Waislamu waitahadharisha serikali
 

WAISLAMU mjini hapa wameitahadharisha serikali kuwa hawataendelea kuwa wavumilivu endapo viongozi wao wataendelea kukamatwa na kurundikwa magerezani.

Wakiongea na gazeti hili mapema wiki hii kwa nyakati tofauti na sehemu tofauti zikiwemo za kazi, biashara na Misikitini, Waislamu hao walisema kuwa imeshakuwa kasumba kuwakamata Masheikh ambao wanaonekana kuwa mbele kuieleza serikali madhila inayoyafanya.

Ustadh Omary Yahya Hussein muumini wa Msikiti wa Uwanja wa Ndege alisema kuwa pamoja na serikali kufahamu kuweko hali inayotishia amani ya nchi kutokana na madai ya Waislamu kwamba wanabaguliwa imeamua kukaa kimya na kuwatisha kwa kuwapiga virungu na kuwakamata ovyo.

Naye Sheikh Ngalawa Sijali wa Msikiti wa Mafiga (Manzese) alisema kuwa serikali inawatonesha vidonda hasa baada ya kukumbuka madhila yaliyowafika Waislamu kadhaa waliojitoa muhanga katika kutetea Uislamu na kuwataja marehemu Sheikh Kassim bin Juma, Mzee Chatta na Mzee Mageta wa hapa Morogoro aliyekufa baada ya kuathirika na mabomu ya FFU yaliyopigwa katika Msikiti wa Uwanja wa Ndege mwaka 1994.

Mwingine aliyetoa dukuduku lake kupitia gazeti hili ni Bi Aisha Rajab wa Msikiti wa Mafiga (B) alisema kuwa inashangaza na kuhuzunisha kuwa wale wanaotoa kauli ya kuitahadharisha serikali wanaitwa wachochezi na wavurugaji wa amani.

Ustadh Khalid Ramadhan wa Msikiti Mkuu (Boma Road) alisema kuwa viongozi wa serikali wasipokuwa makini huenda wakaitumbukiza nchi kwenye janga kubwa hasa kutokana na dhuluma wanayofanyiwa Waislamu na kuwaweka viongozi wao rumande kila kukicha.

Naye Sheikh Awadh Abdul wa Msikiti wa Kichangani aliionya serikali juu ya mbinu yake ya kuwashughulisha Waislamu na mambo ya kesi na vurugu.

"Katika hali hii inayokuja nayo serikali hata Waislamu wenye chembe ya imani watajitoa mhanga kuuhami Uislamu pamoja na viongozi wake", alisema Ustadh Awadh.

Aidha uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa Waislamu katika Misikiti kadhaa mjini hapa wamekuwa wakitafakari kwa kina suala zima la kukamatwa Amir wa Waislamu Sheikh Juma Mbukuzi huku wengine wakianza kuchangishana fedha kwa ajili ya kusaidia familia ya Sheikh huyo pamoja na kesi inayomkabili.

Sheikh Mbukuzi alikamatwa na polisi Septemba 17 kwa madai ya kutoa maneno ya uchochezi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Msikiti wa Mkwajuni, Kinondoni Jijini. Alikaa rumande karibuni wiki tatu kabla ya kuachiwa kwa dhamana Jumatano Oktoba 6, mwaka huu.


Aliyoyasema Mwinyi ni kweli - Sheikh Kassim
 

SHEIKH maarufu mkoani Kagera Kassim Maftah amekemea vikali tabia iliyojengeka kwa Waislamu ya kutofanya kazi wakitegemea kufadhiliwa na mataifa ya nje.

Sheikh Kassim aliyasema hayo baada ya mtu mmoja aliyejiita Mwenyekiti wa Waislamu Kagera kunukuliwa na vyombo vya habari kwamba Waislamu hawana ugomvi na Marekani na kwamba wana thamini na kuhitaji msaada wao.

Aidha, Sheikh Kassim alisema kwamba Waislamu wenye mawazo ya kuwa Marekani itawasaidia katika masuala ya kusimamisha dini ya Mwenyezi Mungu wajue kwamba wanakosea, kwani Marekani ni adui mkubwa wa Waislamu duniani kote.

"Aliyoyasema Rais Mstaafu ni sahihi kabisa na bahati nzuri ametoa na ushahidi kwa kunukuu maneno aliyoyatamka mmoja wa waliowahi kuwa viongozi wakubwa wa nchi ya Marekani baada ya kuanguka kwa taifa la Urusi (Ukomonisti) kwamba adui aliyebaki kwa mataifa ya Magharibi ni Uislamu", alisema Sheikh Kassim.

Hivi karibuni Rais Mstaafu wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi alipokuwa akifungua semina ya akina mama Waislamu iliyofanyika kata ya Ibwera Bukoba Vijijini, aliwataka Waislamu kuutekeleza Uislamu wao kwa matendo kama alivyoufundisha Allah (s.w.) na Mtume wake.

Aidha, Alhaj Mwinyi aliwatahadharisha Waislamu na mbinu wanazozitumia maadui wa Uislamu (Marekani) kwa kuwatoa taratibu kwenye imani yao na kuwaingiza katika imani zingine kimatendo.

"Mtu yeyote kudai haki yake si vurugu, lazima watu wapewe haki zao hata kama ni mtu mmoja", alisema Mzee Mwinyi.

Semina hiyo ambayo ilihudhuriwa na wahadhiri mbalimbali toka ndani na nje ya mkoa huo iliwahimiza Waislamu kuzilea familia zao kimaadili ikiwa ni pamoja na kuwashonea watoto wao hijab zinazofanana na sare za shule ili wavae wawapo shuleni.

Ziara ya Mzee Mwinyi hapa mkoani imetoa changamoto kubwa baada ya kutembelea wilaya mbalimbali na kuzungumza na Waislamu juu ya Uislamu wao.

Katika ziara hiyo iliyoanza Septemba 17 na kumalizika Septemba 20, mwaka huu Alhaj Mwinyi alitembelea kata ya Ibwera ambako alifungua semina ya kinamama, Msikiti wa Bwanjai ulioko kata ya Bwanjai, shule ya sekondari ya Kiislamu Kanyigo iliyoko kata ya Kanyigo pamoja na shule ya sekondari ya Ishozi iliyoko kata ya Ishozi.


London wasoma khitma ya Mtemvu
 

WATANZANIA waishio Uingereza walimsomea khitma marehemu Zuberi Mtemvu Jumamosi iliyopita Oktoba 1, 1999.

Khitma hiyo ambayo ilifanyika katika ukumbi wa shule ya Featherstone eneo la Magharibi mwa jiji la London nyakazi za alasir, iliandaliwa na Watanzania Waislamu waishio katika jiji hilo, na kuhudhuriwa na Watanzania wengi wanaoishi Uingereza.

Kisomo cha Khitma hiyo kiliongozwa na Shariff Qulatain.

Zuberi Mtemvu ambaye alikuwa miongoni mwa waasisi wa mapambano ya kudai uhuru wa Tanganyika toka ukoloni wa Kiingereza, alikuwa Katibu Mipango (Organising Secretary) wa kwanza chama cha TANU kilichoasisiwa mwaka 1954.

Mnamo mwaka 1958 Mtemvu alijiuzulu TANU akipinga uamuzi wa Chama hicho kukubali mapendekezo ya serikali ya kikoloni ya kuweka elimu na utajiri kama sharti mojawapo la mwananchi kupata haki ya kupiga kura kuchagua uongozi wa serikali ya madaraka ya ndani kuelekea uhuru wa Tanganyika.

Marehemu Mtemvu alipinga sharti hilo kwa madai kwamba matokeo ya uchaguzi huo yasingewakilisha hisia na matakwa ya wananchi wazalendo wa Tanganyika ambao wengi wao walikandamizwa kiuchumi na kunyimwa elimu ya kiwango kilichotakiwa isipokuwa wachache tu waliosomeshwa na Kanisa.

Mzee Zuberi Mtemvu alifariki mjini Dar es Salaam Septemba 20, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 71 na kuzikwa jijini katika makaburi ya Tambaza.

Maziko yake yalihudhuriwa na mamia ya wakazi wa jijini akiwemo Rais Mstaafu Alhaj Sheikh Ali Hassan Mwinyi.

Maziko hayo yalihudhuriwa pia na wanasiasa waanzilishi wa mapambano ya kudai uhuru wa Tanganyika akiwemo Alhaj Balozi Abbas Sykes.

Marehemu ameacha mjane na watoto kadhaa akiwemo Abbas Zuberi Mtemvu ambaye ni mmoja wa wanasiasa katika vyama vya upinzani nchini Tanzania.

Wakati huo huo habari kutoka London zinaeleza kuwa hali ya Mwalimu Julius Nyerere aliyelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa kansa ya damu katika hospitali ya St. Thomas London, bado ni ya kutatanisha. Hata hivyo ilielezwa kuwa madaktari walikuwa wamefanikiwa kumtibia kwa kiasi kikubwa magonjwa mengine yaliyojitokeza, ikiwa ni pamoja na homa ya manjano.

Taarifa ya Ikulu jana ilieleza kuwa Mwalimu ataendelea kuwekewa mashine za kusaidia kupumua kwa wiki moja zaidi.
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook