Matokeo na mafunzo yaliyopatikana katika machafuko ya Soweto
 

TUMEONA huko nyuma kilichosababisha machafuko ya Soweto na pia tumeona wanafunzi wakiongozwa na Jumuiya yao, wakianzisha na kuendesha kampeni za kuhamasisha wa umma na kuaandaa Maandamano yaliyolipua hasira ya wazalendo.

Maelezo ya walioshuhudia matukio ya maandamano ya vijana, mashambulizi ya polisi kwa waandamanaji na hatimaye uchomwaji moto magari, majengo na kufanya kila aina ya uharibifu, yameonesha kitu kimoja ambacho tawala za mabavu hushindwa kukizingatia. Kwamba watu hulazimika kuungana kwa namna tofauti. Wanafunzi watakuwa wamoja kutokana na hali ya hayo. Halikadhalika wafanyabiashara, wafanyakazi na hata wakulima.

Baadhi ya wazalendo walilazimika kujiingiza kwenye mapambano baada ya kutafakari hali zao kijamii. Walikuja kuelewa kiini cha mapambano baadaye. Watu wengi walichukizwa na unyama uliofanywa na maaskari polisi dhidi ya wanafunzi, hivyo waliamua kuwaunga mkono vijana waliokuwa mstari wa mbele.

Yalipolipuka machafuko kwa mara nyingine Septemba, watu wengi walishiriki kwa namna moja au nyingine.

Hata madaktari na manesi wa hospitali zilizohudumia majeruhi walitoa mchango mkubwa katika mapambano hayo ya wazalendo wa Soweto dhidi ya utawala wa makaburu.

"Walimu, manesi, makasisi, wauzaji wa biashara za reja reja mitaani na makundi ya kinamama yalishiriki kwa kutoa misaada mbalimbali, waliwapa huduma ya kwanza majerehi, walichota maji kupeleka eneo la tukio ili kupunguza athari ya mabomu ya machozi" , ameandika mwandishi maarufu Bwana Hirson Baruch.

Kwa ujumla mauaji ya polisi Soweto, yaliwaunganisha watu wa daraja zote. Wakasimama kama wazalendo wanaodhulumiwa katika nchi yao.

Hilo linathibitishwa na takwimu rasmi zilizotolewa na Idara ya afya jijini Johanesburg kwamba waliouawa Juni na Agosti 18, 1976 asilimia 50 walikuwa vijana wenye umri kuanzia miaka 20 na asilimia 20 walikuwa watu wazima waliokuwa na umri zaidi ya miaka 30.

Sababu kubwa iliyochochea makundi hayo ni hali ngumu za kijamii na kiuchumi ambazo wakazi wengi wa mijini walikabiliana huku weupe wachache wakifaidi na kustarehe.

Wazalendo wengi walikuwa mafukara walioishi kwenye vibanda duni huku wakikosa matumaini juu ya hali yao ya baadaye. Ubaguzi wa rangi na kiajamii ulifanywa kuwa maisha ya Afrika kusini na kudai haki lilikuwa kosa lililostahili adhabu ya kuwekwa kizuizini, mateso na hata kifo.

Ukandamizaji huu ndiyo uliowafanya wazalendo kuungana kuwa dhidi ya utawala dhalimu.

Watu, hasa vijana, waliamua kujitoa muhanga kupambana na wakandamizaji wakijua wazi kufanya hivyo kungehatarisha maisha yao.

Hawakuwa tayari kuendelea kuwa raia wema chini ya utawala usiozingatia sheria na haki. Utawala wa kinafiki ambao maneno ya viongozi hayakuoana na vitendo.

Watu wa Soweto waliamua kuyatoa muhanga maisha yao kupinga mfumo wa utawala ulioamua kuikandamiza jamii fulani ya watu kwa sababu ya rangi.

Ubaguzi na ukandamizaji ulioshitadi kwa miongo kadhaa Afrika Kusini ulijenga njia kuelekea dhiki na vifo.

Watu walichotarajia bila kujali nani anaongoza, ni maendeleo, usaa na haki. Lakini badala yake kwa muda wote serikali ya John Voster iliandaa mazingira ambayo Mzungu angekuwa Bwana, mweusi angekuwa mtwana asiyestahili heshima wala haki za kiutu.

Maumbile ya wazalendo yalikataa mfumo huu wa maisha wa kikandamizaji, waliamua kuisaka haki yao kwa gharama zote zilizohitajika na hata baadhi yao kuamua kuyatoa muhanga maisha yao!

Mitaani, makundi ya watu, yalikuwa yakizungumzia mabadiliko na mapinduzi ya kijamii ambayo yangewang'oa wakandamizaji.

"Waondoshwe maadui wa jamii, wanaonyonya na kukandamiza wanyonge..... Siku za mwisho za wanaojinufaisha kupitia migongo ya masikini zinakaribia. Makabwela leo hii hawako tayari kuendelea kufanywa wajinga kwa misamiati mitamu nyakati za uchaguzi"

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook