyowekwa ataadhibiwa kwa kosa alilolitenda awali.
Namna ya kutoa adhabu
Mahakama yanatakiwa kutoa adhabu au amri yoyote ile inayofaa (na kuonyesha wazi katika mwenendo wa shauri) kwa kila kosa ambalo mshitakiwa ametiwa hatiani (Meyerowitz (1947) 14 E.A.C.A. 130). Kama makosa ni matano basi kila kosa litakuwa na adhabu yake. Mahakama yataamua jinsi ya kutumikia adhabu hizo. Mshitakiwa anaweza akatakiwa kutumikia kila adhabu pekee (F. 168(2), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Kwa mfano ikiwa amepatikana na hatia ya makosa mawili mbalimbali na kuhukumiwa kifungo, basi ataanza kutumikia kifungo cha kosa la kwanza, halafu ndipo ataendelea kutumikia kifungo cha kosa la pili. Lakini kwa vyovyote vile idadi ya miaka ya kutumikia kifungo haitazidi kumi (F. 168(3), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Njia ya pili, ambayo ndiyo hutumika zaidi, ni kuzitumikia adhabu za makosa yote kwa pamoja (F. 168(2), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).Mshitakiwa atatumikia ile adhabu kubwa kupita nyingine (F. 168(5), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Hivyo hata kama makosa ni arobaini, pengine yote ya wizi na yametolewa adhabu ya kifungo, mshitakiwa atatumikia kifungo kile kikubwa kupita vifungo vingine katika makosa hayo. Mahakama hutumia njia hii zaidi wakati makosa yanayohusika yametendeka wakati mmoja (Sawedi Mukasa v. R. (1946) 1 E.A.C.A. 97). Kwa mfano makosa kama vile wizi (F.265, Kanuni ya Adhabu, i.h.j) na kughushi maandishi (F.337, Kanuni ya Adhabu i.h.j) yanaweza kutendeka kwa kutumia hundi moja, wakati na siku moja tu.
Mahakama yanao uwezo wa kuchanganya aina za adhabu, kama vile kifungo na viboko au na faini. Lakini Hakimu wa Wilaya ambaye siye Mwandamizi hawezi kuchanganya adhabu ya viboko na aina nyingine mpaka ithibitishwe na Mahakama Kuu (F.167, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Pamoja na yote hayo ikumbukwe kuwa kila shauri linaamuliwa kulingana na mazingira yake. Adhabu, halikadhalika, hutolewa kufuatana na mazingira ya shauri lenyewe.
Kuitumikia adhabu
Kwa kawaida adhabu ya kifungo huanza kutumikiwa mara baada ya kutolewa (F. 327, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j) isipokuwa ikiwa mshitakiwa ataomba na kupewa dhamana kabla ya kusikilizwa rufani yake (F. 368, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Adhabu pia inaweza isitumike kwa masharti kuwa mshitakiwa hatatenda makosa katika kipindi kisichozidi miaka mitatu (F. 326(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Iwapo ni adhabu ya faini pekee italipwa katika kipindi ambacho mfungwa anaweza kukata rufani kupinga adhabu hiyo. Na iwapo adhabu mbili, kifungo au faini zimetolewa, mahakama yanaweza kumpa dhamana mshitakiwa, kwa masharti au bila masharti, alipe faini hiyo katika muda wa siku kumi na tano (F.330(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Mwisho wa muda huo mahakama yataamua mshitakiwa aanze kukitumikia kifungo kama atashindwa kuilipa (K.h.j). Lakini bado muda wa kulipa faini hiyo unaweza kuongezwa tena kwa sababu za kutosha (K.h.j).
Utaratibu ulioelezwa hapo juu unahusiana, kwa kiwango kikubwa, na jinsi ya kuzitumikia adhabu nyingine isipokuwa kifo.
Kwa vile adhabu ya kifo ni nzito mno utaratibu wake ni mrefu vile vile. Kwanza, kwa kawaida mashauri yote ambayo kwayo mshitakiwa amehukumiwa kifo, hupelekwa Mahakama ya Rufani kubishaniwa tena, na pili hata pale rufani ya mshitakiwa inapokataliwa, bado adhabu ya kifo haiwezi kutekelezwa mpaka Rais wa Jamhuri ameidhinisha adhabu hiyo (F. 325, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Mambo ya kutiliwa maanani katika utoaji wa adhabu
Baadhi ya waandishi wa vitabu (Brown, D. Criminal Procedure in Uganda and Kenya, Toleo la Pili, London, 1970, uk. 126-130) wameorodhesha mambo ambayo hutiliwa maanani wakati wa utoaji adhabu. Baadhi yake ni chanzo cha kosa lenyewe, uzito wake, tabia ya mkosaji kabla ya kosa na wakati wa mashitaka, makosa ya zamani, wingi wa kosa lenyewe, usalama wa jamii, hali ya familia ya mkosaji na kadhalika.
Hakika yote hayo ni mambo
yanayostahili kuzingatiwa wakati wa utoaji adhabu lakini pengine chanzo
cha kosa lenyewe ndiyo suala kubwa kupita yote. Kwa nini magereza yamejaa
zaidi watu wa kipato cha chini? Wafungwa wengi hutenda makosa kinyume na
ridhaa yao bali kwa msukumo wa mazingira magumu. Suala hili ni la maana
sana kutiliwa maanani katika makosa ya wizi, ambayo ndiyo mengi sana kuliko
yoyote. Kwa maana hii basi Sheria ya Viwango vya Chini vya Adhabu (Sheria
Na. 1, 1972) hailiangalii suala la adhabu katika mtazamo sahihi hususan
kwa sababu kadhaa. Mosi inalirahisisha tatizo la uhalifu, hasa wa mali
ya umma, kuweza kutatuliwa kwa njia ya vifungo virefu. Hii sio sahihi.
Pili inaweka ubaguzi mkubwa wa utoaji adhabu kwa vile karani wa serikali
au shirika la umma atafungwa miaka mitano na kuendelea kwa wizi wa shilingi
mia na hamsini tu wakati ambapo wa laki moja, mali ya raia, anaweza kufungwa
miezi miezi michache tu. Tatu, basi sheria hii inaelekea kudharau usalama
wa raia binafsi na mali yao, jambo ambalo ni muhimu mno kwa vile taifa
ni watu. Sheria imeingilia mno kauli adhimu ya uendeshaji wa mashauri kwamba
kila shauri liamuliwe kutokana na mazingira yake. Mahakama yanaweza kubainisha
kosa zito na mazingira ambayo adhabu kali inastahili bila ya kuyalazimisha
kupitisha adhabu kubwa kwa makosa ambayo kwa kweli, mengine, hayastahili
adhabu hizo. Isitoshe siku zote serikali inaweza kukata rufani kupinga
uamuzi wa mahakama ambayo yanaona yametoa adhabu ndogo kupita kiasi.
--
|
|