Enyi waramba viatu!
Enyi waramba viatu, vibaraka ulamaa,
Nyoyo zimejaa kutu, uchu na nyingi
tamaa,
Unyama kusema utu, kulinda yasiyofaa,
Tenda hizo zenu tenda, tenda tumezing'amua.
Tenda zenu tenda, tenda tumezing'amua,
Mchukie mkipenda, mnune na kujiua,
Hata kama mkikonda, pande tunawaengua,
Sasa tushagutuka, enyi waramba viatu.
Enyi waramba viatu, vibandiko mlovaa,
Mjifanyao wenzetu, kusali nasi jamaa,
Kumbe muadi zetu, wabaya mwatuhadaa,
Tenda hizo zenu tenda, tenda tumezing'amua.
Tenda hizo zenu tenda, tenda tumezing'amua,
Vibaraza kuviunda, kuzuga kutuzuzua,
Mmebaki njia panda, hatuji tumegundua,
Sasa tumshagutuka, enyi waramba
viatu.
Enyi waramba viatu, vikao mnaoandaa,
Hizo mbinu sasa butu, ukweli zimechakaa,
Bure hampati kitu, hadhara twazikataa,
Tenda hizo zetu tenda, tenda tumezing'amua.
Tenda hizo zenu tenda, tenda tumezing'amua,
Ni punde mlituponda, na sumu kutumwagia,
Havijapona vidonda, mwarudi na kutujia,
Sasa tumeshagutuka, enyi waramba
viatu.
Enyi waramba viatu, tena hatutopumbaa,
Umoja na mbwa mwitu, hatuji tunaambaa,
Ujinga hatuthubutu, kuzugwa kama
vichaa,
Tenda hizo zenu tenda, tenda tumezing'amua.
Idd Kikong'ona,
Morogoro.
Sheikh Mbukuzi
Ya Illahi Ya Satari, Ya Illahi Ya
Azizi,
Ya Illahi Ya Qahari, tunakuomba
Mwenyezi,
Mpe maisha mazuri, ya furaha na
mbawazi,
Shekhe wetu Mbukuzi, Amiri wa Maimamu.
Amiri wa Maimamu, Shekhe wetu Mbukuzi,
Ya Illahi Ya Karimu, mwenye nguvu
na ujuzi,
Muondolee magumu, vikwazo na pingamizi,
Shekhe wetu Mbukuzi, Amiri wa Maimamu.
Mbukuzi ni Amiri, abishae mpuuzi,
Hakutwaa kiburi, amepewa hii kazi,
Kwa madhumuni mazuri, kwenye Shura
Kiongozi,
Shekhe wetu, Mbukuzi, Amiri wa Maimamu.
Uislamu ni kweli, Kitabu chasema
wazi,
Afatae neno hili, huonwa mtu bazazi,
Kweli anaebadili, kwa urongo ndo
mjuzi,
Sema kweli Mbukuzi, Amiri wa Maimamu.
Mwisho wa langu shairi, ama yote
simalizi,
Tunakuombea kheri, akili na utambuzi,
Katika dhidi subiri, kesho ukapande
ngazi,
Shekhe wetu Mbukuzi, Amiri wa Maimamu.
(Mshairi Bora)
Amiri A.S. Andanenga
(Sauti ya Kiza),
S.L.P. 4775, Kinondoni
Shamba,
Dar es Salaam.
Siafu wakaitana, kwa pamoja kujadili,
Sababu ya kukutana, kiongozi akakuli,
Mabanati na mabwana, twajifanyaje
vivuli?
Magumu tuyakabili, tulihami pango
letu.
Tulihami pango letu, magumu kuyakabili,
Ili tugombee chetu, kwa kila hali
na mali,
Kwa vipi urithi wetu, kwa kila hali
na mali,
Magumu tuyakabili, tugomboe pango
letu.
Joka lindani ya pango, Mungu alotufadhili,
Limetatiza mlango, kwa kuzinga mizingili,
Tuukubali mpango, wa kukabili kitali,
Magumu tuyakabili, tugomboe pango
letu.
Mkutano kwa umoja, hoja ukaikubali,
Kwa kuungwa ile hoja, joka likaona
kweli,
Mara siafu wakija, kifo kitamkutuli,
Likaona afadhali, liende kwenye
misitu.
Joka pango kaliacha, kwa kuhofu pilipili,
Siafu usiku kucha, mawazo wakibadili,
Joka limeshajificha, mafichoni huko
mbali,
Magumu walikabili, wakatwaa pango
lao.
Kama siafu waweza, wabaya kuyabadili,
Kuja yanayopendeza, nao wadudu dhalili,
Vipi! Sisi twajikwaza, watu tulo
na akili!
Magumu tuyakabili, tuipate haki
yetu.
Hima twende tusilale, msumeno pande
mbili,
Nyuma unga unga mbele, gogo hutengwa
kuwili,
Ishasemwa na wa kale, "haki" bei
yake ghali,
Gharama tuikabili, tuipate haki
yetu.
Si haki kudhulumiwa, kudhulumu si
halali,
Usiridhi kuibiwa, kuiba usikubali,
Bali chako kutopewa, kakitwae bilikuli,
Tamati katika hili, tuchukuwe "haki"
yetu.
(Mshairi Bora)
Amiri A.S. Andanenga
(Sauti ya Kiza)
S.L.P. 4775, Kinondoni
Shamba,
Dar es Salaam.
Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa
maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye
Baraza
ya Wasomaji
Kutoa
maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza
hapa
Au
Andika barua
kwa: webmaster@islamtz.org
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |