MAONI YETU
 
Wakuhubiri sheria nani
 

Kwa wengine, dhamana aliyopewa Sheikh Mbukuzi si stahili yake bali fadhila. Hao ni wale wasio makini na propaganda dhidi ya Waislamu. Propaganda ambazo hulenga kuhalalisha madhila wanayofanyiwa na vyombo vya dola.

Kwa propaganda hizo, Sheikh Mbukuzi alishahukumiwa na vyombo vya habari pamoja na Taasisi zilizokwisha agana na Waislamu. Mahakamani ilikuwa mahali pa kupita tu.

Lakini ipo haja ya kuepukana na kiza hiki cha propaganda kinachopotosha ukweli.

Suala hili lastahili kutizamwa katika yakini yake. Kile kinachozungumzwa au kutendwa na Waislamu kizingatiwe na kufanyiwa upembuzi sahihi. Kwa upande mwingine kile kinachojibiwa na kufanywa dhidi ya Waislamu kichambuliwe mantiki yake kwa kuzingatiwa yale yaliyosemwa na Waislamu.

Chakusisitiza hapa ni kuwa cha kuchambuliwa ni kile kilichosemwa wala si msemaji.

Katika suala la Sheikh Mbukuzi na wale wanaotuhumiwa kuandamana, alichosema kiliachwa ikawa suala ni kumshughulikia yeye na kuleta hoja za kanuni na taratibu. Lakini pamoja na hayo nani wa kumuelekeza Sheikh Mbukuzi kufuata sheria na kanuni. Na kanuni gani hizo zilizotumika kumhukumu kuwa mchochezi.

Kama ni sheria na kanuni tumezipa tafsiri gani. Sheria, kanuni na hata Katiba huwa wapi anapouliwa Muislamu.

Kwanini haki hii ya kutaka sheria na kanuni zifuatwe asiwe nayo Muislamu kuhoji polisi wanapoua watu Mwembechai! Kwanini haki hiyo wasiwe nayo kuhoji sheria na kanuni zinapoacha kutumika kuwashughulikia waliowaua Waislamu!

Ni nani wa kudai matumizi ya kanuni na sheria zinazolindwa na Katiba ya nchi.

Polisi wanaovamia Misikiti, waliowaweka Mzee Chatta na Mzee Katambo ndani bila kosa! Waliomshikilia Mohammed Omar na kukataa kufanya uchunguzi (Inquest) baada ya kufia mikononi mwao!

Nani wa kuhoji na kukumbushwa kanuni hizi; Waislamu waliompoteza Imam wao Mzee Chatta au polisi waliomuweka ndani na kumwachia akiwa taabani na kufa muda mfupi baadaye.

Nani wa kukumbushwa kufuata sheria na nani anayekiuka sheria za nchi. Sheikh Juma Mbukuzi anayedai polisi waliowaua Waislamu wafikishwe mahakamani au wenye mamlaka wanaozuia sheria kufuatwa katika suala hili.

Nani wanaopuuza sheria za nchi na kuvunja amani ya nchi; Sheikh Mbukuzi au wale waliompiga Chuki Athumani risasi na mpaka leo hawajaeleza sheria gani walitumia kumpa hukumu hiyo.

Nani wa kufikishwa mahakamani, polisi waliowadhalilisha akina mama Waislamu ndani ya Msikiti au Amir wa Waislamu anayekemea dhulma hii!

Ubalakala huu katika kutafsiri na kufuata sheria za nchi; isitegemewe kuwa Waislamu watakaa kimya wasihoji kwanini wafanywe daraja la pili.

Kama alivyosema Amir Mbukuzi hii sio hali ya kuachiwa iendelee. Lakini wapo watu wanaodhani kwa virungu vyao na kuwatia ndani watu mambo yatakuwa shwari pamoja na ubalakala huu kuendelea.

Baada ya kuua Waislamu Mwembechai na wengine kupoteza maisha yao wakiwa mahabusu na kisha serikali kukaa kimya; salam gani wanazopewa Waislamu. Kwamba waweza kuuliwa na kupigwa na isiwe kitu! Kwamba wao wameshahukumiwa (lakini kwa kosa gani) waweza kukamatwa wakawekwa ndani na kuachiwa polisi wanapofurahi.

Maadhali dhulma inaendelea isitarajiwe Waislamu kukaa kimya.

Maadhali ubalakala katika kufuata katiba na sheria za nchi unaendelea mengi kutoka kwa Waislamu yatarajiwe. Yatarajiwe kwa sababu ni katika mafundisho ya dini yao kupinga dhulma na kusimamia haki. Kama Qur'an yao inavyowaagiza, si katika sirah yao kuvunja sheria. Bali cha kutarajiwa ni umadhubuti wao na kudumu katika kuipigania haki yao.
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook