UMEKUWEPO wasiwasi miongoni mwa watu kuwa huenda amani, utulivu na umoja wa Taifa ukatetereka baada ya kufa Mwalimu Nyerere.
Wiki iliyopita katika toleo letu Na. 223 tulianza kuelezea kile kilichoitwaMoyo wa Upendo wa TANU.
Tunaimani Moyo huu ukiendelezwa hakuna sababu ya kuwa na hofu.
Rejea pale tulipokomea wiki iliyopita kisha endelea...Tabora likiongozwa na Mzee Muhidi.
Kazi ya awali ya Baraza hili ilikuwa kuweka mipango ya kupeleka suala la uhuru wa Tanganyika katika Baraza la Udhamini. Mipango hiyo ndiyo iliyopelekea Mwalimu kwenda New York Februari, 1955.
Waliosaidia kukusanya fedha za safari hiyo walikuwa Abdul Kandoro, Japhet Kirilo na Abbas Sykes. Wengine walikuwa John Rupia. Idd Faiz Mafongo (aliyekuja kuwa Bwanafedha wa TANU) alitumwa Tanga kuleta fedha ambazo zilikuwa zimekusanywa na Mwalimu Kihere.
Mwalimu Nyerere alirudi kutoka New York Jumamosi Machi 19, 1955, umati mkubwa wa watu ulijitokeza uwanja wa Ndege kumlaki. Dossa Azizi aliruhusiwa kuingia na gari lake hadi eneo la ndege ilikosimama ili kumchukua Mwalimu Nyerere.
Wananchi waliohudhuria walilisukuma gari lililombeba Mwalimu Nyerere hadi Magomeni huku wakiimba na kucheza ngoma ya Kizaramo, mganda. " Baba Kabwela Yuno" ndio wimbo waliokuwa wakiimba ikimaanisha Baba wa Wanyonge karudi toka Yuno.
Baada ya harakati za kupigania uhuru kupamba moto, Wamishionari wa Mtakatifu Francis (St. Francis College Pugu) hawakuwa tayari kuendelea na Mwalimu. Walimtaka achague siasa au kazi.
Mwalimu aliwasilisha tatizo hili kwa Kamati Kuu ya TANU ambapo alishauriwa aache kazi. Na akafanya hivyo Machi 23, 1955.
Kutokea hapa akafanya kazi ya TANU hadi tulipopata uhuru.
Mwalimu Nyerere akielezea maisha yake ya awali ya kisiasa na jinsi wazee wa Dar es Salaam walivyojitoa muhanga kuleta uhuru alisema mwanzo wake katika siasa alipelekwa kwa Abdul Sykes na Abdul Sykes akamtambulisha kwa viongozi wenzake. Kisha akaendelea kusema: "Wenzangu wakanipokea. Nikawa nakuja na kwa muda mfupi, mwaka ule, tukafufua African Association kuanzia Januari pale. Kufika Aprili imefufuka. Kufika Aprili ikawa imefufuka, tukafanya mkutano Anatoglo pale wakanichagua, wakanichagua kuwa President wao, wa Tanganyika African Association. Nasema hili, haya yote nawaelezeni, nataka kutoa shukrani zangu za dhati kabisa. Kwa sababu jamaa hawa walionichagua hawa watu wazima hawa.
"Nimekuja natoka Ulaya tena msomi, msomi ninakuja, nimetoka Ulaya, nimesoma. Muda mfupi tu, jamaa hawa wa mjini Dar es Salaam kwa kweli sijapata kuishi mjini, lakini jamaa hawa mara wakaniamini haraka haraka sana. Wakaniamini haraka sana.
"Katika muda wa miezi mitatu wakanichagua President wa African Association. Tanganyika African Association. Ndipo tukaanza sasa shughuli za kujaribu kuandika Katiba mpya ya TAA kusudi tuipe madhumuni ya shabaha ya kuleta uhuru.
"Mwaka uliofuata 1954 ndio tuka, kwakweli mimi nilidhani tutachukua katiba tu, tutabadili katiba tu, wenzangu wakasema hapana. Tukibadili katiba tubadili na jina.
"Tukahangaika sana kupata jina na hao hao kina Abdul Sykes, jina lile hatukuligundua. Wao walikuwa wamelifikiria zamani wakina Abdul Sykes hao. Walikuwa Burma alikuwa askari na kule waliwahi kufikiria kuanzisha chama. Kusema kweli wao waliwahi kufikiria kabisa Tanganyika African National Union.
"Kwa hiyo wakati tunahangaika hangaika pale tuchukue jina gani tufanye Tanganyika African Union wakasema hali itafanana na Kenya African Union. Watadhani nao ni Maumau. Tunataka kuanzisha hapa Maumau yetu. Ndio wakina Abdul Sykes wakakumbuka jina lao waliokuwa wameliunda walipokuwa Burma, wakasema tuite Tanganyika African National Union Ndio tukaanzisha.
"Nasema mwezi wa nne tangu kuanza kazi pale Pugu nikawa nakuja, sasa wazee wamenipa baiskeli nilikuwa nakuja kwa miguu kutoka Pugu, nakuja na kukutana na wenzangu kila Jumamosi. Jumamosi kama leo hivi, na saa hizi ama nimeshafika au niko njiani nakuja kukutana na wenzangu tupange mkutano. Ndivyo tulivyofanya.
"Wazee wa Dar es Salaam wakaniamini upesi sana. Kijana mdogo sana. Nikawa na uhusiano mkubwa sana na wazee wa Dar es Salaam. Mkubwa sana. Watu wazima mimi mdogo. Wadogo wenzangu wengine walikuwa ni hao Abdul Sykes kina Abbas Sykes, wakina Dossa. Lakini wengine wote walikuwa ni watu wazima.
"Nasema wazee wa Dar es Salaam baadae wananchi nchi nzima wakatuunga mkono sana. Na kila nilipokuwa nikitembea, watu wa kwanza kabisa walionielewa nasema mimi wazee. Mambo haya makubwa ya nchi, kama hayana baraka za wazee hayaendi. Magumu sana. Wanasema ngoma ya watoto haikeshi.
"Safari moja Dossa aliwahi kunifuata. Kunifuata Magomeni pale. 'Leo wazee wanakuita'. Wapi "kwa Mzee Jumbe Tambaza". Wanakutana usiku. Nikasema vyema nitakuja. Nikaja. Nikafika pale tukakaa. Wazee watu wazima wameshakaa wameniita kijana wao kuniombea Dua. Usiku, watu wazima wamejaa mle chumbani kwa Mzee Tambaza nikaombewa Dua.
"Mi Mkristu hawa Waislamu watupu. Wameniombea Dua za ubani, tumemaliza. Tulipomaliza wazee hao Dua wameomba, lakini na Dua za wazee wao hawakusahu.
"Basi wakanitoa nje, wakaniomba nitoke nje. Tukatoka nje. Sasa hizo zilizomalizika hizo za Qur'an na sasa zikaja, zikaja Dua za wazee wa jadi.
"Mimi Mkristu, wazee wangu Waislamu wale, lakini tulikuwa tunaelewana sana na wazee wangu. Wazee wengine wanakumbuka. Tumekwenda Bagamoyo kule; na wazee wangu. Labda Mkristu mimi peke yangu au wakati mwingine John Rupia anakuja. La sivyo wazee wangu wale Waislamu na mimi mtoto wao. Tunakwenda kuomba Dua huko. Baadhi yenu mtakumbuka.
"Safari moja jamaa wa Kenya wakina Tom Mboya hawa walikuwa na mashitaka, walishitakiwa. Tukasema tuwasaidie. Tuwasaidieje hawa, tufunge. Tukaiomba nchi nzima kufunga siku hiyo. Tufunge, tukafunga. Tukafunga siku hiyo.
"Na siku hiyo ya kufunga tuna mkutano Bagamoyo. Tumekwenda Bagamoyo kwenye mkutano. Saa kama hizi tumeanza mkutano. Tumeendelea mpaka labda saa kumi na mbili. Kabla ya saa kumi na mbili tumemaliza mkutano.
"Tumekwenda kwa mzee Mohamed Ramia, marehemu. Tumekwenda kwake ndipo tulipofikia pale. Nikamwambia mzee Sheikh una Aspro? Akaniambia kwanini unataka Aspro. Nikasema kichwa kinaniuma kweli kweli.
"Akaniambia usiwe na haraka hebu subiri. Tukasubiriii. Mpaka saa za kufuturu zikafika. Tukafuturu vizuri. Akaniambia bado unataka Aspro? Nikamwambia hapana. Kichwa kilikuwa hakiniumi. Kumbe kichwa kinaniuma kwa sababu ya njaa.
"Nawalezeni haya wazee kwa sababu huko tulikotoka, tulitoka pamoja na wazee, wazee wa nchi tulishikamana sana, tulishikamana sana, walinisaidia kweli kweli". (Mwalimu Julius Nyerere, Novemba, 1995)
Kisa kingine cha kuonesha moyo wa upendo wa TANU ambao Mwalimu ulikuwa haumtoki katika mazungumzo yake na kukieleza kila alipopata nafasi, ni kile alichomueleza marehemu Profesa Kighoma Ali Malima. Mwalimu alikuwa anazungumza na Profesa Malima nyumbani kwake na katika mazungumzo; Mwalimu alinyanyuka alipokuwa amekaa na kwenda chumbani kwake akatoka na moja ya picha za wakati wa kudai uhuru, akamuonyesha Malima. Mwalimu akasema "Profesa unaona picha hii, Waislamu watupu, Mkristo ni mimi peke yangu."
Mwalimu amefariki dunia wakati nchi yetu ipo katika hofu ya kuvunjika kwa amani. Waislamu ambao walikuwa mstari wa mbele kumpokea Mwalimu na kumuunga mkono katika kudai uhuru wanaichagiza serikali iwafanyie uadilifu kwa kuwa kuna watu ndani ya serikali wameweka maslahi ya dini zao dhidi ya maslahi ya taifa.
Katika kufanya hivyo vyombo vya Dola vimeshamwaga damu ya Waislamu pale Mwembechai. Kuthibitisha kuwa ule moyo wa upendo wa TANU umeshatoweka na hakuna haki wala uadilifu; kilio cha Waislamu kuwa Katiba na sheria za nchi zitumike kulihukumu suala la Mwembechai, kimeangukia sikio la uziwi na macho ya upofu ya serikali.
Hii ni hatari ya wazi na inatishia uhai wa nchi yetu. Waislamu walioleta uhuru wa nchi hii wanashangaa wanaposoma magazeti na kuambiwa na wanasiasa kuwa wao wanataka kuvuruga amani. Kinachowashangaza ni kwa vipi wao wapiganie uhuru wa nchi hii kisha wao waanze kuuvuruga.
Mwalimu ameondoka, wakati watoto, wajukuu na jamaa zao akina Dossa Azizi wanasubiri kauli ya serikali juu ya damu ya Waislamu iliyomwagwa pale Mwembechai.
Nafasi za mbele katika mazishi na maombolezo watachukua wale waliokuja kumkumbatia na kumpenda Mwalimu baadae kwa kuwa kufanya hivyo kuna maslahi makubwa kwao. Laiti kama Mwalimu angeliweza kufunua macho na kuangalia umma unaoomboleza kifo chake kwa hakika kabisa akili yake ingerudi nyuma zaidi ya miaka ya arobaini na kuwakumbuka rafiki zake waliompokea Dar es Salaam na katika TANU katika miaka ya 1950. Kwa rehema za Mungu marafiki zake akina Abdul Sykes, Dossa Azizi, Sheikh Mohamed Ramia, Mzee Mohamed Jumbe Tambaza na wengineo wameshatangulia mbele ya haki. Kwa bahati mbaya wale walio hai kama Mzee Shaaban Gonga, Mzee Juma Mlevi na Mzee Rashid Sisso, historia imekataa kuwatambua. Kwa ajili hii basi wataomboleza kifo cha rafiki yao kimya kimya na katika upweke.
Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa
maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye
Baraza
ya Wasomaji
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |