Wajibu wa waalimu mashuleni katika kuwalea wanafunzi wa Kiislamu


WALIMU wana jukumu kubwa la kuwabadilisha tabia wanafunzi, kutoka tabia mbaya na kuwa wenye maadili mema. Mafundisho yao hasa ya vitendo ni changamoto kwa wanafunzi yanaathari kubwa kwa wanafunzi. Mwanafunzi huamini kuwa Mwalimu wake ni mjuzi, hivyo humwiga. Akienda kinyume na maadili anaharibu jamii ya baadae.

Jukumu la kumlea mwanafunzi wa Kiislamu kwa mujibu wa mafundisho, malezi na maadili ya Kiislamu ni wajibu wetu sisi walimu wote tulio katika shule za serikali na hata zile seminari za Kiislamu. Japo malezi huanza kwa wazazi lakini baada ya muda jukumu hili zito hukabidhiwa Mwalimu. Mtume (s.a.w.) amesema katika kuwalea watoto: "Waadabisheni watoto wenu katika mambo matatu. Kumpenda Mtume wao (s.a.w.), kuwapenda watu wa nyumbani kwake na kusoma Qur'an (ikiwa ni pamoja na utekelezaji wake)".

Ni jukumu letu waalimu kuwaadabisha wanafunzi ili wawe safi kiimani, kiakili na kimatendo. Mtoto akiandaliwa basi ataweza kuwa tayari kuufuata Uislamu mahali, na wakati wowote bila woga.

Mazingira yanaweza yakawa chanzo cha kuharibika kwa mtoto. Mazingira ya kumwandalia mtoto ni yale yanayokubalika Kiislamu. Waalimu Waislamu wana jukumu hili la kuandaa mazingira bora kwa wanafunzi Waislamu katika shule zao.

Tuhakikishe kuwa watoto wa Kiislamu wanaishi Kiislamu japo katika shule ambazo haziendeshwi Kiislamu. Hili linawezekana penye nia. Watoto wote Waislamu wavae Hijab vizuri muda wote wawapo shuleni, wafundishwe dini yao na wahimizwe kuipenda dini yao. Wajibu wa jumla wa mwalimu Muislamu ni kuhakikisha mtoto anakuwa kiakili, kiroho na kimwili katika misingi ya Allah (s.w.).

Ni kweli usiofichika kuwa asiyeshughulikia masuala ya Kiislamu si miongoni mwa Waislamu. Mfano kuna vipindi vya dini mashuleni na walimu Waislamu wapo, lakini katika shule nyingi watoto wa Kiislamu ndio muda wao wa kutumwa na kupewa kazi za waalimu.

Katika shule zingine watoto huzagaa ovyo na kucheza mpira! Kama hatujui Qur'an hata tabia njema kwa watoto hawawezi kufundishwa? Kinyume chake Mwalimu Muislamu ndiyo anakuwa wa kwanza kukataza hijabu au utekelezaji wa swala, je bado unabaki kuwa Muislamu?

Jukumu letu ni kuleta mapinduzi kijamii, mabadiliko yatakayoleta haki na mshikamano wa kweli. Muda wa kutukanwa na wengine umekwisha na sasa tudhihirishe imani zetu kama wanavyofanya wenzetu. Mtume (s.a.w.) anatuambia yeyote mwenye elimu kisha hataki kuifundisha atavikwa mshipi wa moto siku ya kiyama.

Mwalimu wa Kiislamu unatakiwa kujua shule yako ina wanafunzi wangapi. Walemavu wangapi, wangapi hawakuja shule na kwa sababu gani, njia zipi zitumike kuondoa au kupunguza na kudhibiti tabia mbaya au matatizo ya wanafunzi Waislamu na hata wazazi wao. Sisi ni hazina ya jamii ya Kiislamu inayohitaji kuamshwa.

Watoto ni amana kutoka kwa Allah (s.w.). Hivyo tuna wajibu wa kuilinda amana hii. Muda tunaokaa nao wanafunzi utatosha kuwaandaa tukiwa na mipango mizuri ya matumizi ya muda. Tuwe na nia, bidii, subra na uvumilivu katika shughuli hii nzito huku tukitaraji malipo kutoka kwa Allah (s.w.).


Serikali iache vitisho


WAUMINI wa dini ya Kiislamu mjini Dodoma wameitaka serikali ya awamu ya tatu iache vitisho kwa raia zake hasa pale wananchi (raia wema) wanapotumia uhuru wa kikatiba kutoa maoni yao yenye muelekeo wa kuiokoa nchi hii.

Waislamu kadhaa ambao wameonesha kukerwa kwao kutokana na zoezi zima lililotanda la serikali kuwaandama Waislamu kwa kuwapiga virungu kuwasweka rumande kisha kuachwa huru bila ya mashtaka ni kukiukwa kwa katiba na uhuru wa kutoa (rai) maoni.

Bwana mmoja aliyejitambulisha kwa jina Karume Hussein, alisema haoni sababu za msingi iliyopelekewa serikali kumkamata Sheikh Mbukuzi.

"Ni nani haelewi kuwa Waislamu waliuawa pale Mwembechai? Nani haelewi kuwa katika Baraza la Idd Januari, 1999 Waislamu walimkabidhi risala Mheshimiwa Rais Mkapa, naye akaahidi kuwa atayashughulika madhila hayo ya Waislamu", alihoji Bwana Karume.

Mwingine aliyetoa dukuduku lake alikuwa mama Muganyizi ambaye alisema si vema kwa serikali kuwachukulia hatua raia wema kwa shinikizo la vyombo vya habari au BAKWATA.

Alisema kuwa serikali inapaswa kuangalia ukweli na siyo kushinikizwa na nguvu nyingine za nje.

Wakati huo huo, Imam wa Masjid Manyema mjini Dodoma, Sheikh Ahmed Said amewataka Waislamu wadhihirishe Uislamu wao.

Akiwahutubia Waislamu katika sala ya Ijumaa hivi karibuni Sheikh Said alisema dini ya Kiislamu imeletwa ili iwe juu ya dini zote.

"Tekeleza amri za Allah popote pale iwe ofisini au sehemu yako ya biashara, aidha alisikitika hususan kwa baadhi ya akinamama wa Kiislamu wanapokuwa maofisini huwezi kuwatofautisha na wale wasio Waislamu".

Aliwataka wafanyabiashara wa Kiislamu waache udanganyifu katika kuuza na kununua kwao, kupunja katika mizani, kwani tabia hizo Allah (s.w.) amezikemea sana, alisisitiza Sheikh huyo.


Ubungo yakabiliwa na shida ya maji

KWA wiki tatu mfululizo wakazi wa Ubungo Jijini Dar es Salaam wamekuwa katika shida kubwa ya maji.

Akina mama wa eneo hilo wamekuwa wakihangaika huku na kule usiku na mchana wakitafuta maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Kabla ya kuzuka uhaba huu, ambapo plastiki (ndoo) moja ya maji imefikia kuuzwa kwa bei ya shilingi 200, eneo la Ubungo lilikuwa likipata maji kwa siku tatu kila wiki.

Mwandishi alishuhudia baadhi ya watu wakiwa wamebeba ndoo saa tano za usiku wa kuamkia jana katika eneo lililokaribu na shule ya msingi Ubungo Kisiwani.

Akiwa ameshika ndoo zake mbili huku akionekana aliyekata tamaa mama mmoja ambaye alijitambulisha kwa jina la mama Suleiman aliilalamikia DAWASA kuwa imeshindwa kutekeleza wajibu wake.

Alisema Ubungo imekuwa ikikabiliwa na shida ya maji kwa muda mrefu sasa bila ya ufumbuzi.

"Tumeweka mabomba majumbani mwetu lakini maji hatupati, bili za maji tunaletewa, hawa jamaa wa DAWASA wanafanya kazi gani?" Alihoji mama huyo.

Naye Bi Hawa Adam akiwa na mtoto wake mgongoni alikutwa na mwandishi akiwa ameduwaa baada ya kukosa maji.

"Sijui nitapata wapi maji usiku huu jamani", alisikika akiuliza kwa masikitiko mama huyo.

Jitihada za kuwapata viongozi wa DAWASA jana hazikuweza kufanikiwa kufuatia ofisi zote kufungwa jana kwa ajili ya shughuli za kusafirisha mwili wa hayati Mwalimu Nyerere zilizochukua siku nzima juzi na jana.

--
JuuRUDI



 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji


   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook