Kama alivyoleta uhuru,
karne ijayo itakuwa ya maisha bora kwa Watanzania.
Hayo ni maneno ya faraja yanayoweza kunyambuliwa kutoka katika hotuba ya Rais Benjamin William Mkapa kwa Watanzania aliyoitoa jana wakati wa kuuaga rasmi mwili wa hayati Mwalimu Nyerere.
Rais alisema kuwa kama Mussa alivyoletwa kuwakomboa Wayahudi; Mwalimu alitukomboa akaleta uhuru na kuandaa kutupa maisha bora zaidi.
Akaongeza kuwa ni imani yake kuwa karne itakayokuja Tanzania itakuwa nchi yenye maisha bora zaidi.
Kwa nafasi hiyo ya Mwalimu katika Taifa hili, alipewa jina la utani Mussa, alisema Rais.
Akimfananisha Mwalimu na Mtume Mussa; Rais Mkapa alisema kuwa Mwalimu kaondoka kabla Watanzania hawajaingia katika karne yenye matumaini mema kwetu.
Kwa ajili hiyo Mhe. Rais amewaahidi Watanzania kuwa yale yote aliyoyaanzisha Mwalimu yatasimamiwa kikamilifu.
Kumbukumbu za vitabu vya dini zinaeleza kuwa Mussa alikufa mwaka wa 38 wa kipindi cha adhabu. Miaka miwili baadae Joshua akisaidiana na Kaleb waliiteka Palestina wakaanza maisha bora hadi walipoasi tena miaka 25 baadaeRais amesema aliyofanya Mwalimu ni urithi kwa Watanzania, na hatakubali uwaponyoke.
Rais akitoa hotuba yake mbele ya Marais wa nchi za nje, wageni mbalimbali na wananchi alisema kuwa umoja, udugu na upendo utasimamiwa na kudumishwa. Haki na Usawa utaimarishwa pamoja na Muungano.
Katika hadhara hiyo ya kuuaga rasmi mwili wa Mwalimu, Rais alisema kuwa msiba ulioikumba nchi ni mzito. Hata hivyo akasema kuwa mshikamano ulioonyeshwa wakati wa ugonjwa wa Mwalimu na katika msiba ni mwanzo mzuri wa kuanza maisha bila ya Mwalimu.
Marais na wageni mbalimbali walitoa salamu zao za rambirambi.
Salamu hizo zilisherehesha sifa kemkem za Mwalimu na mchango wake katika masuala mbalimbali ya Taifa; Afrika na Dunia kwa ujumla.
Aliyeonekana kuwa na huzuni zaidi alikuwa Rais wa zamani wa Zambia mzee Kenneth Kaunda.
Tofauti na wengine, yeye alipiga magoti kando ya sanduku ulimokuwa mwili wa Mwalimu. Akakaa katika hali hiyo kwa muda mrefu kwa huzuni akionekana kusali. Kisha akatoka taratibu kwa huzuni kubwa sana.
Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa
maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye
Baraza
ya Wasomaji
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |