Chakula na Lishe
 
Mwongozo wa lishe ya mtoto

Na Mujahidi Mwinyimvua

KATIKA nchi mbalimbali duniani hasa zile zinazoendelea kama Tanzania, watoto wenye umri chini ya miaka kumi, wanakabiliwa na matatizo ya lishe. Miongoni mwa matatizo hayo ni kukosa chakula cha kutosha na chenye virutubisho muhimu.

Matokeo ya hali hiyo ni pamoja na watoto hao kuwa dhaifu, kusumbuliwa na maradhi (kwa sababu hawana kinga asili), kudumaa, kupata ulemavu (upofu, upungufu wa akili, n.k.) na mara nyingine huwa vifo kwa watoto hao wadogo.

Sababu moja ya msingi ya lishe duni niliyoieleza hapo juu ni umaskini. Jambo hili (umaskini) linawafanya wananchi kushindwa kuzalisha au kununua chakula cha kutosha. Vile vile, umaskini ni kikwazo cha kupata huduma za kijamii kama vile elimu, maji safi na salama, matibabu mengineyo.

Makala hii inalenga kuchangia juhudi za kuongeza elimu ya chakula na lishe kwa wananchi.

Hata hivyo, kabla ya kuiendea azma hiyo ni vyema nikaweka sawa jambo moja.

Kuna gazeti moja la kidini linalotoka kila Jumapili (Dar es Salaam) katika Tahariri yake liliwahi kuwalaumu wazazi wanaotumia pesa zao kwa kuwanunulia watoto maziwa ili waepukane na vifo. Tahariri hiyo iliwahimiza wazazi (wananchi) wamtegemee Bwana Yesu badala ya maziwa.

Historia inaeleza kwamba, moja ya sababu zilizowafanya wanasayansi (na mfumo wa elimu ya sekula duniani) kuichukia dini na pia Mungu Muumba, ni mafundisho yaliyomo kwenye Biblia kupingana na taaluma ya sayansi.

Mafundisho ya dini iliyoridhiwa na Mungu Muumba (na vitabu vyake) kamwe hayasigani na elimu sahihi ya sayansi (tofautisha na maoni ya wanasayansi kama yale ya nyani kuwa chanzo cha binadamu).

Inachofanya taaluma ya sayansi asilia (Natural Science) ni kugundua maumbile ya ulimwengu na vile vilivyomo ulimwenguni na vilivyomo vimeumbwa na Mwenyezi Mungu, kwa hiyo ni kwa hoja hii ninasema taaluma sahihi ya sayansi haipingani na mafundisho ya dini sahihi (iliyoridhiwa na Mungu Muumba).

Kama kuna kusigana ima mafundisho ya dini inayohusika ni ya bandia au hoja zilizotumika siyo za kisayansi bali ni maoni (theories) za wanasayansi.

Kwa mujibu wa taaluma ya sayansi asilia, ni ukweli usiopingika kuwa vyakula yakiwemo maziwa yana mchango mkubwa katika uhai wa viumbe vyenye uhaki kama binadamu. Ndiyo kusema, mtu mwenye kupata chakula bora afya yake na umri wake huwa ni tofauti na yule asiyepata mambo hayo.

Kwa msingi huu, siyo ajabu inapotangazwa kuwa umri wa kuishi wa watu wa sehemu fulani umeongezeka kutoka miaka kadhaa na kuwa kadhaa.

Na haya si maajabu kwa dini sahihi. Kwa mujibu wa mafundisho ya dini sahihi, kuna watu waliowahi kuishi miaka elfu kasoro hamsini (yaani miaka 950).

Kinachowafanya watu kukanganyikiwa ni kushindwa kujua namna kadari (uwezo wa Mwenyezi Mungu) inavyofanya kazi. Kwa mfano, ni ukweli usiopingika kuwa enzi ya Mtume Muhammad (s.a.w.) hapakuwa na watu waliokufa kwa ajali ya gari (moto) au ndege (aeroplane). Kwa sababu, kwa wakati huo hapakuwa na motokaa wala ndege. Lakini tunashuhudia vifo vya mamia kwa maelfu ya binadamu wanaokufa kutokana na vyombo hivyo vya usafiri.

Haya yote ni katika Qadari (uwezo) ya Mola. Ndiyo kusema, watu wakiboresha huduma za kiuchumi, kijamii, kisiasa na nyinginezo maisha yao yatakuwa bora kuliko siku za nyuma. Hii yote iko ndani ya Qadari. Sasa unapomwambia mtu aache kununua maziwa kwa ajili ya afya ya mtoto wake, bali amtegemee Bwana Yesu, huku ni kumtumia Bwana Yesu (Mjumbe wa Mwenyezi Mungu) vibaya.

Baada ya kueleza hayo ya juu, ni vyema sasa turudi katika kiini cha makala hii (mwongozo wa lishe ya watoto).

Mtoto wa miezi 0-4

Inasisitizwa kupita kiasi kuwa mtoto mwenye umri wa siku 1 hadi miezi minne anyonyeshwe maziwa ya mama pekee. Haya ni mlo kamili kwa mtoto mwenye umri huo. Hata hivyo, mama anayenyonyesha lazima ale chakula cha kutosha na chenye virutubisho vyote (wanga, nyuzi nyuzi, protini, vitamini, madini na maji).

Mtoto lazima anyonyeshwe usiku na mchana zaidi ya mara kumi.

Mtoto wa miezi 4-6

Kama afya ya mtoto ni mzuri na mama anaendelea kutoa maziwa ya kutosha, inasisitizwa mtoto wa miezi 4-6 aendelee kupewa maziwa ya mama pekee. Lakini kama kuna matatizo, ni bora mtoto akaanza kupewa vyakula laini na visivyokuwa na sukari na chumbi nyingi, wala mafuta mengi. Kiini cha yai pia ni hatari kwa mtoto kwa sababu kina 'cholesterol' nyingi. Cholesteral ni moja ya chanzo cha magonjwa ya moyo na ubongo (stroke).

Mtoto wa miezi 6-12

Mtoto wa umri huu aendelee kupewa maziwa ya mama na pia vyakula laini. Vile vile apewe matunda.

Mtoto wa miezi 12 na zaidi

Huyu naye aendelee kupewa maziwa ya mama mpaka pale atakapoachishwa. Pia apewe vyakula vigumu kidogo. Vile vile apewe nyama, samaki, maziwa (ya wanyama), matunda na mboga mboga.

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook