Ni kumkomboa au kumdhalilisha mwanamke
Ndugu Mhariri
HARAKATI za "kumkomboa" mwanamke dhidi ya mafundisho ya Uislamu zinaendeshwa dunia nzima na Tanzania imekwishajiunga na mbio hizo. Lakini hebu na tujaribu kuangalia japo kwa uchache sana "uadilifu" na "ukweli" wa wakombozi hao wanaojigamba kumtetea mwanamke.
Tuitizame kwa undani sana mifano michache ifuatayo ambayo kwa mwenye akili timamu na iliyo huur atakubaliana nami kuwa harakati zote hizo zina ajenda nyingine tu na wala si kumkomboa mwanamke kutokana na kuonewa na kudhalilishwa. Kwanza ni lile la kuvuliwa wanawake na kubaki uchi hadharani katika jina la mashindano ya urembo. Nasema wanawake hawa wanavuliwa kwa sababu kuvua kwao nguvu zao si jambo la hiari ingawa picha ya nje inajionyesha hivyo.
Nasema si jambo la hiari kwa kuwa wanafanya hivyo kutokana n ahadi zitolewazo kuwa washindi watazawadiwa na hivyo kuwafanya kinadada hao kujidhalilisha hadharani hivyo kwa sababu tu ya pesa hizo wanazoahidiwa, kwa sababu ya magari hayo yanayoahidiwa, kwa sababu ya tiketi kuzuru nje wanazoahidiwa na kadhalika. Sidhani kama wangekuwa tayari kujiadhiri hivyo ikiwa ahadi au zawadi kwa mshindi ingekuwa kupigiwa makofi tu na kushangiliwa.
Mfano mwingine ni ule wa wanawake katika magazeti ya ngono. Gazeti litolewalo katika lugha ya Kiingereza kutoka nchini Uganda liitwalo Spice ni mfano halisi wa hili ninalozungumzia.
Kila nakala ya gazeti hilo huwa na mwanamke aliye uchi ambaye "hupamba" jalada la mbele la gazeti hilo. Wanaopigwa picha za uchi namna hiyo magazetini wako katika kundi moja tu na wale wa "mashindano ya urembo" juu ya majukwaa, wote wasingekubali kashfa hiyo kama mwisho wake ingelikuwa ni sifa na kupigiwa makofi tu.
Wale wanaharakati wa kumkomboa mwanamke wangewasaidia hawa kwa kuwashauri wakihifadhi utu wao. Ni ukweli ulio wazi kuwa kitendo cha mwanamke mmoja kubaki uchi hadharani nikuwakashifu wanawake wote.
Kwa vile kimaumbile wanawake wote wanafanana, picha moja tu katika gazeti linalouzwa hadharani ingetosha kuwafanya wanawake wote walioumbwa na haya na wenye utu ku-react dhidi ya wachapishaji wa gazeti husika kwa sababu inawaabisha wote tangu wanawake wa kawaida mitaani, wanawake Wabunge na Mawaziri na hata wake wa viongozi wakubwa kabisa katika taifa. Hatujasikia hata siku moja "wanaharakati" wetu wakizungumza katika semina na makongamano yao au kuitisha maandamano kupinga hatua ya magazeti kumtumia mwanamke, tena aliye uchi kwa ajili ya kuuzia magazeti yao.
Ndiyo maana tunasema, tena kwa fakhari kabisa kuwa ukombozi wa kweli wa mwanamke unapatikana tu kupitia mafundisho ya Uislamu na si kwingineko. Ndiyo mafundisho pekee yaliyomfundisha mwanamke kuwa na haya, yakamuelekeza namna bora ya kuvaa kwa ajili ya kuhifadhi heshima yake aliyopewa na muumba wake na kupitia mafundisho hayo akaahidiwa malipo mema katika maisha yajayo.
Zuhra Tajiri, Shinyanga.
Hii ni heshima gani?
Ndugu Mhariri
NAOMBA wenzetu wa dini ya Kikristo watueleze, kutoa heshima kwa marehemu maana yake nini?
Baba wa Taifa kweli tulimpenda na tungependa kumuenzi kwa kila hali. Tatizo langu ni vipi tumpe heshima zetu za mwisho.
Uingereza Mwalimu alifunuliwa akaangaliwa, alivyotua Dar es Salaam pia. Kisha usiku na mchana siku mbili anaangaliwa na kila mtu.
Je, angekuwa hai angekubali awekwe hadharani mchana kutwa na usiku ule?
Maaskofu tuelezeni Biblia na sheria za Kanisa zinasemaje?
Farida Hamza,
Morogoro.
Historia itajirudia
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi japo kidogo nieleze machache juu ya juhudi za kujikomboa zinazofanywa na Waislamu hivi sasa kutoka katika makucha ya dhulma, ubaguzi na ukandamizaji wa kitabaka.
Kumekuwa na mengi yakisemwa na maadui wa haki. Wapo wanaodai Waislamu wanatumiwa, wengine wanadai hao ni wahuni wachache. Baadhi yao wamekwenda mbali zaidi na kudai kuwa hao wanahatarisha amani ya nchi na umoja wa kitaifa. Wapo wanaodai ni ukosefu wa ajira na kadhalika.
Mimi nasema wengi wayaseme lakini Waislamu tuzibe masikio na tuendelee kudai haki zetu na kuzinduka. Bora tufe tukipiga kelele bila kusikilizwa kuliko kufa kikafiri, kwa kudhulumiwa. Qur'an yatuambia: "Msidhulumu wala msidhulumiwe".
Hata wana TAA mwanzoni mwa harakati za ukombozi wa Tanganyika waliitwa wanywa kahawa kabla ya wavaa kaptula kuungana nao aktika mapambano dhidi ya mkoloni. Hatimaye wanywa kahawa wanakuwa mashujaa wa historia ya nchi yetu japokuwa kutokana na propaganda hili linafahamika kwa wachache. Tusife moyo subra, uvumilivu na imani ya kweli bila ya kusahau Qur'an (8:60) ni muhimu hivi sasa.
Mwalimu,
Morogoro.
Da'awa yahitajika Kisiju
Ndugu Mhariri
KISIJU ni tarafa iliyokuwa na Waislamu na Uislamu lakini hali hiyo haipo kwa sasa. Hali hii ya kutoweka kwa Uislamu katika eneo hili ni kwa kukosekana kwa ulinganiaji.
Kwa kupitia gazeti hili nayaomba mabaraza yote ya ulinganiaji kupanga ratiba za kuja Kisiju kuokoa jamii ya Kiislamu inayoangamia.
Pia hapa napenda kuiomba Kamati ya Wanawake Waislamu Tanzania ije kuokoa kizazi cha Kiislamu. Kwa sasa jamani hali ni ya kutisha, vazi la hijabu ambalo nyinyi wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla mnalipigania huku mabinti wanapokwenda kwenye Maulidi za kula ubwabwa wanavaa, lakini wakienda shule hawavai na shule zote za Kisiju watoto wote ni Waislamu lakin hakuna hijab hata moja. Shime Waislamu msilale mijini njooni Kisiju hali mbaya .
Salum Hamis,
Nasibugani - Kisiju.
Tutahadhari na uhuru wa vyombo vya habari
Ndugu Mhariri
KWA muda mrefu sasa televisheni huonesha tamthiliya inayoitwa TAUSI, kwa Muislamu yeyote mwenye chembe ya imani pindi akiiona tamthiliya hii atagundua kwamba lengo ni kuudhalilisha na kuutukana Uislamu.
Mwenyezi Mungu (s.w.) anatuelezea katika suratil Baqara, kwamba "..wala hawataacha kupigana nanyi mpaka wakutoeni katika dini yenu kama wakiweza...". (2:217)
Waislamu wenzetu wa Kenya waliipiga vita televisheni ya Kenya (KTV) wakati ilipokuwa ikionesha tamthiliya hii (TAUSI) mpaka wahusika wakaisitisha kuitoa hewani. Je, sisi Waislamu wa Tanzania tunairidhia tamthiliya hii na kama hatuiridhii mbona hakuna yeyote (si taasisi au mtu mmoja mmoja) aliyepinga kuoneshwa kwa igizo hili?
Pia Waislamu tutahadhari na magazeti ya kipuuzi ambayo hayana yanachokiandika zaidi ya masuala ya ngono na vichekesho ili kuiharibu jamii kimaadili na kifikra.
Hivyo Waislamu lazima tuwe makini tujinusuru sisi wenyewe na vizazi vyetu ili tusijeingia katika mtego wa makafiri.
Baruani Ally,
Dar es Salaam.
Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa
maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye
Baraza
ya Wasomaji
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |