Nani atajibu swali hili?
NCHI hii ina udini! Nani kauleta. Nini tafsiri ya dhana ya udini kwa ujumla. Nini tafsiri ya dhana ya udini kwa Watanzania. Nini tafsiri ya dhana ya udini kwa viongozi wa serikali yetu ya leo. Na nini ilikuwa tafsiri ya dhana ya udini kwa hayati Mwalimu Nyerere.
Haya ni maswali ambayo yapasa kujiuliza wakati tunamzika Mwalimu Nyerere.
Ni maswali muhimu kwa sababu tunamzika Mwalimu huku tukikariri yale muhimu aliyoyafanya. Wanasiasa wanakariri kuwa kaondoa udini, vyombo vya habari vinakariri kuwa kajenga umoja kwa kuondoa udini. Hali ni hiyo hiyo kwa baadhi ya watu wa tabaka mbalimbali katika jamii.
Wakati haya yakikaririwa kumbukumbu za hutuba za Mwalimu zinasema kuwa; Mwalimu akiwa mgeni Dar es Salaam miaka ya 1950 alipokewa na kuaminiwa na watu wa Dar es Salaam. Watu ambao hawakuwa wa kabila lake wala wa dini yake na dhehebu lake la Kikatoliki.
Kwa kauli yeke Hayati Mwalimu Nyerere alisema (Novemba, 1985):
"Wazee wa Dar es Salaam wakaniamini upesi sana. Nikawa na uhusiano mkubwa sana na wazee wa Dar es Salaam. Mimi Mkristo hawa Waislamu watupu wameniombea dua.... Mimi Mkristo wazee wangu Waislamu wale; lakini tulikuwa tunaelewana sana na wazee wangu.
"Wazee wengine wanakumbuka. Tumekwenda Bagamoyo kule; na wazee wangu. Labda Mkristo mimi peke yangu wakati mwingine John Rupia anakuja. La sivyo wazee wangu wale Waislamu na mimi mtoto wao (Mkristo)".
Mwalimu alisisitiza kuwa alikuwa akiyaeleza hayo kwa sababu huko tulikotoka tulishikamana sana. Huo ulikuwa ni wakati wa kudai uhuru na hata miaka iliyofuata mara baada ya uhuru.
Ni kwa muktadha huu watu wangependa wajue: Kama hayati Mwalimu Nyerere mwenyewe anasifu na kukiri kuwa waliompokea na kupigania uhuru nao hawakuwa na udini. Hawakuwa nao kwa vile pamoja na kuwa wote walikuwa Waislamu hawakumbagua kwa Ukatoliki wake. Kama leo tunasema upo udini, umeanza lini na nani kauleta?
Pengine imekuwa bahati mbaya kwamba Mwalimu ametutoka kabla hatujatanabahi kuuliza maswali haya muhimu.
Tungejua tukamuuliza Mwalimu mapema pengine yeye angetueleza huu udini unaosemwa, tafsiri yake ni nini, umeanza lini na nani kauleta. Je, ni wale aliokwenda nao Bagamoyo! Je, ni waliokuja kunufaika na kazi ngumu walioifanya akina Abdul Sykes na Dossa Azizi!
Bila ya kuwa na tafsiri sahihi ya suala hili na kupata majibu sahihi ya maswali haya; hatuwezi kudai kuwa tutamuenzi Mwalimu kwa kupiga vita udini. Lakini pia itabidi tuwe makini katika kila hatua tutakayochukua katika kulinda amani na kudumisha umoja suala la dini linapoingia.
Hayati Julius Kambarage Nyerere ameishi kama Mwalimu. Moja ya chumba chake cha Darasa ilikuwa Tanzania; sisi sote tulikuwa wanafunzi wake.
Mwalimu bora akisomesha hupenda pia kutekeleza kwa vitendo yale anayowaelekeza wanafunzi wake.
Mengi ameyatekeleza katika yale aliyosomesha. Lakini yapo mengi pia ambayo udhaifu wa kibinadamu na uhai haukumpa muda wa kuyakamilisha.
Ni imani ya wananchi kuwa walioachiwa uongozi wa nchi hii watayatekeleza yale ambayo Mwalimu hakuyakamilisha japo aliyafundisha.
Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa
maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye
Baraza
ya Wasomaji
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |