WATANZANIA wanajivunia kuwa na uhuru wa dini ambao unalindwa na Katiba ya nchi.
Anapokumbukwa Mwalimu leo ni pamoja na mchango wake katika kuujenga na kuimarisha uhuru huu.
Mtu kutupa haki yake ya kikatiba si kuonesha upendo kwa Mwalimu. Kuhofu mtu kuonesha msimamo wake katika dini ni alama ya kutokuwa huru, masikini wa mawazo na kutokujiamini.
Yote haya ni katika madhila yaliyotarajiwa yaondoke na mkoloni.
Na inaelezwa Mwalimu Nyerere katika uhai wake alipigania kuona watu wanaondokana na unyonge; kuwa na mawazo ya kufugwa na wasio na kauli hata katika yale mambo ya msingi yanayogusa uhai wao na utu wao.
Tathmini ya yaliyotuka baada ya msiba wa Mwalimu Nyerere yanaonesha kuwa wenye umaskini wa mawazo na akili za kushikiwa bado wapo. Lakini wako pia waliokwisha hitimu mafunzo ya hayati Mwalimu. Wanajua kwa nini watu walipigania uhuru, wanajua haki zao na uhuru wao katika imani.
Hao tuliwaona katika misa mbalimabli za kumuombea hayati Mwalimu Nyerere. Waliotaka kupiga magoti wakati wa "kulishwa chakula cha Bwana" (Eucharist) walinyimwa hata kama walikuwa wa kutoka familia ya hayati Mwalimu Nyerere. Wote walilazimika kufuata taratibu zilizowekwa na uongozi wa Kanisa Katoliki Dar es Salaam chini ya Kadinali Polycarp Pengo.
Hao ndio waliokombolewa na wanaojua haki zao na uhuru wao katika mambo ya imani.
Wapo ambao imani yao haiwaruhusu kuendesha "misa ya wafu" wasio katika imani yao. Lakini waliamua kutelekeza imani yao wakafanya kwa ajili ya Mwalimu.
Wako pia ambao dini yao inawaelekeza kuwa mtu akifa anatakiwa afanyiwe mambo manne na haraka azikwe. Akoshwe, akafiniwe, aswaliwe na azikwe. Kwao "heshima ya mwisho" kwa marehemu ni kumswalia baada ya kumkafini. Sio kumfunua na kumuweka hadharani kila mmoja akipita kumwangalia.
Hatuwezi kudai tunamuenzi Mwalimu Nyerere kwa kuvunja yale yanayoelezwa kuwa aliyapigania. Hatuwezi kumuenzi Mwalimu kwa kutupa haki za kikatiba. Si kumuenzi mtu umpendaye kwa kuhujumu yale aliyoyapigania.
Kama katiba inakupa uhuru wa imani na dini, na kama Mwalimu mwenyewe alitoa uhuru huo hata wa kuabudu miti; vipi mtu leo ushindwe kushiriki msiba wa hayati Mwalimu kwa kuzingatia sheria na taratibu za imani yako.
Wanamaombi ni Wakatoliki kama Wakatoliki wengine, lakini wapo waliokataa kulishwa "Chakula cha Bwana" hali ya kuwa wamesimama katika misa ya kumwombea Mwalimu.
Pamoja na mapenzi yao kwake hawakutaka kukiuka wanavyosadiki wao kwamba lazima "Chakula cha Bwana" kiliwe hali ya kupiga magoti. Hao ndio waliokombolewa na hao ndio walio na imani.
Lakini wapo wanaohitaji
ukombozi wa mara ya pili. Hao ni wale wanaodhani uzalendo wao na utii wao
kwa serikali utapimwa kutokana na jinsi wasivyoijali dini yao.
--
|
|