Baada ya Sheikh Mbukuzi kuendesha darsa gerezani
 
Wafungwa Keko waomba miswala
 

Na Mwandishi Wetu

WAFUNGWA na mahabusu Waislamu wa gereza la Keko jijini wamewaomba ndugu zao Waislamu wawapelekee mablanketi ili yasaidie kutandikwa sehemu wanayoswalia.

Wafungwa hao wamelifikisha ombi hilo kupitia Amir wa Waislamu Sheikh Juma Mbukuzi ambaye ameachiwa hivi karibuni kutoka rumande.

Imeelezwa kuwa kipindi alichokaa Sheikh Mbukuzi gerezani kimekuwa fursa kwa wafungwa kadhaa kubadili tabia ambapo hivi sasa wengi wao wanasimamisha swala tano gerezani hapo.

Sheikh Mbukuzi amemueleza mwandishi wa habari hizi kuwa ameitumia fursa ya kuwepo kwake gerezani kuendesha darsa kila baada ya Magharibi ambalo alisema liliwavutia wafungwa na mahabusu wengi.

"Nimeacha wafungwa wasiopungua 40 walioamua kusimamisha swala na wameahidi kudumisha mwenendo huo", ameeleza Sheikh Mbukuzi.

Aidha, amesema vijana kadhaa ambao baadhi yao ni wafuasi wa dini nyingine walivutika na yale aliyokuwa akiyaeleza wakati wote alipokuwa mmoja wa mahabusu wa gereza hilo.


Taasisi nchini zatakiwa kuacha kuwagawa Waislamu
 

Na Rajab Rajab, Morogoro

TAASISI za Kiislamu nchini zimetakiwa kukutana na kupanga kwa pamoja jinsi ya kuwaendeleza waumini wa dini hiyo badala yakuwagawa kwa tofauti mbalimbali zikiwemo za kimadhehebu.

Hayo yalisemwa Jumamosi iliyopita na waumini wa Kilakala mjini hapa walipokuwa wakisoma risala yao katika sherehe za Maulid kwa mgeni rasmi wa hafla hiyo Imamu wa Msikiti wa Ijumaa Mohammed Kairo.

Walisema kuwa mfumko wa taasisi uliojitokeza miaka ya hivi karibuni unazidi kuwachanganya waumini wa Kiislamu kutokana na taasisi hizo kuja na vitu vipya na kuacha mambo mbalimbali ya msingi ya dini hiyo.

Aidha, waliziomba taasisi zilizopo kuunda mfumo mmoja wa kutoa elimu kwa kuwa na mitaala na mihutasari inayofanana tangu shule za awali, msingi, sekondari hadi vyuo vikuu ili kujenga mazingira mazuri kwa vijana wa Kiislamu.

Vile vile waumini hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Waumini wa Kilakala (UWAKI) Ustadh Saidi Dogoli wamewaomba Maimamu na Waalimu wa madrasa kuendelezwa kitaaluma ili waweze kuwa na upeo mpana wa kueleza mambo vizuri zaidi kwa vile wamebeba jukumu kubwa la kuwaongoza vijana wa Waislamu kwa ujumla.

Waumini hao ambao kwa muda mrefu eneo lao limekuwa halina Msikiti wala madrasa, wametoa wito kwa Misikiti yote kuweza kutumika kama vituo vya kutolea elimu ya dini kwa watoto na watu wazima wa jinsia zote tangu asubuhi hadi jioni badala ya kuifanya (Misikiti) kama ni mahali pa kuswalia tu.

Pia katika risala yao wamelaani vikali mmomonyoko wa maadili uliopo nchini ambapo vitendo viovu vya wizi, uporaji, ujambazi, umalaya na kutembea nusu uchi vimetawala.

"Sisi tunaamini hali hiyo imetokana na ukosefu wa elimu sahihi ya dini na utekelezaji wa elimu hiyo kivitendo", ilisema sehemu ya risala hiyo.

Akijibu risala ya waumini hao Sheikh Kairo alisema kuwa lazima Waislamu wote nchini bila ya kujali tofauti zao ndogo ndogo wajenge umoja wenye nguvu na kufikia malengo ya kuusimamisha Uislamu hapa ulimwenguni.


TAMPRO wafungua ofisi Dodoma
 

Na Abu Zuberi, Dodoma

JUMUIYA ya Wanataaluma wa Kiislamu Tanzania (TAMPRO) imefungua ofisi rasmi katika mkoa wa Dodoma hivi karibuni.

Kabla ya ufunguzi wa ofisi hiyo uliyofanyika katika Chuo cha Ualimu Darul Muslimeen, Mshauri Mkuu katika idara ya dini kutoka TAMPRO, Ustadh Mussa Yusuph Kundecha aliwataka viongozi wa TAMPRO mkoani Dodoma na wanajumuiya wawe tayari kujitoa muhanga katika kuimarisha ofisi hiyo,

Ustadh Kundecha alisema kuwa juu ya uendeshaji wa ofisi hiyo kila mwanajumuiya anawajiibika kuchangia uendeshaji wake.

Aidha, aliwataka viongozi wa TAMPRO mkoa kuorodhesha Waislamu wote wenye taaluma mbalimbali ili wawe wanachama wa TAMPRO na kufahamiana.

Naye Mwenyekiti wa TAMPRO tawi la Dodoma Bwana Ally Iddi Ndekile alisema kuwa amefurahishwa kwa hatua iliyofikiwa ya kuwa na ofisi hiyo mkoani.

Mwenyekiti huyo aliahidi kushirikiana na viongozi wake ili waweze kuboresha harakati za Kiislamu mkoani.

Viongozi wa TAMPRO mkoani Dodoma ni Ally Iddi Ndekile (Mwenyekiti), Abdullah Saidi Hanchi (Katibu) na wajumbe watatu ambao ni Khan Nassoro, Rashid Futo na Athumani Kwariko.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook