Tufuate mila ya Ibrahim ila katika neno lake...


Na Abu Qassim

KUMEKUWA na utata kama kuwaombea dua wasio Waislamu ni sahihi au sio sahihi. Hivyo makala hii inajaribu kwa undani kuoanisha msimamo wa Uislamu juu ya jambo hili kama ifuatavyo: Turudi nyuma kidogo na tuishi katika enzi ya Mtume Nuhu (a.s.w.) gharqa kwa watu wa Mtume Nuhu ni darasa mashuhuri lisilohitaji sherhe.

MIONGONI mwa waliogharikishwa ni mtoto wa Mtume Nuhu. Wakati wa tukio Mtume Nuhu akimwita mwanae aliyekuwa mbali: "Ewe mwanangu panda pamoja nasi wala usiwe pamoja na makafiri" (11:42).

Mtoto wake akajibu: "Nitaukimbilia mlima utakaonilinda na maji". Akasema (Nuhu) hakuna leo wa kulindwa na amri ya Mwenyezi Mungu isipokuwa atakaye mrehemu. Mara mawimbi yakaingia baina yao na akawa miongoni mwa waliogharikishwa. (11:43).

Hapo ndipo Nabii Nuhu alipomuomba Mola wake kwa kusema:

"Ewe Mola wangu! Mwanangu ni katika watu wa nyumba yangu. Na hakika ahadi yako ni haki, nawe ni mwenye haki kuliko mahakimu (wote)". (11:45).

Baada ya ombi la Nuhu kumuombea mwanae aliyejiweka pamoja na makafiri (11:42) ndipo tunapopata fundisho kuwa kwa Muislamu haifai kabisa kumuombea asiyetamka shahada (11:42) kama alivyofanya mtoto wa Nuhu kwa namna Mwenyezi Mungu alivyomsomesha Nabii Nuhu.

"Ewe Nuhu! Huyu si miongoni mwa watu wako. Yeye ni miongoni (mwenye) mwenendo usiokuwa mzuri. Basi usiniombe ambayo huyajui. Mimi nakusihi usiwe miongoni mwa wajinga". (11:46).

Ikiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ameambiwa hivi kuhusu mwanae asiyetamka shahada, basi ni dhahiri kufanya hivyo sisi leo ni katazo na kufanya hivyo ni dhambi.

Funzo hili pia limekaririwa kwa Nabii Ibrahim historia yake pia ni maarufu katika darasa za historia. Nukta ninayoisoma ni ile ya dua ya Ibrahim kumuombea baba yake na jibu la Mwenyezi Mungu.

Nabii Ibrahimu alimwambia baba yake asiabudu visivyosikia, visivyo ona na visivyomfaa chochote (19:42) Ibrahimu alimfahamisha baba yake amfuate atamuongoza njia kwa vile ana elimu asiyopewa baba yake (19:43) kisha alimuasa asimuabudu shetani kwa kuwa shetani anamuasi Mungu wake (19:44). Na hatimaye akamfahamisha baba yake kuwa yeye Ibrahimu ana khofu kuwa baba yake asije kupata adhabu (19:43).

Baba yake Ibrahimu alimjibu mwanae kwa kuonesha mshangao kuwa Ibraihimu anaichukia miungu yake. Kisha akaahidi kumpiga mawe na akamfukuza (19:46).

Hapo ndipo Nabii Ibrahimu akasema: "Amani iwe juu yako! Nitakuombea msamaha kwa Mola wangu, bila shaka yeye ananihurumia sana (19:48).

Tendo hili la Mtume Ibrahimu la kutamka "nitakuombea msamaha kwa Mola wangu". (19:48) limemchukiza Mwenyezi Mungu hakulitaka lifanyike. Ukweli huu unadhihirishwa katika sura ya sitini (60) aya ya 4 (nne) pale Mwenyezi Mungu alipotutaka tumuige Ibrahimu ila katika usemi wake Ibrahimu kumuombea baba yake. Hakika nitakuombea msamaha wala sina uweza wa chochote kwa ajili yako mbele ya Mwenyezi Mungu..." (60:4).

Ushahidi mwingine unaoonesha kuwa Muislamu haruhusiwi kumuombea mtu asiyetamka shahada au mshirikiana, ni wakati mazishi ya Abdullah bin Ubayy huko Madina muda mfupi baada ya msafara wa Tabuk. Mtoto wake ambaye alikuwa Muislamu mwema alimuaomba Mtume (s.a.w.) aongoze swala ya maiti na Mtume kimsingi alikubali, lakini Umar kwa heshima alimkumbusha Mtume uovu wa hayati dhidi ya Uislamu Mtume aliposimama tu kumswalia sawia akashushiwa aya ya 84 ya surat ya tisa inayomkataza kumswalia Abdallah bin Ubbayy inayosema:

"Wala usimswalie kamwe mmoja wao yeyote yule akifa, wala usisimame kaburini kwake (kumwombea dua). Hakika wao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume na wakafa na hali ni wenye kuvunja amri (9:84). Iliposhushwa aya hii Mtume aliacha kumswalia marehemu yule. Tukio hili limepelekea kuwekwa kanuni katika Uislamu kuwa viongozi wema wa dini na Waislamu mashuhuri kwa ucha Mungu wao wasiwaswalie wala kuongoza swala ya maiti ya watu wanaofahamika kwa tabia zao dhidi ya Uislamu. Tangu litokee tukio hili Mtume hakumswalia maiti yeyote ila aliuliza alivyokuwa na ikibainika kuwa alikuwa dhalimu dhidi ya Uislamu aliwaambia watu wake: "Mnaweza kumzika mpendavyo".

Halikadhalika kemeo la kuwaombea wasioishi maisha ya shahada na Tawhiid limetajwa katika suratul Tauba aya ya 80 kama ifuatavyo:

"(Ewe Mtume!) Waombee msamaha (hao wanafiq) au usiwaombee. Hata ukiwaombea msamaha mara sabini Mwenyezi Mungu hata wasamehe. Hayo ni kwa sababu wao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu wavunjao amri (zake). (9:80).

Lakini sunna ya Mwenyezi Mungu haibadiliki. Kama alivyo Mitume waliotangulia Nuhu na Ibrahimu ndivo hivyo hivyo alivyomnasibisha Mtume Muhammad (s.a.w.). Imamu Bukhari katika kitabu cha pili (Sahihi Al-Bukhari) hadithi namba 442 ukurasa 248 ameandika hadithi ifuatayo:

"Amesimulia Said bin Al- Musaiyab kutoka kwa baba yake kuwa: Kifo cha Abu Talib kilipokuwa kinakaribia Mtume wa Mwenyezi Mungu alikwenda kwa baba yake mdogo na alimkuta ndani humo Abu Jahl bin Hasham na Abdallah bin Abi Umaiya bin Al-Mughira wakiwa wamekaa nae. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alimwambia Abu Talib "O baba mdogo sema; Hapana apasae kuabudiwa ila Allah. Kauli ambayo mimi itaniwezesha kukuombea mbele ya Mwenyezi Mungu. Abu Jahl na Abdallah bin Abi Umaiya wakamuuliza. "O Abu Talib! Utaacha dini ya Abdul Muttalib?

Mtume (s.a.w.) aliendelea kumlingania baba yake mdogo atamke shahada. Wakati huo huo Abu Jahl na Abdullah waliendelea na tamko lao mpaka Abdul Mutalib akatoa tamko lake la mwisho kuwa anafuata dini ya Abdul Muttalib na amekataa kutamka - Hapana Mola apasae kuabudiwa ila Allah. Kutokana na kauli hii Mtume akasema: Kuwa nitaendelea kukuombea maghufira kwa Mwenyezi Mungu mpaka Mwenyezi Mungu anikataze: Ndipo Mwenyezi Mungu akashusha aya isemayo haipaswi Mtume na wale walioamini kuwatakia samahani washirikina hata kama ni jamaa (zao), baada ya kuwabainikia kuwa wao ni watu (watu wa) Jahannamu? (9:113)

Haya ndiyo maagizo ya Mwenyezi Mungu kuhusu kuwaombea wasiotamka shahada.

Waarabu waliwaheshimu sana viongozi wao na Abu Tallib alikuwa miongoni mwa viongozi walioheshimiwa na Maquraishi. Pamoja na kuwa hakusilimu lakini Mtume alikuwa chini ya dhamana yake mbele ya jamii ile ya Maquraish. Ndio maana Makafiri wa Kiquraish walimuendea Abu Talib kumtaka amuase mwanae aache kuhubiri Uislamu kwa namna kadhaa. Mara moja walimtisha na kumuonya kuwa asipomkataza mwanae basi atakiona. Hapa ndipo Mtume (s.a.w.) alipojibu kuwa hata kama jua litawekwa mkono wa kulia namwezi mkono wa kushoto sitoacha kazi ya kufundisha Uislamu. Abu Tallib kusikia hivi alimwambia mwanae aendelee yuko naye.

Sio hivyo tu lakini Abu Talib hakumuacha mwanae hata pale ilipofikia wafukuzwe Makka na wakakaa kwenye bonde la Shabi Abi Thahib kwa muda wa miaka mitatu. Abu Talib na ukoo wa Bani Hashim walikubali mateso hayo kuliko kumtenga ndugu yao wa damu. Hivyo hali ilikuwa hii hadi alipofariki Abu Talib. Kutokana na hali hii ndiyo maana Mtume alisema nitakuombea maghufira mpaka Mwenyezi Mungu aamue vinginevyo.

Angalia sasa Mwenyezi Mungu alivyokuwa mkali kuhusu suala la kuwaombea wasiotoa shahada. Pamoja na yote aliyoyafanya Abu Talib kumsimamia Mtume kufanya kazi yake ya Utume bado Allah ameagiza kuwa haimpasi Mtume na wale masahaba walioamini kuwatakia samahani.

Hii ndiyo hali ya wasiotamka shahada lakini waliousaidia Uislamu kwa namna moja au nyingine. Tunaambiwa tusiwaombee Dua.

--
JuuRUDI



 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji


   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook