Bakwata hawana jukumu la kuwathibitisha Waislamu
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi katika gazeti hili ili niweze kuielezea kauli iliyotolewa na uongozi wa Bakwata hivi karibuni kuhusiana na maandamano yaliyopangwa kufanyiwa, kufuatia Shura ya Maimamu kwamba "Bakwata hawaitambui Maimamu hao walio panga maandamano hayo" ni ya kichochezi.
Napenda niwakumbushe Waislamu wa Tanzania na kuwaelimisha viongozi wa nchi hii pamoja na wananchi wasio Waislamu, kuwa Bakwata haina jukumu la kumtambua wala kumtambulisha Muislamu kwa yeyote. Hivyo kauli ya kutoitambua Shura ya Maimamu na Maimamu imeifedhehesha serikali.
Ieleweke wazi kwamba Bakwata ni Taasisi kama zilivyo taasisi nyingine kama World Muslim Congress, IIRO, Africa Muslim Agency, CARITAS, CCT ni tofauti na vyama kama CCM, NCCR au TLP na nyinginezo ambavyo vinao uwezo wa kutomtambua mwanachama na hata kumfukuza uanachama yule anayekiuka kanuni za chama. Pia vyama hivi vinao uwezo wa kumkataa yeyote asiyetimiza masharti ya kujiunga.
Muislamu anajitambulisha yeye binafsi kwa Allah (s.w.) kwa Muislamu mwenziwe na kwa asiyekuwa Muislamu. Ama jamaa ya Waislamu inajitambulisha chini ya Maimamu.
Katiba ya Jamhuri inasema "Kila raia anao uhuru wa kuamini dini anayotaka...". Hili tamko linamhusu raia mmoja mmoja, na ndivyo Muislamu anajitambulisha kwa tamko la shahada: "Nakiri kwa moyo na ninatamka kwa ulimi kwamba hapana Mola apaswaye kuabudiwa kwa haki ila Allah (s.w.) na kwamba Muhammad (s.a.w.) ni Mjumbe wake". Sasa hao Bakwata wanataka watupe tamko zaidi ya hili?
Nayo serikali inapaswa kuwa na watendaji wazuri, kwani inapoambiwa na Bakwata kwamba Amiri Mbukuzi si Imamu inakubali tu ilhali Amir Mbukuzi ni Imamu wa Msikiti wa Mburahati Barafu, hii si agenda ya siri kati ya serikali na Bakwata?
Waislamu na kila mpenda amani wanapaswa kuwalaani watoaji wa kauli kama hizo, ambazo kila Waislamu wanapotoa madai yao dhidi ya uonevu kutoka kwa dola yao, utasikia. Pia yatupasa kufanya Istighfari kwa kushindwa kuuondoa uozo machoni petu, tumwambie Mwenyezi Mungu kuwa sisi tumeshindwa auondoe mwenyewe kwani Allah (s.w.) anasema: "... Sema haki imekuja, batili imeondoka, hakika batili ni yenye kuondoka". Hivyo tutake tusitake batili itaondoka tu.
Lililo muhimu zaidi Waislamu ni kuwa bega kwa bega na viongozi wetu sio kuwaacha wao wametangulia maili kadhaa, hatutafanikiwa malengo yetu abadan, Allah (s.w.) anasema: "Muhammad Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na walio pamoja naye ni wagumu kwa makafiri na wana hurumiana wao kwa wao...". Kwa hiyo yatulazimu kuwa bega kwa bega na viongozi wetu.
Mshindo S.M.,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi kidogo nitoe yangu machache, kufuatia serikai kumkamata Amir wa Shura ya Maimamu kwa madai ya kutoa kauli ya uchochezi.
Mimi nasema kukamatwa kwa Sheikh Juma Mbukuzi serikali inajijengea mazingira mabaya baina yake na Waislamu. Kauli ya Sheikh Mbukuzi ilikuwa na lengo la kuitaka serikali itende haki na iwape Waislamu haki zao za kikatiba bila upendeleo, pia kutoa wito kwa serikali na watendaji wake kulitazama suala hili kwa uzito unaostahiki na kuchukua hatua za makusudi zenye lengo la kulitatua tatizo hili kwa kikweli ili kuinusuru nchi hii na janga ambalo dhahiri litaikumba nchi iwapo ufumbuzi hautapatikana.
Jumanne Mussa Tetele,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
NAPENDA kutoa mchango wangu wa mawazo katika gazeti lako kufuatia kukamatwa kwa Amir wetu Sheikh Juma Salim Mbukuzi kutokana na kusema kwake ukweli.
Nitastajabu kusikia kauli za baadhi ya viongozi wa serikali wakinadi na kujisifia kuwa hizi ni zama za ukweli na uwazi ikiwa wao wenyewe hawautekelezi huo ukweli na uwazi, na wanapoambiwa ule ukweli wanakuja juu na jazba nyingi.
Badala ya kuyatafakari yale yanayosemwa na kuyafanyia kazi. Kitendo cha Bakwata kumuhukumu Amir wa Shura ya Maimamu Sheikh Juma Mbukuzi kuwa ni mchochezi na hatambuliki hiyo ni kwa wao Bakwata peke yao lakini sisi Waislamu tunamtambua na ndiyo tuliyemchagua wenyewe.
Jeta Gode,
Kisarawe,
Pwani.
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi kidogo katika gazeti letu tukufu la AN-NUUR niwaonye waandishi wa habari vibaraka kutokana na mwenendo na tabia zao, wawe na adabu, heshima na nidhamu wanapoandika habari zao.
Kutokana na kichwa cha habari cha gazeti moja toleo lake Na. 1236 la Jumamosi Septemba 18, 1999 kisemacho "Imamu msema ovyo asekwa korokooni Dar" kinaonesha chuki dhidi ya Waislamu.
Tunawataka wasirudie kututukania viongozi wetu wa dini. Sisi wenyewe (Waislamu) tunamheshimu kutokana na hadhi na cheo alichonacho. Waelewe kuwa huyu Amir (Sheikh Mbukuzi) ana cheo kikubwa kabisa hapa duniani na kesho akhera, sio kama hao wanaowajua wao.
Waislamu tunaitambua Shura ya Maimamu na Amir wa Shura hiyo pia tunamtambua na tutatii lolote atakalotuamrisha kwa ajili ya Allah (s.w.) na Mtume (s.a.w.) kwa maslahi ya dini yetu kwa sababu tumemchagua wenyewe wala hakuchaguliwa na serikali.
Abdallah O. Uliza,
Mburahati,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi japo pembezoni ili nipate kutoa maoni yangu.
Waislamu tunapiga kelele kuwa tunadhulumiwa. Wadhalimu wanasema kuwa kama kweli dhulma ipo tuwapelekee ushahidi wa kisayansi.
Ushahidi gani wa kisayansi zaidi ya mauaji ya Mwembechai! Ushahidi gani wa teknolojia wanaoutaka zaidi ya mtoto Chuki Athumani.
Waislamu madhalimu hawatatugaiya haki zetu kwa kuandika tu, kusema tu kuomba tu na kadhalika, kwa sababu kama kusema tumesema mpaka hivi sasa hao madhalimu wamechoka kusikia sauti zetu. Matokeo kamata weka ndani, piga, uwa.
Turudi kwenye mafundisho ya dini yetu. Allah anasema tusidhulumu wala tusidhulumiwe. Je sisi hatudhulumiwi? Na kama kweli tunadhlumiwa tunachukua hatua gani?
Salum H. Gubi,
Kisiju Mkuranga,
Pwani.
Ndugu Mhariri
NIPE nafasi kidogo ili nitoe muongozo kwa Waislamu wenzangu. Nimesoma gazeti lako na kuona viongozi wa serikali wameanza kampeni kwa Waislamu, kuna kiongozi mmoja amewaahidi Waislamu kuwajengea shule ya Kiislamu, ni katika kampeni za mwaka 2000.
Kwa hiyo Waislamu tuwe macho na kampeni kama hizi. Tukumbuke mauaji ya Mwembechai, kutembeza mkong'oto kwa Waislamu, kuwekwa ndani kwa Amir wa Shura ya Maimamu na kadhalika.
M.N. Mwanga,
Dar es Salaam.
|
|